TIMU za Polisi na Uhamiaji, zitafungua dimba la Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2025-2026 baada ya ratiba kutangazwa rasmi.
Ratiba hiyo iliyotangazwa na Bodi ya Ligi Zanzibar, inaonesha mechi zitaanza kuchezwa Septemba 20, mwaka huu ambapo Polisi itakuwa mwenyeji wa Uhamiaji kwenye Uwanja wa Uwanja Mao A uliopo Unguja, saa 10:15 jioni.
Katika ratiba hiyo, raundi ya kwanza itakuwa na mechi nane, huku KMKM na Mlandege zikishuka dimbani Oktoba 3, 2025 baada ya kukamilisha mechi zao za kimataifa hatua ya awali. Kumbuka Mlandege inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na KMKM ipo Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya mchezo huo wa kwanza, ligi hiyo itaendelea Septemba 21, mwaka huu kwa kuchezwa mechi mbili, Junguni itaikaribisha Zimamoto kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba na Mwembe Makumbi itacheza dhidi ya New King, Uwanja wa Mao A, zote zikichezwa saa 10:15 jioni.
Septemba 22 pia kutapigwa mechi mbili, Chipukizi dhidi ya Malindi kwenye Uwanja wa Gombani na JKU ikiikaribisha KVZ kwenye Uwanja wa Mao A. Kisha Septemba 23, ni Mafunzo dhidi ya New Stone Town kwenye Uwanja wa Mao A na Kipanga dhidi ya FFC, Uwanja wa Mao B.
Ligi hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Mei 31, 2026, bingwa mtetezi ni Mlandege.