Misafara ya bodaboda kwenye mikutano ya kampeni yazua mjadala

Dar es Salaam. Wiki ya tatu ya kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025 inapoyoyoma, taswira mpya imeendelea kujibainisha mitaani, vijana waendesha bodaboda wamegeuka kuwa injini ya hamasa na kivutio kikuu cha misafara ya kisiasa.

Makundi haya yamekuwa yakionekana kwa wingi barabarani, pikipiki zao zikipambwa kwa bendera na mabango ya wagombea wakisindikiza misafara na mikutano kwa vuvuzela, honi na maandamano.

Lakini swali linasalia, je, nguvu hii ya ushiriki itaakisi matokeo halisi ya kura siku ya uchaguzi, au itabaki kuwa sehemu ya shamrashamra za kampeni mpekee?

Swali hili linajibiwa kwa mitazamo tofauti, wapo wanaoona ushiriki huo unaleta mwamko mpya kwa vijana ambao awali haokuwepo, na hivyo kuhisiwa kuwa wanaweza kuchochea mwitikio chanya siku ya kupiga kura.

Lakini wengine wanaitazama hali hiyo kinyume chake, kwamba si rahisi kuongeza wapiga kura na wanatahadharisha kuwa ipo hatari ya mikutano kugeuka sherehe badala ya jukwaa la kunadi sera.

Pia, yapo maoni kwamba baadhi ya waendesha bodaboda wanashiriki misafara hiyo kwa sababu ya kifedha au zawadi wanazopata kutoka kwa wagombea, ikiwemo kujaziwa mafuta, fedha na fulana za vyama. Mitazamo hii inahoji iwapo hamasa hiyo ni ya dhati au inatokana na malipo.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Waendesha Bodaboda na Bajaji nchini, Said Kagomba alipozungumza na Mwananchi amefafanua dhana hiyo, akieleza kuwa bodaboda ni ajira rasmi na kinachofanyika ni sahihi.

Amesema bodaboda kukodishwa kwa ajili ya kuongoza au kuwa miongoni mwa vyombo vya moto kwenye misafara ya kampeni ni sehemu ya shughuli zao za kawaida.

“Bodaboda na bajaji ni ajira kama zingine. Ukiwa na chama unawahitaji, watakusafirisha. Ukiwa na sare au mabango watavaa au kuyabeba. Baada ya kazi wanarudi vituoni. Lakini pia wapo wanaoshiriki kwa imani ya kisiasa, si kwa sababu ya kulipwa pekee,” amesema Kagomba.

Waendesha bodaboda wenyewe wanasema wanajivunia nafasi hiyo katika kampeni. Hamis Abdul, mwendesha bodaboda kutoka Tandika, Dar es Salaam anasema:

Ni nafasi ya kuonyesha kuwa tunafuatilia na tunaweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu nani anafaa kuchaguliwa siku ya uchaguzi,” amesema.

Hata hivyo, Abdul anakiri kuwa ushiriki wa waendesha bodaboda kwenye kampeni za mwaka huu umeongezeka na kuibua mijadala.

Anasisitiza kuwa si wote wanaoshiriki kwenye misafara ni kwa sababu ya fedha au kwa sababu ya kujaziwa mafuta na wagombea, bali wengine wanajitokeza kutokana na mapenzi ya vyama wanavyoviunga mkono na wengine wanapenda tu kusikiliza sera za vyama na wagombea.

Selemani Mohamed, mwendesha bodaboda wa Buza anasema: Si kila bodaboda unayemuona kwenye kampeni anafuata pesa, wengine tunakwenda kusikiliza sera za wagombea tunaowapenda.”

Kwa upande wake, Peter Ali kutoka Tabata Segerea amesema ushiriki wao si ushabiki pekee, bali pia ni fursa ya kutangaza kazi zao na kupata wateja.

Bodaboda hatuendi tu kuchangamsha kampeni, tupo kazini. Tunapeleka wateja kwenye mikutano na mara nyingine hupata abiria wengi zaidi. Wanasiasa wanapotuona wasituone kama mapambo, bali waje na hoja za kutetea maslahi yetu,”amesema mwendesha bodaboda huyo.

Kwa upande wa pili, wanasiasa waliozungumza na Mwananchi wamesema mikutano ya kampeni inayoendelea nchini ni fursa kwa kundi la bodaboda, hivyo wasibezwe kwa kuwa wanajiingizia kipato.

Katibu wa Ilani na Uchaguzi wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Fahad Hassan Doyo, amesema: Ni kundi linaloguswa moja kwa moja na changamoto za kila siku, kuanzia ajira, usafiri hadi kipato cha kila siku. Ndiyo maana mara nyingi huonekana kwa wingi katika mapokezi ya kisiasa, kwani wana ushawishi na mshikamano mkubwa wa kijamii.”

Mtazamo huo umeungwa mkono na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano wa Chaumma, Ipyana Njiku aliyebainisha kuwa bodaboda ni kundi kubwa lenye nguvu ya kiuchumi na kijamii.

“Ni kweli misafara ya bodaboda imekuwa imeonekana kwa wingi mwaka huu ukilinganisha na mikutano ya kampeni katika chaguzi zilizopita. Ni kundi hai linaloonyesha mshikamano na uthubutu,” amesema Njiku.

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda akizungumzia hilo, amesisitiza kuwa pamoja na bodaboda kuwa kichocheo cha hamasa kwenye mikutano ya kampeni, uamuzi wa kura unategemea zaidi sera na haiba za wagombea.

Tafiti zinaonyesha mara nyingi ni watu wale wale wanaohudhuria mikutano kwa kubadilisha sare. Hivyo bodaboda huleta watu, lakini kura yake inategemea hoja na ubora wa mgombea,” amesema.

Dk Mbunda ameonya kuwa shamrashamra za misafara ya bodaboda zisigeuze kampeni kuwa maonyesho pekee, badala ya kuwa majukwaa ya kujadili hoja zinazohusu wananchi moja kwa moja.