Andabwile afichua siri ya kumzima Mpanzu Dabi, Aucho ampa tano

WAKATI Yanga ikitangaza kikosi cha kwanza kitakachoikabili Simba katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo uliochezwa juzi Jumanne na kumalizika kwa timu hiyo ya Jangwani kushinda bao 1-0 lililofungwa na Pacome Zouzoua katika dakika ya 54, jina la Aziz Andabwile liliwashtua wengi, lakini mwenyewe kuna siri ameifichua.

Hiyo ilitokana na nyota huyo tangu atue Yanga mwanzoni mwa msimu uliopita huku zikichezwa Dabi ya Kariakoo tatu zikiwemo mbili za Ligi Kuu Bara na moja Ngao ya Jamii hakuwahi kuanza kitu ambacho kiliacha maswali kwa nini benchi la ufundi chini ya kocha mpya Romain Folz kumuamini katika mchezo huo mkubwa na wenye historia.

Lakini baada ya mchezo, habari ikabadilika, wengi walionekana kumpongeza kwa kile alichokifanya kwani alikuwa mtulivu katika eneo la kiungo mkabaji akifanikiwa kucheza kwa dakika zote 90 akiwaweka benchi viungo wengine wa nafasi hiyo.

Kilichoshangaza zaidi ni namna ambavyo Andabwile amemaliza dakika zote wakati viungo alioanza nao Duke Abuya na Mudathir Yahya walitolewa na nafasi zao kuchukuliwa na Mohamed Doumbia na Moussa Balla Conte.

Akizungumza na Mwanaspoti, Andabwile alisema alipewa kazi maalumu na kocha Folz kuhakikisha hasogei zaidi mbele kwani kazi yake ni kulinda ukuta na kutembea na wachezaji ambao wangekuwa na hatari eneo lake.

“Sikuwa na kazi ngumu sana kiwanjani kutokana na maelekezo niliyopewa na benchi la ufundi kuhakikisha nasaidiana na walinzi wenzangu huku nikiwaacha Duke na Mudathir wapande kuongeza mashambulizi.

“Nilikuwa na kazi maalum niliyopewa maelekezo na benchi la ufundi, ukiangalia muda mwingi nilikuwa eneo la ulinzi nikiwa dhidi ya kina Charles Ahoua, Elie Mpanzu na Neo Maema ambao wangeweza kuleta hatari langoni kwetu, nashukuru nilifanikiwa,” alisema Andabwile.

Kiungo huyo wa zamani wa Mbeya City na Fountain Gate, alisema Folz alimwambia ahakikishe anatembea na wachezaji hatari langoni mwao huku akifichua kwamba baada ya mchezo, kocha huyo alimfuata na kumpa pongezi kwa kuifanya kazi ilivyotakiwa.

“Kocha aliniamini, akanipa kazi na mara baada ya mchezo aliniita na kunipongeza kutokana na kazi niliyoifanya na kunihakikishia kuwa endapo nitaendelea kufanya kazi hiyo kwa usahihi nitakuja kuwa mchezaji mkubwa na tegemeo kwenye kikosi chake.

“Haikuwa rahisi kwani ilihitaji umakini na kutokufanya makosa, ukuta pia ulikuwa sehemu ya msaada mkubwa kwangu, nampongeza kipa Djigui Diarra alisawazisha baadhi ya makosa tuliyoyafanya hasa kipindi cha kwanza na kuifanya timu itoke mapumziko ikiwa haijaruhusu bao hata moja licha ya wapinzani kupata nafasi,” alisema Andabwile.

Andabwile alisema kitendo cha kocha kumuamini na kumpa nafasi, kilitosha kwake kufanyia kazi yale aliyopewa kama maelekezo ili kujiweka kwenye nafasi ya kuendelea kuaminiwa huku akiweka wazi kuwa bado anaendelea kujifunza na yupo tayari kujifunza ili awe bora kwenye kila mchezo.

Wakati huohuo, kiungo wa zamani wa Yanga, Khalid Aucho, amempongeza Andabwile kwa kumwambia: “Mchezo mzuri kaka, endelea kupambana.” Aucho alitoa pongezi hizo katika posti aliyoiweka Andabwile kwenye akaunti yake ya Instagram baada ya mchezo.

Siku chache kabla ya mchezo huo, Folz alisema anatambua kulikuwa na Khalid Aucho ambaye ni kiungo bora aliyefanya mambo mazuri ndani ya Yanga huku akiweka wazi ana imani kubwa na wachezaji waliopo watafanya vizuri zaidi.

“Aucho alikuwa muhimu kwenye kikosi cha Yanga, lakini nakuahidi yeyote nitakayempanga atatimiza wajibu kama alivyowahi kufanya mchezaji huyo,” alisema Folz.

Kauli ya kocha huyo imedhihirishwa na Andabwile baada ya dakika 90 ambapo alionyesha mchezo mzuri ambao kila mmoja aliona.

Eneo la kiungo mkabaji anapocheza Andabwile, kuna vita kubwa ya namba kwani pia wapo Moussa Balla Conte, ambaye katika mchezo huo aliingia kipindi cha pili.

Pia kuna Duke Abuya na Mudathir Yanga ambao walianza kikosi cha kwanza, lakini wakatolewa baadaye kupisha kuingia wachezaji wengine.

Andabwile pia ana uwezo wa kucheza beki wa kati, amekuwa akitumika nafasi hiyo tangu msimu uliopita na msimu huu kwenye mechi za maandalizi alicheza sambamba na nahodha, Bakari Mwamnyeto wakati Yanga ikishinda 3-1 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.

Kwa kiwango alichoonyesha Andabwile na kauli ya Kocha Folz, ni wazi Yanga mpango wake wa kumrudisha Aucho kipindi cha dirisha dogo unaweza ukafa kwani iliripotiwa kiungo huyo raia wa Uganda huenda akarudi kama nyota wapya waliosajiliwa kuziba pengo lake watashindwa kufanya vizuri. Kwa sasa Aucho anaitumikia Singida Black Stars baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika.