DK SAMIA:NILETEENI DK.HUSSEIN ALI MWINYI ILI TUSHIRIKIANE KATIKA KULETA MAENDELEO

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Zanzibar

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Mgombea Urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi ndiye mgombea sahihi kwa sasa ambaye atakayeshirikiana naye kuleta maendeleo kwa manufaa ya pande mbili za muungano.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Jimbo la Nungwi Wilaya ya Kaskazini A katika Mkoa wa Kaskazini Unguja visiwani Zanzibar Rais Dk. Samia amesema matokea ya ukuaji uchumi na utekelezaji ahadi za CCM kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, umeonekana dhahiri uwezo wa kiongozi huyo katika kuwaongoza Wazanzibar.

“Pamoja na majanga yote tuliyopitia ikiwemo Covid na kushuka kwa uchumi duniani bado tumeweza kufanyakazi kubwa pamoja katika sera za kifedha na uchumi na ndiyo maana hatukuweza kukwamisha miradi yetu.

“Kwenye sera za kifedha na sera za kiuchumi, Dk. Hussein ameweza kusimamia na kuimarisha uchumi ambao kwa sasa unakuwa kwa kasi kubwa.Ukuaji wa uchumi kwa Tanzania bara umeongezeka kwa asilimia sita huku Zanzibar ukiwa juu zaidi kule kwetu Bara maana umekuwa kwa asilimia 7.1 kwa mwaka.”

Amesisitiza kwamba kubwa zaidi uchumi umekuwa hata mifukoni kwa kila mwananchi huku akieleza alipokuwa akiwasili Nungwi alikuwa akıtazama kila pande na kujionea namna ambavyo kumejengeka nyumba nzuri za makazi.“Biashara zinafanyika na mambo yanaenda vyema kwa amani na utulivu.”

Pamoja na hayo amesema mbali ya kukuza uchumi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla pia idadi ya watalii imeongezeka kufikia jumla ya milioni tano kwa Tanzania Bara na hapa Zanzibar mpaka mwezi uliopita ilishavuka lengo lililowekwa la watalii 700,000 na idadi ya watalii inakwenda kuongezeka.

“Tutakapomaliza mwaka tutakuwa tumevuka lengo letu tulilojiwekea. Kuongezeka kwa utalii kunaongeza mapato ndani ya serikali, kunaongeza mapato ndani ya wananchi.Kwa hiyo hongereni sana ndugu zangu.

“Kuhusu mazingira katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kushirikiana na Dk.Mwinyi tumefanyakazi vizuri kuna miradi tuliyoanza nayo ikiwemo kule Sikweze Kaskazini A lakini pia Wete kule Pemba.Kuna miradi mikubwa ya mabadiliko ya tabia nchi tumeanza nayo na tutaendelea nayo.”