Wasira: Wagombea msibweteke kaombeni kura kwa wananchi

Mbeya. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema hakuna mgombea aliyepita bila kupingwa, na amewataka wagombea wa chama hicho kuendelea kusaka kura kwa wananchi nyumba kwa nyumba.

Amesema lengo la kusaka kura ni   kuhakikisha ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 unapatikana.

Wasira ametoa kauli hiyo leo, Jumatano, Septemba 17, 2025,  baada ya kuwasili katika Ofisi za CCM Mkoa wa Mbeya, ambapo amepokewa na viongozi mbalimbali akiwamo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa.

Akizungumza na wanahabari nje ya ofisi za CCM kabla ya kuingia kwenye kikao cha ndani, Wasira amesema ziara yake mkoani Mbeya inalenga kufahamu hali ya kisiasa na maandalizi ya uchaguzi, kwa kuwa huu ni mwaka muhimu kwa chama na Taifa kwa ujumla.

“Nimefika  kukutana na kamati ya siasa  mkoa  hakuna kupoa wala kulala,  kwani  baadhi ya majimbo tunakutana na viongozi  wote wa matawi na kata ili tupeane majukumu namna ya kushinda sio kushindwa,” amesema.

Makamu Mwenyekiti  CCM Bara, Stephen  Wassira  akisalimiana na mgombea mteule  viti maalum Mkoa wa Mbeya  Maryprisca  Mahundi  mara baada  ya kuwasilisha  katika  Ofisi  za Chama. Picha na Hawa Mathias

Amesema huu ni mwaka wa uchaguzi  wagombea   ubunge, udiwani waende wakasake kura kwa wananchi kwani  hakuna mgombea aliyepita bila kupigwa.

Wasira, amewahimiza wanawake ndani ya CCM kuendelea na kampeni za nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anashinda kwa kishindo.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Nsalaga (Uyole), Clement Mwandemba, amesema wamepokea kwa mikono miwili maelekezo yaliyotolewa na Wasira na  wapo tayari kutekeleza wajibu wao kwa bidii.

“Tumepokea  maelekezo   tumetakiwa kwenda kusaka kura usiku na mchana nyumba  kwa nyumba, lakini pia tumeambiwa wazi hakuna mgombea aliyepita  bila kupingwa,” amesema.

Amesema hatua hiyo inawapa hamasa ya kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi kupigia kura  CCM na  kushiriki  katika uchaguzi  Oktoba  29,2025 .