WAKATI ukitafakari hilo juu ya mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa jana, Azam kuna kocha Florent Ibenge na Singida Black Stars yupo Miguel Gamondi. Je wataweza kupindua utawala wa Simba na Yanga. Hao ni makocha wa daraja la juu na wapo kwenye timu zenye wachezaji bora kama ilivyo kwa Simba na Yanga.
Hapo ndipo pale inapofaa kutumia ule usemi usemao “acha inyeshe tuone panapovuja”, kwani mbali na rekodi ya kufungwa kwa bao la kwanza la msimu na nyingine za kawaida ambazo zimekuwa zikiwekwa kila msimu unapoanza, leo tuaangalie zile ambazo zimekuwa zikisumbua miaka na miaka je zitavunjwa?
Licha ya Simba na Yanga na kukutana kwenye Ligi ya Bara kwa miaka 60 tangu 1965, imeshuhudiwa hat trick moja tu iliyopigwa Jumanne, Julai 19, 1977.
Katika mechi hiyo, Yanga ilifungwa mabao 6-0 na Simba iliyokuwa inalipa kisasi cha 1968 ilipofumuliwa mabao 5-0 kwenye mechi iliyopigwa Juni Mosi. Mwaka 1977 Abdallah ‘King’ Kibadeni alifunga hat trick ambayo haijawahi kujibiwa na mchezaji yeyote hadi leo.
Licha ya kushuhudiwa mechi kadhaa za watani zikizalisha mabao mengi ikiwamo sare ya 4-4 kwenye mchezo uliopigwa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha 1996 na kipigo cha 5-0 ilichopokea tena Yanga katika mchezo uliopigwa Mei 6, 2012 hakuna mchezaji aliyefunga tena hat trick.
Kwa misimu ya karibuni, Max Nzengeli ni miongoni mwa wachezaji ambao walikaribia kuvunja rekodi hiyo Novemba 11, 2023 wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 5-1, lakini aliishia kufunga mwili.
Pamoja na kushuhudiwa wachezaji wakali wa kigeni na wazawa wakikipiga kwenye Ligi Kuu Bara kwa misimu kadhaa iliyopita, msimu huu kuna wadau waliamini ile rekodi ya mabao mengi katika msimu mmoja iliyowekwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ enzi akiwa Yanga itavunjwa, lakini wapii. Mmachinga aliyekipiga pia Bandari Mtwara, Simba, Mmbanga na Twiga Sports alifunga mabao 26 msimu wa 1998.
Kwa hesabu za haraka ni kwamba hadi sasa ni miaka 26 rekodi hiyo ya Mmachinga imeshindwa kufikiwa, japo msimu wa msimu wa 2006, straika aliyekuwa akikipiga Mtibwa Sugar, Abdallah Juma ‘AJ’ aliikaribia kwa kufunga mabao 25 na tangu hapo hakuna tena aliyewahi kuisogelea rekodi hiyo hadi leo.
Straika huyo wa zamani aliyeichezea Taifa Stars, pia alikuwa akishikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 153 katika misimu 13 kuanzia 1993-2005 kabla ya kuvunjwa na John Bocco aliyefunga mabao 156 katika misimu 17 tangu 2008-2025.
Nani anajua msimu ujao utakuwaje baada ya msimu uliopita nao kushuhudiwa rekodi ya Mmachinga ikishindwa kufikiwa kama ilivyokuwa ile ya Kibadeni ya kupiga hat trick kwenye Kariakoo Derby.
Meddie Kagere kwa sasa yupo zake Rwanda baada ya mwishoni mwa msimu uliopita kuachana na Namungo, lakini wakati anaondoka Msimbazi, nyota huyo aliweka rekodi tamu kwa mastaa wa kigeni katika Ligi Kuu Bara ambayo hata yeye mwenyewe ameshindwa kuifikia.
Kagere alitua Msimbazi kutoka Gor Mahia ya Kenya msimu wa 2018-2019 na kufunga jumla ya mabao 23 akiipiku rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Amissi Tambwe alipokuwa Yanga ya nyota wa kigeni kufunga mabao mengi kwenye msimu mmoja alipotupia 21 na kubeba kiatu 2015-2016.
Msimu wa pili kwa staa huyo, alifunga mabao 22 na kutetea tuzo ya Mfungaji Bora ikiwa pia ni rekodi kwani, haikuwahi kutokea kwa mchezaji yeyote iwe mzawa au wa kigeni kutwaa tuzo ya ufungaji mara mbili mfululizo. Simon Msuva akiwa na Yanga na Tambwe kama ilivyo kwa John Bocco ni wachezaji pekee tangu 2000 kuwahi kupata tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu mara mbili kwa misimu tofauti. Bocco alitwaa 2011-2012 enzi akiwa na Azam FC kisha akarudia tena 2020-2021 akiwa na Simba, wakati Tambwe aliinyakua 2013-14 akiwa Simba na kurudia 2015-2016 akiwa na Yanga, ilihali Msuva yeye alibeba 2014-2015 na 2016-2017, mara zote akiwa na Yanga kabla ya kuutwa Difaa El Jadida.
Juma Kaseja anashikilia rekodi ya kufunga mabao kwenye Ligi Kuu Bara, akiwa na mawili moja akifunga enzi akiwa na Yanga mwaka 2009 wakati wanaizamisha Toto Africans kwa mabao 2-1, kisha kurudia tena 2011-2012 wakati akiizamisha Simba ikiizamisha Yanga kwa mabao 5-0.
Kwa misimu kadhaa imeshuhudiwa makipa wakijifunga mabao na kuzinufaisha timu pinzani, lakini hakuna aliyejaribu kuipita rekodi ya Kaseja ya kuibeba timu yake kwa kufunga kwenye Ligi Kuu Bara.
Ally Yusuf ‘Barthez’ aliwahi pia kufunga kwenye Ligi Kuu mwaka 2016 wakati Yanga ikitoka sare ya 2-2 na Majimaji, huku Idd Pazi ‘Father’ akifanya hivyo kwenye Kariakoo Derby mwaka 1985 kabla ya Kaseja kumjibu 2012 na rekodi zao zimeendelea kudumu.