Nyuki wa Tabora wamepania kung’ata zaidi msimu huu

TAYARI Tabora United inafahamu ladha tamu na chungu za Ligi Kuu Bara kutokana na kushiriki michuano hiyo kwa misimu miwili na sasa inakwenda wa tatu.

Katika msimu wa kwanza 2023-24, timu hiyo iliponea chupuchupu kushuka daraja baada ya kushinda michezo ya mtoano kufuatia kumaliza katika nafasi ya 14 kati ya timu 16, hilo likawafanya viongozi msimu wa 2024-2025 kuja kivingine katika kuiboresha timu, ikafanikiwa kumaliza nafasi ya tano.

Kutoka nafasi ya 14 hadi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikawapa jeuri viongozi wa klabu hiyo na kusema msimu huu, nne bora inawahusu. Kwa kifupi, timu hiyo maarufu kwa jina la Nyuki wa Tabora, imepania kuwang’ata zaidi wapinzani uwanjani.

Akizungunza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Charles Obiny, anasema wakati wanajiandaa na msimu huu, msisitizo mkubwa ulikuwa katika kuimarisha kikosi chenye ushindani zaidi.

Kiongozi huyo raia wa Kenya, anasema uimara wa kikosi chao utafanya kufikia malengo waliyojiwekea.

“Ligi inaanza na kama unavyofahamu msimu uliopita tulimaliza katika nafasi ya tano, safari hii tunaitaka nafasi ya juu zaidi ya hapo, kila timu huwa na malengo na hayo ndio malengo yetu,” anaanza kusema kiongozi huyo.

Obiny amebainisha kuwa, hata usajili walioufanya umelenga kufikia hayo malengo, hivyo anaamini hakuna kinachoshindikana.

“Kuna wachezaji wameondoka hivyo lazima tufanye usajili kuziba hayo mapengo, tunaamini hawa tuliowasajili watatufikisha kule tunakotaka,” anasema Obiny.

Timu hiyo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kukusanya pointi 38 ikishinda michezo kumi 10 kati ya 30, sare minane na kupoteza 12.

Miongoni mwa wachezaji walioondoka Tabora United ni Heritier Makambo, Offen Chikola, Andy Bikoko na Nelson Munganga ambao walikuwa wakiunda kikosi cha kwanza.

Maboresho ya kikosi hicho yamefanyika kwa kushusha wachezaji wanaoaminika wanaziba nafasi za walioondoka. Baadhi yao ni Shaban Chilunda, Adam Adam, Abdulaziz Makame, Nnanna Churchil, Chewe Chanda na Palai Mba Manjie.

“Usajili tulioufanya ulilenga mahali ambapo tumekuwa na upungufu. Ukiangalia tumejiimarisha kwa ajili ya kufanya vizuri msimu huu.

“Kama unavyokumbuka tulimaliza msimu uliopita tukiwa katika nafasi ya tano. Hivyo tunataka kufanya vizuri zaidi ya vile tulivyofanya msimu uliopita.

“Hizo zipo kila mahali, sana sana changamoto ni umbali wa kusafiri. Ukiwa na mechi katikati ya wiki na wikiendi inawachosha sana wachezaji.

“Inatokea mechi wikiendi hadi wikiendi hapo unakuwa na muda wa kupumzika sana, lakini wakati mwingine unacheza leo kisha kesho uko njiani kwenda kituo kingine cha mechi, hiyo ndiyo inachosha sana.”

Msimu uliopita, Tabora United ilifundishwa na makocha wanne, ilianza msimu na Mkenya Francis Kimanzi, akafuatia Mkongomani Anicet Kiazayidi, kisha Mzimbabwe Genesis ‘Kaka’ Mangombe, akamalizia Mzambia, Simonda Kaunda ambaye bado yupo hadi sasa.

Simonda anasaidiana na Thomson Sakapaji, huku Khalfan Mbonde akiwa kocha wa makipa na daktari ni Francis Mhagama.

“Tunaamini benchi la ufundi tulilonalo linaweza kufanya vile ambavyo tumepanga, yaliyotokea msimu uliopita hatutarajii yatokee tena kwani kubadilisha makocha si kitu kizuri kwa timu yenye malengo.

“Msimu uliopita tungeweza kufika mbali zaidi ya pale, lakini changamoto tulizokutana nazo zimetufanya tumalize nafasi ya tano ambayo si mbaya sana kwetu.

“Wanatabora kikubwa watafurahia mpira mzuri kutoka katika timu yao na hatutawaaibisha,” anasema Obiny.

Ratiba ya Ligi Kuu Bara 2025-26 inaonyesha Sept 20, 2025 Tabora Utd itaanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kukabiliana na Dodoma Jiji.

Kuhusu kuanza kwa ligi, Kocha Simonda ameliambia Mwanaspoti kuwa: “Tumekuwa na maandalizi mazuri ikiwemo kushiriki mashindano maalum ya pre-season yaliyofanyika Babati, tumecheza dhidi ya timu ambazo tutakuja kucheza nazo ligi kuu.

“Kikosi kipo tayari kuanza kwa ligi huku tukiwa na malengo ya kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita.