AWAMU YA SITA YAIPIGA JEKI ELIMU ARUSHA – WALIMU WAPONGEZWA

Na Pamela Mollel,Arusha 

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu mkoani Arusha kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 267 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu na ujenzi wa miundombinu ya shule.

Akizungumza Septemba 17, 2025 kwenye Kongamano la Wadau wa Elimu kuelekea Wiki ya Elimu Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala wa Mkoa, Missaile Albano Musa, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa CPA Amos Makalla, alisema fedha hizo zimekuwa chachu ya mapinduzi makubwa ya kielimu.

Missaile alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia, Mkoa wa Arusha umepokea shilingi bilioni 267 ambapo bilioni 107.08 zimetumika kuboresha miundombinu ya shule. Maboresho hayo yameongeza idadi ya wanafunzi, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kupandisha kiwango cha taaluma kwa ujumla.

“Niwahakikishie, walimu wetu wamekuwa si tu wasimamizi wa taaluma shuleni bali pia wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa. Nawapongeza kwa kazi kubwa iliyoleta heshima kwa Serikali yetu. Niwasihi mjiendeleze kimasomo, muendane na mabadiliko ya teknolojia na muendelee kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kufanikisha malengo ya taifa,” alisema Missaile.

Walimu wa Mkoa wa Arusha nao hawakusita kuipongeza Serikali kwa maboresho hayo ambayo yameongeza ari ya wanafunzi kusoma na kurahisisha ufundishaji. Mwenyekiti wa TAHOSA Mkoa wa Arusha, Mwl. Omari Nyangu, alisema hatua ya Serikali imewaondolea wazazi adha ya kuchangia ujenzi wa madarasa, jambo lililoongeza hamasa ya kupeleka watoto shule.

Maboresho haya yameonesha dhamira ya Awamu ya Sita ya kubadilisha sekta ya elimu kwa vitendo, huku walimu wakihamasishwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maendeleo na taaluma kwa vizazi vijavyo.