Tanga. Maandalizi ya mazishi ya miili mitano ya watu wa familia moja waliofariki dunia kwenye ajali ya gari Septemba 13, mkoani Pwani yanaendelea mkoani Tanga, ambapo ibada itafanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), lililopo Donge.
Akizungumza na Mwananchi kwenye eneo la msiba uliopo maeneo ya Magaoni jijini Tanga leo Jumatano Septemba 17,2025 mdogo wa marehemu Dismas Kaggi amesema ratiba ya ibada itafanyika katika Kanisa ya Kiinjili la Kilutheri Tanzania liliopo maeneo ya Donge.
Amesema ibada ya awali itaanzia nyumbani kwa ufupi na baadaye waombolezaji wataelekea kanisani, itakayofanyika ibada kubwa ya mwisho katika kuwaombea marehemu hao kabla ya kwenda makaburini.
Amesema baada ya ibada waombolezaji wataelekea makaburini Kange ambapo ndio yatafanyika mazishi.
“Tunatarajia walau kuwa na ibada fupi kwa ajili ya kuiaga miili kisha tunakwenda kanisani ambako itafanyika ibada ndefu, baada ya ibada tunakwenda makaburini kuzika na huo ndio utakuwa mwisho wa safari ya maisha yao,”amesema Kaggi.
Amesema familia imeweka utaratibu maalumu wa usafiri kwa wote watakaotaka kushiriki mazishi kuanzia kwenda kanisani na baadaye kwenye Kange, hivyo kila ambae atajaaliwa kuhudhuria anaweza kwenda kusindikiza miili hiyo.

Bado wananchi wanaendelea kuwasili msibani hapo na miili imehifadhiwa ndani kwa ajili ya taratibu za ibada, na kupelekwa kanisani.
Ajali hiyo iliyotokea Septemba 13,2025 mkoani Pwani na kusababisha vifo vya watu watano ambao ni baba wa familia Francis Kaggi na watoto wake watatu na mmoja wa kumlea, ambapo mkewe aliyekuwa pamoja na marehemu kwenye gari alinusurika.