Unguja. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja ili kuhakikisha wanafikia azma ya kuwa na Taifa linalojitegemea kiuchumi.
Samia amebainisha hayo leo Alhamisi Septemba 18, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika Jimbo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mkutano huo wa kampeni za mgombea huyo zimeingia siku ya pili katika visiwa vya Zanzibar huku akitarajiwa kuhitimisha kwa mkutano wa kampeni utakaofanyika katika Kisiwa cha Pemba, kabla ya kuendelea na maeneo mengine ya Tanzania Bara.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Samia amesema ili kuwa na Taifa linalojitegemea, lazima uchumi wa mtu mmoja mmoja uimarike, mtu huyo aweze kujitegemea, wakati huohuo uchumi wa Taifa nao ukikua zaidi.
“Ahadi za CCM katika miaka mitano ijayo, ni kuendelea kukuza uchumi na kipato cha wananchi, kuinua hali za maisha za Watanzania wote, kulinda usawa wa jamii, kulinda amani, usalama na utulivu katika nchi yetu, vilevile kudumisha demokrasia na utawala bora na kujenga Taifa linalojitegemea.
“Katika kujenga Taifa linalojitegemea, tutafika huko mpaka kila mtu ndani ya Tanzania hii awe na shughuli inayompa kipato, yeye mwenyewe asimame kama mtu mmoja, halafu kwa umoja wetu tunaweza kujitegemea. Hii ndiyo kazi tunayoendelea kuifanya, kuandaa mazingira kwa Watanzania, kuwa na shughuli za kufanya kuingiza kipato ili kila mmoja aingize kipato,” amesema.
Samia amempongeza mgombea urais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akisema wakati anaingia madarakani kulikuwa na mlipuko wa Uviko-19, hali ya uchumi ilishuka, lakini sasa ameweza kukuza uchumi unaokuwa kwa kasi ya asilimia 7.1 wakati kule Tanzania Bara ukikua kwa asilimia 6, kutokana na sera nzuri za fedha.

Amesema kwa matokeo ya ukuaji huo wa uchumi na utekelezaji wa ahadi walizozitoa, yanaonekana dhahiri kupitia utekelezaji wa ahadi walizozitoa.
Samia amesema matokeo hayo yamewawezesha kujenga skuli za kisasa, masoko na madaraja.
Pia, amemshukuru Dk Mwinyi kwa ushirikiano wake katika kukuza utalii nchini kwa kuwa, idadi ya watalii imeongezeka hadi kufikia milioni tano kwa Tanzania Bara na 700,000 kwa Zanzibar, ikiwa imevuka lengo iliyojiwekea mwaka uliopita.
Mgombea huyo amesisitiza kuwa, kuongezeka kwa watalii, kunakuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa jumla.
“Suala la uchumi wa buluu, tunakwenda kulifanyia kazi kwa pamoja, uvuvi kwenye bahari kuu. Suala la mafuta na gesi, ni jambo la Muungano, tunakwenda kulifanyia kazi kwa pamoja kuhakikisha tunakwenda kunufaika na rasilimali hizo,” amesema Samia.
Kuhusu, programu ya kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), amesema imefanya vizuri, wanakwenda kuendelea nayo na sasa wanajiandaa kufanya awamu nyingine ili kuinua maisha ya wananchi wale walio chini kabisa.
Piua, ameahidi kuendelea na programu ya mikopo kwa wafanyabiashara na watarasimisha biashara ndogondogo Tanzania Bara na Zanzibar ili kuwasaidia wafanyabiashara hao kuendesha shughuli zao katika namna inayotambulika.
“CCM tuna ujasiri wa kuja kwenu kuomba kura, na ujasiri huu unatokana na kwamba tumeweza kufanya makubwa na tunataka kufanya makubwa mkitupa ridhaa yenu,” amesema mgombea huyo.

Mgombea urais wa Zanzibar, Dk Mwinyi amewahamasisha Wazanzibari kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Pia, amewataka wagombea wengine katika nafasi zote wahimize jambo hilo.
“Niwaombe wagombea wote, kabla ya kueleza mtafanya nini, himizeni kwanza amani na utulivu katika Taifa hili, tukiwa na amani hayo mengine ya maendeleo yatafanyika kikamilifu,” amesema mgombea huyo.
Dk Mwinyi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura kama wanavyojitokeza kwenye mikutano yao ya kampeni akitamka kwamba, uchaguzi ni kura
“Nakuombeni tujitokeze kwa wingi Oktoba 29 ili tukafanye ile kazi ya kuchagua viongozi wetu. Naomba mkampigie kura mgombea urais wa Tanzania, mkanipigie na mimi, pamoja na wabunge na madiwani wote wa CCM,” amesema Dk Mwinyi.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro amesema Samia na Dk Mwinyi wamesimama katika kuusimamia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Pia, amesema Samia amezidi kuuimarisha Muungano huo kiuchumi.
Amesema ameshuhudia viongozi hao wakisisitiza kudumisha amani na utulivu nchini.
“Kupitia filamu ya Royal Tour… Zanzibar kama kituo cha utalii katika nchi yetu. Kwa sisi uliotupa nafasi ya kuhudumu huko nje, tumeshuhudia namna filamu hiyo ilivyochochea kuongeza kwa watalii,” amesema.
Dk Migiro amesema kupitia filamu hiyo, Tanzania imepata hadhi ya kipekee kimataifa kwa kuwa, inashuhudiwa watalii wanavyoongezeka na namna ndege kutoka mataifa mengine zinavyotua nchini husasani katika visiwa vya Zanzibar.
Katibu mkuu huyo amesisitiza kuwa, Samia amewekeza kwenye rasilimali watu kwa kuwajengea uwezo na kutoa ajira, hivyo amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kuwachagu viongozi hao siku ya uchaguzi, Oktoba 29, 2025.
“Tuna kila sababu ya kuwaunga mkono viongozi hawa ili Tanzania yetu iwe yenye maendeleo na chachu ya ukuaji wa uchumi…ifikapo Oktoba 29, tunatiki, tunatiki, tunatiki,” amesema Dk Migiro.
Wagombea ubunge waomba kura
Mgombea ubunge wa Nungwi, Mdoe Haji amesema ni heshima kwake kama kijana kupata nafasi ya kugombea nafasi hiyo, akisema vijana wamepata heshima kubwa ya kuaminiwa katika uongozi, jambo ambalo ni deni kubwa kwao.
“Niwahakikishie tutailinda heshima hii na vijana wote tujitokeze kwenda kupiga kura kumchagua Samia na Dk Mwinyi ili waendelee kufanya makubwa na kutuamini sisi vijana katika kuwasaidia kazi,” amesema mgombea huyo.
Mgombea ubunge wa Donge, Sadifa Juma Hamis amesema waendesha bodaboda na bajaji wameahidi kwenda kuwapigia kura wagombea urais wa CCM kwa sababu wamefanya kazi kubwa hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara katika jimbo hilo.
Amesema wamejengewa hospitali za kisasa za hadhi ya nyota tano, jambo ambalo limeboresha huduma za afya sio tu katika jimbo lake, bali pia Zanzibar nzima.
“Viongozi wetu hawa, wametekeleza kikamilifu wajibu wao katika kuwaletea wananchi maendeleo. Dk Mwinyi na Samia wanafaa kuendelea na uongozi, twendeni tukawapigie kura ikifika Oktoba 29, 2025,” amesema mgombea huyo.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Chaani, Ayoub Mohamed Mahmud amesema katika miaka mitano iliyopita, kwenye eneo la elimu ya juu, ameshuhudia uamuzi wa Serikali ya CCM wa kutoa fedha kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu.
“Uamuzi huu umewasaidia watoto wa wanyonge katika mkoa huu wa Kaskazini Unguja ili kuwasaidia watoto hao kuzifikia ndogo zao za maisha, tunawashukuru sana,” amesema mgombea huyo.
Amesisitiza kwamba, watahakikisha majimbo yote manane katika Mkoa wa Kaskazini Unguja yanapiga kura kwa wingi ili kuhakikisha wanapata ushindi.