Kibaha. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema taifa linahitaji wanasheria wenye moyo wa kujifunza daima, akibainisha kuwa elimu haiishii chuoni bali ni safari endelevu ya kukuza weledi na uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali.
Johari ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Septemba 18, 2025, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yanayofanyika Kibaha mkoani Pwani.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wanasheria kuhusu masuala ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa wa kisheria katika sekta ya hifadhi ya jamii.

“Msikubali kuwa watu walewale miaka yote. Jitahidini kubadilika kwa kujifunza mambo mbalimbali ili muwe na ujuzi na uelewa mpana zaidi,” amesema.
Ameongeza kuwa mtu anayejitahidi kujifunza na kutafuta maarifa mapya huwa na uwanda mpana wa kutatua changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya kazi na kuwa msaada mkubwa katika kuchochea maendeleo ya taifa.
Amesema baada ya mafunzo hayo atamteua mmoja wa washiriki kufundisha darasa kulingana na walichojifunza, jambo alilolieleza kuwa ni sehemu ya kupima uelewa na mshikamano wa maarifa waliyopata.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Vupe Ligate amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wanasheria wa Serikali kupata uelewa mpana kuhusu dhana ya hifadhi ya jamii pamoja na sheria zinazoiendesha.
“Tunatarajia baada ya mafunzo haya maofisa hawa watakuwa na mtazamo mpana na uelewa wa pamoja ili tunapokutana kufanya mashauriano, mjadala uwe rahisi na wenye tija kwa pande zote,” amesema Ligate.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wamepongeza hatua ya kuwajengea uwezo wanasheria wa Serikali wakieleza kuwa itasaidia kulinda masilahi ya jamii na kukuza uwajibikaji.
Neema Mlay, mkazi wa Kibaha amesema: “Wanasheria wakipata mafunzo ya mara kwa mara wataweza kushauri vizuri Serikali na taasisi. Hii inaleta ufanisi na kupunguza migogoro ambayo mara nyingi inasababisha hasara kubwa kwa taifa.”
Kwa upande wake Juma Shabani amesema kuna wakati wananchi wanakosa haki kwa sababu sheria haziwekwi wazi au kueleweka. Ikiwa mafunzo haya yatawasaidia wanasheria kueleza mambo kwa urahisi, itakuwa faida kubwa kwa jamii
Halima Ally, amesema kuwa mafunzo hayo yanafungua milango kwa wanasheria chipukizi kupata mifano ya utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi hususa katika kusaidia jamii.