Pemba. Hatua ya Jimbo la Kojani la Mkoa wa Kaskazini Pemba kuzungukwa na maji, haikumzuia mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman kulifikia kwa ajili ya kuomba kura.
Othman ametumia usafiri wa mtumbwi (fiber boti) kutoka Likoni hadi Kojani Kisiwani, safari yenye umbali wa takriban dakika 20. Baada ya kushuka aliwasalimia na kuwaomba kura wakazi wa Kojani wilayani Wete waliojitokeza kumlaki.
Mgombea huyo, yupo katika kampeni za siku nne kisiwani Pemba katika kusaka kura zitakazomhakikishia ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025.
Akizungumza leo Jumatano Septemba 17,2025 kwa nyakati tofauti na wakazi wa Kojani, Othman amesema hatua ya kutembelea kisiwani hicho ni mahsusi kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuwapa matumaini ya mabadiliko.

Akizungumza kwenye uwanja wa Kambini Kichokochwe Jimbo la Kojani Mkoa wa Kaskazini Pemba, Othman ameahidi kuwa endapo akishika madaraka uongozi wake utakuwa wa vitendo, sio maneno.
Amesema akiapishwa kushika dola ataweka mifumo madhubuti ya haki, ajira kwa vijana, huduma bora za kijamii na fursa za kiuchumi zinazowagusa wananchi wote bila ubaguzi.
“Huu ni mwaka wa mabadiliko ya kweli na wa kuinusuru Zanzibar na kuitoa mikononi mwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Mkinipa ridhaa ya kuwa Rais wenu, nitarudi hapa Kojani ili nisikie kutoka kwenu mambo yote mnayohitaji,” amesema Othman huku akishangiliwa.

Katika maelezo yake, Othman amesema wananchi wa Kojani Pemba wana haki sawa kama Wazanzibari wengine hivyo, atahakikisha anaboresha mazingira na kuwapelekea maendeleo.
“Naamini watu wa Kojani wanahitaji haki sawa na raia wengine wa Zanzibar, nitahakikisha zinapatikana,”amesema Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Mmoja wa wananchi wa Kojani, Salum Mbarouk Juma amempongeza Othman kwa hotuba yake na kuahidi kumpa ridhaa Oktoba 29 ili kupata kiongozi mpya atakayeijenga Zanzibar.
Juma amemweleza Othman kuwa wanakabiliwa ukosefu wa maji safi na salama, ajira, vyombo duni vya uvuvi visivyoweza kushindana na mazingira ya kisasa na ugumu wa maisha.

Akijibu kilio hicho, Othman amewaahidi kuleta mapinduzi ya kweli ya kiuchumi na kijamii pindi atakapopata ridhaa ya kuongoza Zanzibar.
“Nikichaguliwa kuwa Rais, nitahakikisha tunatengeneza miundombinu mbadala ya maji, tutaondoa ubaguzi katika ajira, tutawapatia vijana fursa za kazi na kuwawezesha wanawake kiuchumi,” amesema Othman.
Katika mkutano wa hadhara Othman uliofanyika Uwanja wa Kambini Kichokochwe Kojani, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa amewataka wananchi wa Pemba kujiandaa na ushindi Oktoba 29.

“Uzuri wenyewe ACT Wazalendo huwa hatusafirishi watu, lakini kama mtu una kidau (mtumbwi) au meli, hakikisha upo Unguja ukishuhudia tukimwapisha Othman Masoud Othman atakayeweka historia.”