Masista wanne waliofariki ajalini Mwanza kuzikwa Dar

Mwanza. Masista wanne waliopoteza maisha katika ajali ya gari jijini Mwanza wanatarajiwa kuzikwa Septemba 19, 2025, Boko, jijini Dar es Salaam, huku dereva wao akizikwa Nyegezi, Mwanza.

Masista hao ambao ni Lilian Kapongo, aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Duniani na aliyekuwa Mshauri Mkuu na Katibu Mkuu wa shirika hilo, Nerina De Simone (Muitaliano), walifariki Septemba 15, mwaka huu baada ya gari lao kugongana uso kwa uso na lori.

Wengine ni Damaris Matheka (Mkenya), aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Bukumbi, Jimbo Kuu la Mwanza, Stellamaris Muthini aliyehudumu katika utume wa Kimisionari Kenya, pamoja na dereva wao Boniphace Msonola.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, ajali hiyo ilitokea saa 1:50 usiku katika kijiji cha Bukumbi, Kata ya Idetemya, Wilaya ya Misungwi, barabara ya Usagara-Kigongo Feri.

Masista hao walikuwa wakielekea Uwanja wa ndege wa Mwanza wakitokea Jumuiya ya Bukumbi kwa ajili ya safari ya kwenda Dar es Salaam.

Kabla ya ajali, walikuwa mjini Kahama, mkoani Shinyanga, kushiriki sherehe ya Nadhiri za Daima za masista wenzao watatu, hatua ya mwisho ya kujiweka rasmi katika maisha ya utume wa kudumu.

Ratiba ya mazishi iliyotolewa leo Septemba 17,2025 na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza inaonesha kesho Septemba 18, 2025, miili itawasili katika Kanisa la Epiphania Bugando jijini Mwanza.

Kisha, waombolezaji wataingia kanisani kabla ya Misa Takatifu kuanza saa 2:00 asubuhi na kumalizika saa 5:30 asubuhi.

Baada ya ibada, miili ya masista itapelekwa uwanja wa ndege wa Mwanza kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, huku mwili wa dereva ukipelekwa Nyegezi kwa ajili ya mazishi.

Taarifa hiyo imeeleza, misa ya mazishi ya masista hao itafanyika Septemba 19, 2025, kuanzia saa 4:00 asubuhi katika Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko, Dar es Salaam, ikifuatwa na ibada ya mazishi katika Kituo cha Kiroho cha Mtakatifu Teresa wa Avila, Boko.