NIKAMJIBU: “Sikutaka nikupe mshituko. Nilikuwa nakungoja urudi.”
“Mimi nimepata habari hii leo wakati narudi.”
“Ni nani aliyekupa habari hiyo?”
“Ni mke wake. Alinipigia simu akanijulisha hivyo. Nikashituka sana kwa sababu juzi juzi tu nilikuwa naye. Kwa hiyo nilipofika stendi nikaona niende huko kwanza nikampe pole.”
“Hata mimi nilishituka, yaani mpaka hivi sasa picha yake inanijia akilini mwangu!”
“Kushituka ni lazima. Mauaji yake yametokea ghafla sana.”
“Huyo mke wake amekwambia mumewe ameuawa na nani?”
“Hawafahamu. Polisi ndiyo wanaendelea na uchunguzi. Ameniambia hujafika kumpa pole.”
“Ni kweli. Nilikuwa niende leo na Raisa, lakini niliamka vibaya. Mwili ulikuwa unaniuma sana. Nikamwambia Raisa aende. Msiba bado upo, naweza kwenda hata kesho.”
Wakati namjibu hivyo nilikuwa najiuliza hivi kweli huyu mwanaume hajamuua yeye huyo rafiki yake na kuniachia mimi kizaazaa? Kufika na kufika tu aende kwenye msiba! Mbona hakunipigia simu kunijulisha?
Si hasha kwamba ukweli wote alikuwa anao yeye. Vile nilivyokuwa namjibu nilihisi kama alikuwa akinifanya mpumbavu.
“Na maziko yake ni kesho. Nashukuru kuwa nitaweza kuhudhuria,” akaniambia.
Ile hisia kwamba huenda Sufiani alikuwa anajua kila kitu ilifanya nijione kuwa na hatia. Nikainamisha uso wangu kabla ya kumwambia: “Imekuwa vyema utaweza kumzika rafiki yako.”
“Masikini kumbe pale juzi ninaondoka ndio nilikuwa ninaagana naye.”
“Binaadamu hujui yaliyoko mbele yako. Unajua Mwenyezi Mungu ameficha siri ya mauti.”
“Hata sijui nani amemuua rafiki yangu!”
“Wanaweza hata kuwa majambazi waliomdhania kuwa ana pesa.”
“Mimi nafikiri kitu kimoja. Yule bwana alikuwa anapenda sana wanawake. Inawezekana alichukua mke wa mtu, mwenyewe akamfuma akampiga na kumuua.”
Moyo wangu ukashituka. Sufiani amelenga mahali pale pale panapohusika!
Amejuaje? Itakuwa ni yeye tu ananizunguka. Huku nikimtazama kwa macho ya mshituko nikamuuliza.
“Kwani alikuwa na tabia hiyo?”
“Hiyo ndiyo ilikuwa tabia yake. Nimesikia mwili wake ulitupwa makaburini. Na kama ulitupwa makaburini atakuwa ameuawa nyumbani kwa mtu.”
Moyo wangu uliendelea kunidunda kwa nguvu. Hapo nilihisi wazi kuwa Sufiani alikuwa akijua kila kitu kwani ilikuwa kweli Shefa aliuawa nyumbani tena nyumbani pale pale. Sasa amejuaje. Tuseme amekisia tu? Haiwezekani?
Sikuyatia mdomo tena yale maneno yake. Nikabaki kimya nikiwaza.
“Lakini kwa vile nimesikia kuwa gari lake limepatikana nina imani mtu aliyemuua atafahamika tu,” Sufiani aliendelea kuniambia lakini nikajifanya kama nilikuwa na mawazo yangu.
“Halafu naona kama hao polisi ni wazembe,” akasema.
“Kwanini?” nikagutuka na kumuuliza.
“Hapo walipolipata gari lake wangekamata watu wa hapo na kuwahoji. Nasikia gari lake lilikutwa limeegeshawa mbele ya nyumba moja. Sasa hao wenye nyumba ndio wangeulizwa.”
Kwa vile sikutaka Sufiani aendelee na maneno yale ambayo yalikuwa yananichanganya akili yangu, nikamkatiza: “Umeshakula au nikupikie chakula?”
“Nimekula huko msibani”
“Umekula nini?” nikamuuliza kupoteza muda.
“Si unajua misiba ya Tanga lazima wapike pilau.”
“Kwa hiyo umeshiba.”
“Nimekula kidogo tu. Sisikii hamu ya kula sana.”
“Ni kama mimi, pia sina hamu ya kula tangu jana”
“Huenda na wewe una malaria. Ulikwenda kupima?”
“Sijakwenda. Hivyo ninavyoogopa sinadano ukinitajia kupima mwili unasisimka.”
“Sasa utafuga maradhi kwa kuogopa sindano?”
“Nimememza dawa. Nitapona tu.”
Sufiani hakuridhika na jibu langu, akaguna kisha akainuka.
“Unakwenda wapi?” nikamuuliza.
“Ninakwenda msalani.”
Alipotoka haukupita muda mrefu nikasikia akiniita.
“Rukia hebu njoo.”
Nikaenda.
Nikamkuta ameshika lile rungu nililokuwa nimeliweka stoo.
Moyo wangu ukashituka. Miguu ikaninyong’onyea. Kama nisingejikaza ningeanguka pale pale.
“Hili ni nini?” akaniuliza akiwa amenikazia macho.
“Hilo ni rungu,” nikamjibu kama mtoto wa shule anayemjibu mwalimu wake.
Nilijifananisha na mtoto wa shule kwa sababu wakati Sufiani ananiuliza alijua fika kwamba lile lilikuwa rungu.
“Limewekwa na nani kule stoo?” Akaendelea kuniuliza.
Swali hilo la pili lilikuwa rahisi kuliuliza lakini lilikuwa gumu kulijibu. Lilikuwa gumu kwa sababu rungu hilo ndilo lilitumika kumuua Shefa na aliyelileta pale nyumbani na kuliacha ni huyo mtu aliyemuua Shefa. Sasa hapo ningejibu nini wakati nilikuwa nikificha kuyaeleza mauaji ya Shefa yalivyotokea nikijifanya sijui lolote.
Lakini kwa upande mwingine swali hilo lilikuwa gumu kulijibu kwa sababu sikuwa na uhakika kwamba aliyeliuliza alikuwa hajui ukweli kuhusu rungu hilo. Na kama yeye ndiye aliyemuua Shefa kwa hila, atakuwa anajua kuwa rungu hilo nimeliweka mimi.
“Nimeliweka mimi, kwani lina nini?” Nikamjibu hivyo ili nione ataniambia nini.
“Ni la kazi gani?”
“Ni rungu tu nililiona nyumbani Sahare nikalichukua.”
“Mbona hapa lina kama nywele nywele, halafu kama lina damu iliyoganda?”
“Nani amekwambia kwamba hizo ni nywele na hiyo ni damu?”
“Sasa ni nini?”
“Nimelichukua hivyo hivyo. Kama ni damu basi labda waliwahi kumpigia mwizi. Lakini mimi najua hiyo si damu.”
“Limenitisha. Nilidhani labda ulimpiga mtu.”
“Hapana. Sijampiga mtu. Nililichukua hivyo hivyo.”
Sufiani akalitazama lile rungu kisha akalirudisha kule stoo.
Sasa kama Sufiani ameshaliona rungu hilo, nikienda kulitupa usiku si ataniuliza lile rungu liko wapi? Nikajiuliza.
Nikajiambia nimechelewa kwenda kulitupa. Nikagundua kuwa nilifanya uzembe kuliacha pale nyumbani, ni bora pale nilipoutupa mwili wa Shefa na rungu hilo ningelitupa hapo hapo.
Sufiani alipofungua mlango wa stoo na kulirusha lile rungu, nikaondoka kwenye mlango na kurudi ndani. Nikakaa lakini nilikuwa na mawazo mengi. Baadaye kidogo Sufiani akarudi. Safari hii akaingia chumbani.
Nikadhani angetoka tuendelee na mazungumzo lakini hakutoka. Nikamfuata huko huko.
Nikamkuta amesimama kando ya kitanda. Pochi yangu niliiweka kwenye stuli nikaikuta juu ya kitanda.
“Shefa hakuwahi kufika hapa nyumbani kabla ya kuuawa?” Akaniuliza ghafla.
Swali hilo lilinishitua zaidi kuliko lile la kwanza.
Nikajiuliza kwanini Sufiani ameniuliza swali hilo? Amegundua nini? Au ni yeye aliyenikomoa?
Nilivuta pumzi kwa nguvu nikazishusha. Ninaamini Sufiani alizisikia.
“Kwanini umeniuliza hivyo?” Nikamuuliza.
Ngoja nikueleza ukweli”
Sufiani akajiegemeza kitandani, mimi nikakaa kabisa. Nilikuwa siwezi tena kusimama. Moyo ulishaanza kunienda mbio. Sufiani anataka kunieleza ukweli gani?
“Nieleze huo ukweli,” nikamwambia huku nikijikaza nisionyeshe aina yoyote ya hofu.
Kama ukweli huo utahusu mimi kumuua Shefa, baba yangu alishanieleza kuwa nisiukubali hata kidogo. Msimamo wangu ulikuwa ni huo huo, si kwa polisi tu bali hata kwa mtu yeyote atakayenieleza kuhusika na mauaji ya Shefa.
“Mke wa shefa amenilalamikia. Ameniambia amepata taarifa kuwa gari la mume wake limepatikana katika mtaa wetu tena nyumba ya tatu kutoka nyumba yetu. Imani yake ni kwamba mume wake aliliacha gari hilo kwa madhumuni ya kuja kwetu kwani hakuwa na mtu yeyote anayefahamiana naye katika mtaa huu. Umenielewa?”
“Nimekuelewa.”
“Sasa ameniambia mimi au wewe utakuwa unajua kuhusu mauaji yake kwa sababbu alipoliacha gari hilo hakurudi tena kulichukua. Maana yake ni kuwa Shefa ama aliuawa kwetu au aliuawa katika mtaa huu na kwenda kutupwa makaburini.”
Mpaka hapo sikuwa na lolote la kukana au la kukubali, bado nilikuwa namsikiliza ingawa moyo wangu ulikuwa ukienda mbio kweli kweli.
“Kitu ambacho mwanamke huyo kimemshangaza ni swali, kwanini Shefa aliache gari nyumba ya tatu kutoka nyumba yetu badala ya kuliacha barazani kwetu kama kawaida yake. Tena amefanya hivyo katika siku ambayo mimi sikuwepo!” Sufiani aliendelea kuniambia akiwa amenikazia macho.
Nikayakwepa macho yake na kuangalia upande mwingine.
“Baada ya yeye kukwambia hivyo, wewe ulimwambia nini?”
“Mimi nilimpinga sana. Nilimwambia Shefa hakuja nyumbani kwangu, kama angekuja nyumbani kwangu mke wangu angeniambia. Nilimwambia anapokuja kwangu, gari lake huliegesha barazani kwetu na sio nyumba ya tatu. Na pia Shefa hawezi kuja nyumbani kwangu usiku akijua mimi sipo. Yule mwanamke nilimwambia hivyo lakini bado alikuwa na shaka shaka. Sikuelewa shaka yake ilitokana na nini.”
“Anataka kuleta uzushi na fitina. Maana yake ni kwamba sisi ndio tuliomuua mume wake?”
“Sio sisi. Yeye anajua kuwa mimi sikuwepo. Hapo anakushutumu wewe. Kwa kweli sikutilia maanani malalamiko yake lakini nilipokuja hapa nyumbani na kuona lile rungu, nilipata shaka. Lile rungu halikuwapo wakati naondoka na lina nywele na damu iliyoganda! Mjane wa Shefa aliniambia kwamba uchunguzi wa mwili wa marehemu mume wake ulionyesha kwamba alipigwa na kitu kizito kama rungu upande wa kushoto wa kichwa chake na kusababisha kifo chake….”
Sasa hofu yangu ilisomeka waziwazi usoni kwangu kwani kama lile rungu litapelekwa kwa wataalamu, itafahamika kuwa ile iliyoganda ni damu ya Shefa na zile zilizonata ni nywele zake.
Hapo sitakuwa na ujanja wa kuepuka kuhusika na mauaji yake. Kwa vyovyote vile nisingeweza kujitetea kwamba marehemu alikuja kwangu usiku, akaja mtu akampiga rungu wakati nimeshakataa kwamba Shefa hakuja kwangu.
“Mume wangu unaonekana kama unakubaliana na mawazo ya mjane wa marehemu Shefa.”
“Alipokuwa ananieleza nilihisi alikuwa na uchungu tu wa mauaji ya mume wake lakini nilipokuja hapa kuna vitu viwili vimenichanganya. Kimoja ni lile rungu na cha pili.…”
Bado Watatu – 32 | Mwanaspoti
