Chaumma yaahidi boti za mwendokasi Kanda ya Ziwa

Kagera. Mgombea urais wa Chaumma, Salum Mwalimu ameahidi mageuzi ya kiuchumi katika Kanda ya Ziwa ikiwa ni pamoja na uwekezaji wa maboti ya kisasa ya mwendokasi kasi ya Mwanza na Kagera, endapo atachaguliwa kuwa rais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza Septemba 18, 2025, katika mkutano wa kampeni uwanja wa Red Cross, Muleba,  Mwalimu amesema serikali yake itashirikiana na sekta binafsi kuboresha usafiri wa haraka kwa njia ya maji kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa.

“Kama leo kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar unatumia dakika 60, kwa nini Mwanza hadi Kagera iwe tofauti? Tunao wawekezaji, tuna uwezo, na watu wanaosafiri ni wengi. Tunahitaji maboti ya mwendokasi, na tutayaleta,” amesema Mwalimu.

Ametolea mfano kampuni ya Bakhresa ilivyoleta mageuzi makubwa ya usafiri kwa maboti ya kasi kati ya Dar es Salaam na Zanzibar, Mwalimu amesema haoni sababu ya Kanda ya Ziwa kuendelea kusalia nyuma kimaendeleo wakati rasilimali na fursa zipo.

“Kama Bakhresa ameweza kuifungua  Zanzibar, iweje Serikali ishindwe kuleta mabadiliko kama hayo Kanda ya Ziwa,” amesema.

Mwalimu ameeleza kuwa serikali ya Chaumma itawekeza fedha za kutosha kupitia Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi, kinachoongozwa na David Kafulila, ili kuwezesha upatikanaji wa maboti ya mwendokasi na kuboresha miundombinu ya bandari na vituo vya usafiri.

“Nitawekeza mabilioni kwa ajili ya maboti ya mwendokasi na miundombinu yake. Tuko tayari kushirikiana na wawekezaji wote wanaotaka kusaidia kuleta maendeleo ya kweli,” amesema.

Ufunguzi wa soko, kiwanda

Katika hatua nyingine, Mwalimu ameahidi kuanzisha soko kubwa la kahawa na kiwanda cha kuchakata zao hilo mkoani Kagera ili kuongeza thamani na kuwainua wakulima.

“Tutafungua soko la kahawa hapa na kuanzisha kiwanda ili kuongeza thamani na kipato kwa wakulima wetu,” amesema.Vilevile ametangaza mpango wa kujenga kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki, hatua itakayochochea sekta ya uvuvi, kuongeza ajira, na kukuza uchumi wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria.

Kuhusu uhakika wa sukari na mapambano dhidi ya umaskini amesema matatizo yaliyopo ni ya kisiasa na wala si ukosefu wa rasilimali.

“Hakuna uhaba wa sukari Tanzania miwa ipo, mabonde yapo, kinachokosekana ni dhamira ya kisiasa. Tutajenga viwanda zaidi, tuzalishe sukari ya kutosha, tupunguze bei na tuondoe umaskini,” amesema.

Mbali na ahadi hizo pia ameahidi kuwa, endapo atachaguliwa kuwa rais, atahakikisha wakazi wa Kanda ya Ziwa wanapata huduma ya majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria.

Mwalimu amesema yupo tayari kununua ugomvi na yeyote ili kutetea haki ya wananchi kupata maji safi kutoka ziwa hilo, akisisitiza kuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa watu wa eneo hilo.

 “Nimewaambia Mwanza, lakini nawaambia nyie hapa Muleba, nipo tayari kama mkuu wa nchi kununua ugomvi na yeyote kuhusu matumizi ya majisafi ya Ziwa Victoria. Hatujampangia Mungu kuzaliwa Muleba au kuleta ziwa Muleba,” amesema Mwalimu.

Mwalimu ameeleza kuwa ni haki ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa ziwa hilo kunufaika na maji yake kwa matumizi ya kila siku na shughuli za kiuchumi, kwani ni sehemu ya mazingira yao ya asili.

“Mungu aliwaleta wananchi Muleba na ziwa hilo bila kumuomba, na aliwaweka waishi pembezoni mwa ziwa hilo na wanufaike na majisafi na salama,” ameongeza.

Akitaja mikoa ya Mwanza, Geita na mingine inayozunguka Ziwa Victoria, Mwalimu amesema haiwezekani maeneo hayo yakabiliwe na uhaba wa maji safi huku ziwa hilo likiwa ni chanzo kikuu cha maji nchini.

Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa  (Chaumma), John Mrema ametoa wito  kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera kukikataa Chama cha Mapinduzi (CCM), akidai kuwa ni chanzo kikuu cha umaskini wa Watanzania na mateso ya kila siku ya wananchi wa kawaida.

Mrema ameelezea hali ya kusikitisha ya maisha ya wananchi licha ya rasilimali zilizopo mkoani humo.

 “Kagera mnazalisha sukari, lakini wananchi mnauziwa kwa bei kubwa kuliko Mwanza. Hii ni dhuluma. Kwa nini wenye kiwanda mnunue kwa bei ya juu?”