MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA AENDELEA KUWAPIGA MSASA WANASIASA

Na; Mwandishi Wetu – Kilindi

Vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu nchini mwaka 2025,katika Jimbo la Kilindi vimetakiwa kufanya kampeni za kistaarabu ili kuendeleza utulivu na amani iliopo nchini.

Wito huo umetolewa na Afisa mwandamizi kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa Bi. Edna Assey katika kikao cha mafunzo na vyama vya siasa vyenye wagombea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, katika jimbo la Kilindi kilichofanyika tarehe 17/09/2025 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi.

“wakati wa kufanya kampeni zenu acheni sera ziongee” alisema Afisa mwandamizi Bi Assey na kuvitaka vyama vya siasa kunadi sera zao ili zieleweke kwa wananchi na kuacha kutumia maneno na vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha kuvunjika kwa amani na utulivu.

Aliongeza kusema kuwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ina majukumu mbalimbali ikiwemo kusimamia utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa sura ya 258 na kuvitaja vitendo vinavyokatazwa na sheria ya vyama vya siasa kuwa ni pamoja na Kunadi sera zinazopingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Katiba ya Zanzibar na Sheria nyingine za nchi, Kuunda kikundi cha ulinzi na usalama cha aina yeyote au kuwa na taasisi inayolenga kufanya majukumu ya jeshi la polisi au vikosi vingine vya ulinzi na usalama wa nchi.

Kuratibu,kuendesha au kufadhili mafunzo yeyote ya kutumia nguvu au silaha kwa wananchama wake au kwa mtu yeyote Kuhamasisha udini,ukabila na ukanda ,kuhamasisha kuvunjika kwa Muungano wa Tanzania au kuwa na lengo la kufanya siasa upande mmoja wa Muungano Vitendo vingine vinavyokatazwa na sheria ya vyama vya siasa ni kuruhusu au kuhamasisha matumizi ya nguvu kama njia ya kufikia malengo ya kisiasa.

Kuruhusu viongozi au wananchama wake kutumia maneno ya matusi,dhihaka,kashfa na uchochezi yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani Kupeperusha bendera ya chama,kufanya siasa au kufungua tawi katika maeneo ya kazi,shule,vyuo,ibada
,majengo ya serikali au umma Kutoa matamshi,kuandaa machapisho,kuharibu au kufanya kitendo chochote chenye dhamira ya kudhalilisha au kudhihaki bendera ya chama kingine na kufanya mikutano au maandamano bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Kwa upande wao viongozi wa vyama vya siasa Wilayani Kilindi waliipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi na kuomba kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya serikali na vyama vya siasa.