Uzuri wa Tanzania Kupitia Sanaa, Vivo Energy Yazindua mashindano ya Awamu ya pili kwa shule za Sekondari na Vyuo nchini

Katibu Mtendaji, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana katikati akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Jangwani wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Sanaa ya Uchoraji kuelezea uzuri wa Tanzania, uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam Septemba 16, 2025.

Wnafunzi wa shule ya Sekondari Jangwani wakionesha utaalamu wao katika kuelezea uzuri wa Tanzania wakati wa Uzinduzi wa Mahindano jijini Dar es Salaam Septemba 16, 2025.

Mkurugenzi wa Vivo Energy Tanzania, Mohamed Bougriba akichora wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Uzuri wa Tanzania.

*Vivo Energy Yajikita Katika Maendeleo ya Elimu, Afya na Mazingira

Na Avila Kakingo, Michuzi Blog

KAMPUNI ya Vivo Energy Tanzania imeonyesha dhamira yake ya dhati katika kuunga mkono maendeleo ya jamii kwa kuwekeza katika sekta tatu muhimu: elimu, afya, na mazingira. 

Dhamira hiyo ilielezwa jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mashindano ya Sanaa ya Uchoraji kwa wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo nchini, yenye lengo la kuonesha uzuri wa Tanzania kupitia sanaa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Vivo Energy Tanzania, Mohamed Bougriba, alisema kuwa mchango wa kampuni hiyo hauishii tu kwenye biashara, bali pia unalenga kuleta mabadiliko chanya kwa jamii ya Watanzania.

“Mwaka jana tulizindua mashindano haya kwa mafanikio makubwa hapa Dar es Salaam. Mwaka huu, tumeamua kupanua wigo wake hadi kufikia miji mikuu na maeneo mbalimbali nchini, tukilenga kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kuonesha vipaji vyao,” alisema Bougriba.

Aidha, alitoa pongezi kwa wadau mbalimbali waliotoa msaada na kushiriki katika safari hiyo ya maendeleo, akibainisha kuwa mafanikio ya mradi huu ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na jamii.

Kwa mujibu wa Bougriba, kupitia mashindano haya ya Uzuri wa Tanzania, kampuni inalenga kuwawezesha vijana kuonesha utamaduni wao, mandhari ya taifa, na kutumia sanaa kama njia ya kueleza fahari ya Tanzania na urithi wake kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Bona Masenge, Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa za Ufundi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), alisema kuwa baraza hilo linaendeleza juhudi za kukuza vipaji vya vijana katika sanaa, hasa uchoraji, tangu wakiwa wadogo.

“Mashindano haya yanawajenga vijana kuwa wazalendo, kuipenda na kuitumikia nchi yao kwa fahari. Kupitia sanaa, wanaweza kuelezea uzuri wa Tanzania kama vile usafi, afya ya mazingira, na uzuri wa mandhari ya asili,” alisema Bona.

Bona aliongeza kuwa mradi huo umeunganisha taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali katika kuandaa vigezo bora vitakavyotumika kumpata mshindi wa mashindano hayo.

Kwa upande wake, Liliani Hipolyte Mushi kutoka Nafasi Art Space alifafanua kuwa mashindano hayo yatashirikisha shule zote za sekondari na vyuo nchini, huku wanafunzi wakiruhusiwa kutumia mbinu yoyote ya kuchora iwe kwa mikono au kutumia vifaa vya kielektroniki kama kompyuta.

Liliani alieleza kuwa michoro inaweza kuwasilishwa kwa njia ya kawaida au kwa njia ya mtandao kupitia vituo maalum kama vile Shule ya Sekondari Jangwani, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Mwanza, Mtwara, na maeneo mengine yatakayoainishwa kupitia tovuti rasmi ya Vivo Energy.

Tarehe ya mwisho ya kukusanya michoro hiyo itakuwa mwisho wa mwezi Oktoba 2025, na washindi watazawadiwa fedha taslimu pamoja na vifaa vya shule kama Laptop na iPad.

Kwa upande wa Mkuu wa Shule ya Sekondari Jangwani, aliishukuru Vivo Energy kwa mchango wao wa kujenga barabara ndani ya shule hiyo kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, hasa wanaotumia viti mwendo.

 Alitoa wito kwa kampuni hiyo na taasisi nyingine kuendelea kusaidia mahitaji ya wanafunzi hao, ikiwemo usafiri wa kuwapeleka hospitali, sehemu za ibada, na kwenye shughuli za michezo.

Nao wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jangwani walieleza furaha yao kwa kuchaguliwa kuwa sehemu ya uzinduzi wa mashindano hayo, na kushukuru kwa miundombinu waliyojengewa, ambayo inaboresha hali ya kujifunza kwa wanafunzi wenye ulemavu.