FIFA yaweka mamilioni Simba, Yanga

SIMBA, Yanga, Azam na klabu nyingine chache za Ligi Kuu Tanzania Bara, zitakuwa miongoni wa wanufaika wa kupata fidia ya fedha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) kwa kuruhusu wachezaji wao kuzitumikia timu mbalimbali za Taifa katika mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Mgawo huo wa fedha ni sehemu ya Mradi wa FIFA wa kuzinufaisha klabu na ni matunda ya makubaliano baina ya FIFA na Chama cha Klabu za Soka Ulaya (ECA) kilichoketi Machi 2023.

Tofauti na hapo nyuma ambapo klabu zilikuwa zikilipwa kwa kutoa wachezaji kwenda kuzitumikia timu za taifa katika Fainali za Kombe la Dunia tu, hivi sasa fedha zitatolewa kwa klabu ambazo zinatoa wachezaji wake kwa timu tofauti za taifa kwenda kutumika katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia ambazo huwa zinachezwa katika mabara sita duniani.

Kutekeleza mpango huo kwa hivi sasa, FIFA imetenga kiasi cha Dola 355 milioni ambacho kitagawanywa kwa klabu ambazo wachezaji wake wameshiriki mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Kiasi hicho cha Dola 355 milioni (Sh873 bilioni) ni ongezeko linakalokaribia asilimia 70 ya fungu ambalo FIFA ilitoa kwa klabu ambazo wachezaji wao walishiriki Fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar.

“Awamu iliyoboreshwa ya Mpango wa Kunufaisha Klabu wa FIFA kwa Kombe la Dunia la 2026. inaenda hatua zaidi kwa kutambua mchango mkubwa ambao klabu nyingi na wachezaji wao duniani kote hutoa kwa upangaji wa mechi za mtoano na fainali za mwisho.

“Rekodi ya fedha kiasi cha Dola 355 milioni kitagawiwa kwa klabu kwa ajili ya kuwaachia  wachezaji wao. Hii inaimarisha ushirikiano wetu thabiti na Chama cha Klabu za Ulaya na Klabu ulimwenguni kote kwani sote tunatazamia toleo la msingi na linalojumuisha kimataifa la Kombe la Dunia la FIFA mwaka ujao,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa FIFA, kiasi hicho cha fedha kitaingizwa moja kwa moja katika akaunti za klabu.

Ikumbukwe Simba, Yanga na Azam kwa hapa nchini ndio klabu ambazo zimekuwa zikitoa idadi kubwa ya wachezaji kwenda kuzitumikia timu za taifa katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Yanga imetoa wachezaji ambao wamezitumikia timu za Taifa za Tanzana, Kenya, Chad na Mali huku Simba yenyewe ikiwa na wachezaji wanaozitumikia Taifa Stars, Uganda na Guinea.

Timu nyingine ambazo zimetoa wachezaji kwenda kuzitumikia timu za taifa katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia ni Azam, Singida Black Stars, KMC na JKT Tanzania.

Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasugula alisema kuwa habari hiyo ni njema kwa upande wa klabu.

“Kama ni kweli basi ni habari njema ukizingatia tunaziendesha hizi klabu kwa ugumu sana kutokana na changamoto ya kiuchumi, hivyo hilo jambo kama lipo litasaidia klabu kwa namna fulani.

“Lakini pia itasaidia kuhamasisha zaidi wachezaji kufanya vyema ili wapate fursa ya kuwemo katika timu za taifa,” alisema Mwakasungula.

Wakati zikipata habari hiyo njema kutoka FIFA, Yanga, Simba na Singida Black Stars jana ziliondoka Tanzania na kuwasili salama katika nchi za Angola, Botswana na Rwanda ambako zitacheza mechi za kwanza za hatua ya awali ya mashindano ya Klabu Afrika.

Yanga ipo Angola ambako itaumana na Wiliete Benguela kesho Ijumaa, huku Simba ikiwa Botswana ambako Jumamosi itakabiliana na Gaborone United ya huko.

Singida Black Stars imejikita Rwanda ambako itakabiliana na Rayon Sports. Awali Azam ilikuwa ya kwanza kwenda Sudan Kusini kukabiliana na Al Merreikh, Jumamosi.