Kila rika huwa na mitindo yake ya maisha. Wakati fulani nilishuhudia wazee wetu wakivaa suruali pana na mashati ya kubana, wajomba na baba wadogo wakavaa mashati makubwa na suruali za kubana, sisi tuliokuwa wadogo tukavalishwa mitindo kwa kutegemea anayekuvalisha.
Tuliweza kujuana kuwa huyu kavalishwa shati la “puto” na mjomba au “slim fit” na baba yake. Hatukuwa na uwezo wa kuingia dukani na kujichagulia nguo kwa mapenzi yetu.
Siku hizi kila siku inakuja na mambo mapya. Mengine yalipata kuwapo siku za nyuma, lakini yanaibuka tena kwa sura au jina lingine.
Ni kama wavaavyo vijana wa sasa, wenyewe wanaziita “suruali za modo” wakati mjomba aliita “tinabuu”. Ni ileile ila ilitoweka na kurudi na jina jipya.
Nakubaliana na wajuzi wanaposema hakuna jipya chini ya jua. Mambo yote ni yaleyale ila yanajirudia yakiacha nafasi ya muda baina yao.
Kizazi kilichopo kinaweza kudhani kuwa huo ni ubunifu wao. Lakini ukweli ni kwamba hata kizazi hiki kitakapoondoka, utamaduni wao utabaki ukijitokeza katika vipindi tofauti katika vizazi nitakavyofuata.
Ni kama uongozi ulivyokuwapo tangu enzi na enzi. Kama kawaida, nao unatofautiana baina ya awamu na awamu kulingana na wakati.
Naweza kabisa kusema wakati huu umekuwa mgumu sana kutokana na mabadiliko ya kidunia. Niliwahi kumsikia babu akisema kwamba wakati wa ukame, watu walivuka mipaka kwenda kuwa manamba katika nchi za jirani.
Lakini walipoona neema ya mvua imerudi, nao wakarejea nyumbani. Tofauti ni kwamba matatizo ya sasa hayatakwisha. Kuna mabadiliko ya hali ya nchi, lakini tatizo limekuwa kubwa zaidi kutokana na aina ya maisha tuliyochagua.
Dunia ya sasa inakwenda kwa teknolojia, uhitaji wa binadamu kazini umekuwa mdogo kulinganishwa na mashine. Kila mtu amekumbwa na kadhia hii. Dunia imekumbwa na ukame wa ajira, na mzunguko wa pesa umezidi kupungua. Hivyo mtu mmoja mmoja anajaribu kwenda kutafuta maisha katika nchi za jirani.
Tumesikia jinsi raia kutoka mataifa mbalimbali wanavyokamatwa katika jitihada zao za kuingia Marekani.
Kwa sasa, biashara kubwa haramu inayosumbua zaidi ni usafirishaji haramu wa binadamu (human trafficking).
Kwa nini mtu anaamua kuzamia ugenini ilhali dunia nzima imeathirika? Sababu zipo nyingi zikiwamo za “mfa maji” asiyeisha kutapatapa.
Yeyote anaweza kudhani kuwa kubadilisha maisha kunaweza kumpatia ahueni. Lakini inawezekana nchi yetu ikawa inapokea wageni wengi zaidi ya wenzetu. Hii ni kwa sababu ya umakini wetu juu ya wageni si mkubwa sana. Mara nyingi tunawafanya “wajisikie kuwa nyumbani.”
Kumbuka mtu yeyote anapotafuta fedha ugenini, anaweza kujituma kuliko anavyotafutia nyumbani. Kama unakumbuka tuliwahi kuwa na wasomi wenye shahada za uzamivu kutoka Nigeria.
Walikuwapo hapa nchini wakifanya uchuuzi na hata kazi zingine duni ukilinganisha na elimu zao. Walithibitisha kuwa mtafutaji (hasa ugenini) habagui kazi; “mchagua jembe si mkulima” na “jiko la shamba halichagui kuni”. Nao walitimbika bila kujali nani anawacheka.
Katika sakata hili, tunaona jinsi raia wa kigeni wanavyojitahidi kuhemea hapa nchini. Kila siku malori ya Polisi na Idara ya Uhamiaji yanakamata raia wa kigeni wanaoingia nchini kinyume na utaratibu.
Si ajabu hata huko kwao wanawakamata vijana wetu kwani ni tatizo la kiulimwengu. Lakini mimi naamini kuna sababu maalum zinazowavutia wageni hapa kuliko katika nchi zingine. Hiki ndicho hasa kiini cha mazungumzo yetu ya leo.
Wafanyabiashara waliopata kwenda China na Marekani wanatusimulia jinsi wenzetu walivyo makini katika sera zao za biashara.
Wafanyabiashara wamewekewa madaraja tofauti ya leseni kutokana na uraia. Kuna leseni haziruhusiwi kwenye baadhi ya maeneo, pia tofauti ya leseni za wageni na wazawa.
Katika nchi hizo wageni wanawekewa mipaka ili wasiathiri maisha ya wazawa. Hapa kwetu panaonekana kuwa na udhibiti mdogo na ndio maana tunaona mafuriko ya wageni kutoka kila kona.
Rais ajaye apange mikakati ya kudhibiti uhuru wa biashara za wageni.
Kwanza atazame sana biashara na huduma zinazoweza kugusa afya za Watanzania moja kwa moja kama chakula na dawa. Mgeni anayejali kuvuna utajiri akiwa ugenini anaweza kutojali maisha ya wenyeji.
Lakini pia hii ni tahadhari dhidi ya vita ya silaha za kibaiolojia. Vita hii ni mbaya kuliko ya mabomu ya mlipuko. Biashara ndogondogo kama mama lishe, wamachinga waachiwe wazawa kwani ndio uwezo wao ulipo.
Njia hii inaweza kupunguza ukali wa tatizo la ajira. Wageni washiriki kuwekeza kwenye biashara kubwa tu, kama hawawezi basi wakafanye umachinga makwao. Wakiachiwa kuendesha saluni wanaweza kupotosha mila na desturi zetu kwa kuongeza huduma za masaji na majosho ya utupu (sauna).
Mwisho ni lazima Serikali isimamie moja kwa moja biashara za mipakani. Mipaka ni moja ya malango makuu ya kuingilia nchini.
Wageni wakijiachia na biashara za hapo, kuna hatari ya kutorosha raslimali za Taifa. Pia wanaweza kuachia mianya kwa maadui. Adui anaweza kupenyeza silaha katika vifungashio vya bidhaa halali kama samani na vyombo vya ndani. Biashara za mipakani ziwekewe udhibiti sawa na viwanja vya ndege na bandari.