Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kuongeza bajeti ya ununuzi wa bidhaa za afya, Bohari ya Dawa (MSD) na watumishi katika sekta ya famasia wameagizwa kusimamia kwa usahihi mnyororo wa ugavi wa bidhaa hizo, ili kuleta tija kwa wananchi ikiwamo kupata huduma bora bila manung’uniko.
Hayo yamesemwa leo Jumatano, Septemba 17, 2025 na Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte wakati akifungua kikao kazi kati ya MSD na wadau kilicholenga kujadili na kubaini changamoto zilizojitokeza katika mnyororo wa ugavi.
Mhinte amewaagiza wadau hao kujadili na kuona namna ya kufanya maboresho ya kimifumo na kiutendaji kwenye maeneo yenye changamoto.

Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Rajab Mhinte akizungumza wakati akifungua kikao kazi kati ya MSD na wadau wa Mkoa wa Dar es Salaam kilicholenga kujadili, kubaini na kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika mnyororo wa ugavi.
“Serikali ya Samia Suluhu Hassan imeendelea kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya bajeti ya kununua bidhaa za afya na kuboresha utendaji wa huduma za afya, kila mmoja wetu ana jukumu la kusimamia kwa usahihi ili kuleta tija kwa wananchi.
“Wenyewe mmesema hamuidai Serikali, hivyo timizeni wajibu wenu wa kufikisha huduma kwa wananchi kwa juhudi kubwa,”amesema.
Ametumia fursa hiyo kuvikumbusha vituo vya huduma za afya Mkoa wa Dar es Salaam vifanye maoteo kwa wakati na kwa usahihi ili kuwezesha MSD kuandaa bidhaa za afya kwa kadri ya mahitaji ya mkoa.

Akitoa salamu za MSD, Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji, Victor Sungusia amesema kwa sasa fedha zipo kwani 2020 walikaa mwaka mzima bila kupatiwa fedha, lakini sasa fedha inaletwa hivyo taasisi hiyo inapaswa kufanya kazi ya ziada kufikisha huduma kwa wananchi.
“Alipoingia Rais Samia tukaanza kuona mabadiliko mpaka mwaka jana tumepata fedha yote ya dawa, ukiangalia bajeti ya mwaka huu wa fedha imeongezeka kutoka Sh200 bilioni mpaka Sh300 bilioni.” “Tumeshamaliza miezi miwili Julai na Agosti fedha zote tumeshapata kwa sasa tunasubiri fedha ya Septemba,” amesema.
Sungusia amesema bila kukaa na wadau na kuzungumza hawawezi kusonga, tangu mabadiliko yamefanyika wapo tofauti kazi yao ni kuhakikisha wanapata bidhaa za afya, kipimo chao kikuu ni uwepo na bidhaa na mteja ameagiza kiasi gani na iwapo amepata huduma.
“Maboresho haya tumetoka kwenye upatikanaji wa dawa wa asilimia 54 mpaka asilimia 74 ni hatua kubwa. Baada ya maboresho tukagundua hatuna akiba ya kutosha, magari hayatoshi hivyo tukifika lengo itakua shida, tumeanza kuongeza kwenye utunzaji, uhifadhi na tunaendelea,” amesema Sungusia.

Amesema MSD bado wanaendelea kuboresha mifumo, hivyo amewaomba wadau hao kutoa mrejesho ili waweze kufanyia kazi changamoto zilizopo na kufanya maboresho zaidi.
Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Betia Kaema amesema kwa sasa taasisi hiyo imeanza kusambaza bidhaa mara sita kutoka mara nne ya awali, na wanahakikisha changamoto zote zinazoathiri mnyororo wa ugavi zinashughulikiwa.
Mfamasia kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Magreth Lali amesema sasa wapo kwenye kufanya maoteo ya bidhaa za afya watakazozitumia mwaka 2026/2027.
“Ningeshauri iboreshwe mifumo kusomana kuanzia mapokezi kwa daktari mpaka anapokwenda kuchukua dawa, isomane mpaka kwenye mfumo unaotumika na MSD kwa maana itakuwa rahisi kupata taarifa za bidhaa za afya hata tunapofanya maoteo tunaongeza kwa kiasi kidogo tukiamini mwaka ujao mahitaji yataongezeka,” amesema.
Mfamasia wa Manispaa ya Kinondoni anayeshughulikia upatikanaji wa bidhaa za afya, Oswin Sanga amesema ni vema kuwe na maboresho eneo la mifumo ikiwamo mawasiliano kati ya MSD na washitiri.