Kigoma. Wagombea ubunge wa majimbo ya Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Kigoma, kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria na taratibu za uchaguzi.
Wagombea hao wametoa kauli hiyo leo, Jumatano Septemba 17, 2025, mjini Kigoma, baada ya kushiriki mafunzo yaliyotolewa na Takukuru kuhusu sheria za uchaguzi, ambapo walikumbushwa kuhusu makosa ya rushwa na adhabu zake.
Mafunzo hayo yamewahusisha wagombea ubunge kutoka vyama 19 vya siasa mkoani humo.
Wakizungumza baada ya semina hiyo, wagombea hao akiwamo mgombea ubunge wa Kigoma Kaskazini kupitia chama cha ACT Wazalendo, Kiza Mayeye, amesema kuwa kila uchaguzi kunajitokeza tuhuma nyingi za rushwa kati ya wagombea na wananchi, lakini hatua madhubuti hazichukuliwi.
“Nashauri uchaguzi wa mwaka huu, Takukuru iwe macho, ifuatilie mwenendo wa uchaguzi ili kuhakikisha unakuwa huru na wa haki. Pia, waangalie uwepo wa kura feki na wachukue hatua bila upendeleo wa chama chochote, kama kweli wanataka kuimarisha demokrasia.
Naye Mgombea ubunge Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya CUF, Kashimbi Adam amesema licha ya kuwa Takukuru ina mamlaka na uwezo wa kuchukua hatua, bado haijaonekana kutumia rasilimali hizo ipasavyo, hali ambayo inatuma ujumbe wa uwepo wa upendeleo kwa baadhi ya vyama vinavyotuhumiwa kujihusisha na rushwa.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Kigoma Mjini kupitia chama cha NLD, Aisha Ramadhani, amedai kuwa vitendo vya ugawaji wa fedha, baiskeli na bidhaa nyingine vimekuwa vikiendelea waziwazi, lakini hakuna hatua zinazoonekana kuchukuliwa na Takukuru.
Mwanasheria wa Takukuru Mkoa wa Kigoma, James Nyarobi amesema amewapa wagombea wa ubunge katika vifungu mbalimbali vya sheria vinavyohusu uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, hususan vinavyohusiana na makosa ya rushwa.
“Tumepitia Sheria Na. 1 ya Mwaka 2024, Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na marekebisho yake, na pia Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Sheria zote hizi zimeweka makatazo ya wazi dhidi ya vitendo au viashiria vya rushwa wakati wa kipindi cha uchaguzi,” amesema Nyarobi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kigoma, Asha Mwariko, amesema lengo la kuwakusanya wagombea hao ni kuwakumbusha masharti ya kisheria kuelekea uchaguzi mkuu, huku akisisitiza umuhimu wa kuendesha kampeni kwa nidhamu na amani.