Sh3 milioni zamweka matatani Mtendaji wa kijiji Simanjiro

Simanjiro. Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruvu Remit wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Godbles Mollel amefikishwa mahakamani kwa kosa la rushwa kwa kutumia Sh3.3 milioni isivyo halali.

Mollel amesomewa shitaka hilo la uhujumu uchumi leo Septemba 17, 2025 mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Onesimo Nicodemo.

Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Faustin Mushi akisoma hati ya mashitaka amesema Mollel amefanya kosa hilo akiwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruvu Remit.

Mushi ameeleza kwamba Mollel amefanya ubadhirifu wa fedha za kijiji hicho Sh3.3 milioni ambazo zilikuwa chini yake kutokana na nafasi yake.

Ameeleza kuwa mshtakiwa huyo amefanya makosa hayo ya ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 (1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 329 R.E 2822

Ameieleza mahakama hiyo kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu hicho pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza Kifungu cha 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi pamoja na ya kupanga sura ya 200 R.E.2022.

Mwendesha mashtaka huyo amedai kuwa mshtakiwa Mollel amefanya kosa hilo la wizi akiwa mtumishi wa umma kinyume na vifungu vya 258 na 270 vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 R.E 0202.

  Mollel amekana kutenda kosa hilo na yupo nje kwa dhamana baada ya kukidhi vigezo kwa kuwa na wadhamini wawili walioweka bondi ya Sh2 milioni

Hakimu Nicodemo ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 25, 2025 kwa ajili ya kusikilizwa kwa hoja za awali (PH).