Dodoma. Mgombea ubunge wa Jimbo la Manyoni, Dk Pius Chaya (CCM) amewaahidi wananchi endapo atachaguliwa kwa mara nyingine, anakwenda kuongeza kasi ya kufungua barabara jimboni humo.
Dk Chaya alitoa ahadi hiyo jana Jumatano Septemba 17,2025 katika vijiji vya Kata ya Isseke wilayani Manyoni.
Mgombea huyo ameitaja barabara ya Mangoli -Igwamadete, Iseke -Ipanduka hadi Ntumbi, Simbanguru-Mafurungu na Simbanguru-Nkambalala ambayo inagusa uchumi wa watu wengi.
Katika kampeni hizo ambazo ziliongozwa na Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Manyoni, Charles Chimaisi, Dk Chaya amesema licha ya kazi kubwa iliyofanyika katika kipindi cha miaka yake mitano ya ubunge, bado anaona haja ya kuwekeza nguvu kuifungua Manyoni kwenye miundombinu.
“Chini ya mama yetu Samia Suluhu Hassan tumefanya mambo makubwa, tunaamini kuwa tutaendeleza pale tulipofikia, tupeni kura tukayatimize kwa vitendo ili jimbo hili lizidi kupata maendeleo ya kweli,” amesema Dk Chaya.
Katika mkutano huo ambao ulifurika umati mkubwa wa watu, mgombea huyo akiahidi kusimamia maboresho ya mawasiliano hasa Kijiji cha Simbanguru ambacho kwa sasa hakina kabisa mawasiliano ya simu.
Yeye na wagombea udiwani Kata na viti maalumu wameahidi kujenga zahanati vijiji vya Mangoli, Ipanduka, Chidudu, Mafurungu na Nkambalala na kusogeza maji katika vijiji vya Simbanguru, Mangoli, Igwamadete na Ipanduka.
“Mkiichagua CCM tunakwenda kuboresha mawasiliano ya simu Simbanguru sanjari na kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga sekondari mpya Simbanguru na kuongeza madarasa katika Shule ya Msingi Mpapa, na kujenga josho katika kijiji cha Mangoli ili lisaidie wafugaji waishio maeneo hayo,” amesema Dk Chaya.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Chimaisi amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na uchaguzi sahihi utakuwa ni kwa Rais, mbunge na madiwani wanaotoka CCM.
Chimaisi amesisitiza umoja, amani na mshikamano kuwa silaha ya mafanikio katika maendeleo, huku akawaagiza viongozi wa ngazi ya chini kuwatumikia wananchi kwenye maeneo yao bila kuwabagua kwa namna yoyote ile.