BAO pekee lililofungwa na Pacome Zouzoua katika mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, limezua mjadala mzito.
Katika mjadala huo, upande mmoja unasema kulikuwa na mazingira ya mfungaji kuwa eneo la kuotea ambaye pia alicheza faulo kwa kumzuia beki wa Simba, Rushine De Reuck kwenda kuokoa hatari, huku wengine wakisema mtego huo ulivunjwa na Maxi Nzengeli aliyekuwa sehemu salama.
Matokeo ya bao hilo ambalo lilifungwa katika dakika ya 54, liliifanya Yanga kutetea Ngao ya Jamii huku ikiibuka na ushindi wa sita mfululizo dhidi ya Simba katika mashindano tofauti waliyokutana.
Wakati mashabiki wa Yanga wakishangilia ushindi huo wa 1-0, upande wa Simba na baadhi ya wadau waliona kama bao hilo lilitokana na mazingira ya kuotea, kitu ambacho kimewafanya waamuzi wa zamani, Abdallah Kambuzi, Israel Nkongo na Najim Nagy kuchambua kwa kina tukio hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kambuzi amesema kwa mtazamo wa kwanza Pacome alikuwa ameotea. Hata hivyo, akaeleza mabadiliko ya sheria ndiyo yaliyoipa Yanga faida. Kwa maelezo yake, bao hilo lilikuwa halali kwa mujibu wa tafsiri mpya ya kanuni.
Kambuzi amesema: “Ukitazama Pacome kweli alikuwa mbele ya walinzi wa Simba, lakini hakugusa mpira wa kwanza. Moussa Camara (kipa wa Simba) aliona hilo na kulalamika kwa mwamuzi wa pembeni, lakini kumbuka Maxi (Nzengeli) ndiye aliyecheza mpira huo na kuendelea na shambulio akiwa hayupo eneo la kuotea. Baada ya hapo, ndipo Pacome akajitokeza kumalizia mpira uliorudi kufuatia Camara kuokoa shambulizi la kwanza. Hapo mtego ulikuwa umemalizika na kwa mujibu wa sheria mpya hakuna kosa tena.”
Ameongeza kuwa, tafsiri ya kuotea imepanuka sana miaka ya hivi karibuni. Zamani mchezaji akiwa mbele ya mstari wa mwisho tu alihesabiwa ameotea, lakini sasa lazima aonekane kuhusika moja kwa moja.
“Mashabiki wengi wanahitaji kuisoma upya kanuni hii. Si sawa kuendelea kufikiri kwa mtazamo wa zamani. Waamuzi wa jana walifanya kazi nzuri,” amesema Kambuzi.
Lakini si kila mwamuzi aliyekubaliana na hoja hiyo. Najim Nagy, mwamuzi mstaafu aliyewahi kuchezesha michuano ya Conference League nchini England, aliona tofauti kabisa. Kwa maoni yake, bao hilo halikuwa sahihi.
Nagy amesema: “Kwangu Pacome aliotea kwa sababu alihusika kimazingira. Wakati mpira ule wa kwanza unapigwa, yeye alizuia mwelekeo na umakini wa mabeki wa Simba. Hata kama hakugusa mpira, tayari alikuwa sehemu ya tukio na aliwazuia mabeki kuzuia kwa uhuru. Hapo sheria iko wazi, hiyo inachukuliwa kama kuhusika, hivyo bao halikuwa halali.”
Nagy amesisitiza kuwa, waamuzi wanapaswa kutazama si tu kugusa mpira bali pia athari za mchezaji aliyeko nafasi ya kuotea kwa wapinzani.
“Hata ukisoma sheria za FIFA inasema kama mchezaji anaathiri uwezo wa adui kucheza mpira au kufanya uamuzi, tayari ameotea. Hii ndiyo hoja yangu,” amesema.
Kwa upande mwingine, mwamuzi wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Israel Nkongo ambaye sasa ni mkufunzi wa waamuzi, alikuwa upande wa Kambuzi. Mkongo ameeleza kuwa kosa la kuotea si kusimama tu kwenye nafasi bali ni kuhusika moja kwa moja Nkongo amesema: “Kimazingira kama Pacome angecheza ule mpira wa kwanza, bao hilo lingefutwa. Lakini hakufanya hivyo. Maxi ndiye aliyehusika moja kwa moja, na hakuwa kwenye nafasi ya kuotea. Baada ya shambulio kuendelea, Pacome akawa salama na akamalizia. Hilo ni bao halali kwa mujibu wa sheria.”
Nkongo alieleza kuwa uamuzi wa waamuzi wa jana ulikuwa sahihi kwa kuwa waliangalia hatua kwa hatua.
“Kwenye hili, hakuna cha kubishana, bao lilikuwa halali. Ni muhimu mashabiki wakajua tafsiri ya sasa ya kuotea ili tuondokane na mijadala inayotuchanganya,” amesema.
(Offside Law 11 – IFAB/FIFA)
Mchezaji anahesabiwa yuko kwenye nafasi ya kuotea (offside position) iwapo wakati mpira unapochezwa au kuguswa na mchezaji mwenzake:
Yuko karibu zaidi na goli la wapinzani kuliko mpira na mlinzi wa pili wa mwisho. Lakini kusimama kwenye nafasi ya kuotea si kosa.
Ni kosa la kuotea (offside offence) kama, wakati akiwa kwenye nafasi ya kuotea, mchezaji atahusiana moja kwa moja na mchezo kwa kufanya moja ya haya:
Kugusa au kucheza mpira uliopigwa na mchezaji mwenzake.
Kuathiri uwezo wa mpinzani kucheza mpira (mfano: kumzuia kipa kuona mpira, kuzuia mchezaji kusogea au kumpotosha).
Kufaidika kutokana na mpira uliomgonga, kutoka kwa adui au baada ya kurudi (rebound) kutoka kwa nguzo au kipa.
Si kosa la kuotea iwapo mchezaji atapokea mpira moja kwa moja kutoka na matukio haya matatu: Goal kick (goli-kiki), Throw-in (mpira wa kurusha), Corner kick (mpira wa kona).