Februari 5, 1967, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akiwa mkoani Arusha, alilitangaza rasmi Azimio la Arusha.
Watanzania mikoa yote walijitokea kuunga mkono kwa namna mbalimbali. Sehemu nyingi njia iliyotumika ilikuwa ya matembezi ya mshikamano.
Umbali kutoka Kijiji cha Mwanhala hadi Nzega Mjini (wilayani) ni kilometa 24.
Wanakijiji wa Mwanhala walitembea wakiwa kundi kubwa hadi Nzega Mjini kuunga mkono Azimio la Arusha. Katika msafara huo wa wanakijiji, alikuwepo mtoto mwenye umri wa miaka tisa. Jina lake ni Georges.
Gabriel Bussungu ni baba mzazi wa Georges, alikuwa miongoni mwa wanakijiji cha Mwanahala walioandamana kuunga mkono Azimio la Arusha.
Wanakijiji walikuwa wengi katika matembezi hayo, kwa hiyo Gabriel hakumwona Georges. Msafara ulipokuwa unakaribia kuwasili Nzega Mjini, Gabriel alimwona Georges, akahamaki akataka kumwadhibu.
Gabriel mwenye hasira akiwa amekamia kumwadhibu Georges, mara macho yake yalimtazama mwanamke shujaa wa Uhuru wa Tanganyika, Amina Maufi ambaye ni mwasisi wa Tanu (Tanganyika African National Union), vilevile alipata kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Tanu.
Amina alikuwa Nzega Mjini akisubiri kuupokea msafara huo kutoka Kijiji cha Mwanhala.
Wakati Amina anapokea msafara, macho yake kwa haraka yalitua kwa Georges.
Ooh! Amina alisisimka mwili kwa furaha. Akamshika Georges, akambeba. Aliomba kumjua mzazi wa Georges mara Gabriel akajitokeza.
Amina alimpongeza Gabriel kwa malezi bora. Kwa tafsiri ya bibi Amina, ilihitaji msingi bora wa wazazi kwa mtoto kutembea kilometa 24 kuunga mkono Azimio la Arusha.
Gabriel alipokea pongezi na hasira zilimwisha, akapona adhabu. Alirejea nyumbani akiwa shujaa baada ya wazazi wake kupongezwa na Amina.
Baada ya kuwasili Mwanhala, Gabriel aliwaza kuendelea kulea watoto wake vizuri ili asifiwe tena na tena.
Georges baada ya kufika Mwanhala, akili yake iliwaza tofauti, alitamani kuwa mwanasiasa.
Georges anayetajwa hapa ndiye Georges Gabriel Bussungu, ambaye Agosti 27, 2025, aliteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Uchaguzi Mkuu 2025 kwa tiketi ya Ada Tadea.
Kutoka mwaka 1967 mpaka 2025 ni miaka 58 iliyotimia. Miaka hiyo inawakilisha kipindi ambacho damu ya siasa imekuwa ikizunguka ndani ya Bussungu.
Mwaka 1969, ikiwa ni miaka mwili baada ya Azimio la Arusha, Bussungu alijisajili na kupata kadi ya uanachama wa Umoja wa Vijana Tanu. Wakati huo, Bussungu alikuwa anasoma shule ya kati (middle school), iliyokuwa daraja la pili katika masomo ya shule ya msingi.
Bussungu alikuwa anasoma Mwanhala Middle School. Wakati anaingia shuleni hapo, hakukuwa na mwamko wa siasa. Bussungu aliwashawishi wanafunzi wenzake, wakaanzisha tawi la Umoja wa Vijana Tanu. Bussungu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tawi hilo.
Mwaka 1970, Bussungu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chipukizi Tanu, Wilaya ya Nzega.
Aliongoza kwa mwaka mmoja, kabla ya kukabidhi kijiti mwaka 1971. Huo ni wasifu wa Bussungu ambaye ameingia kwenye kinyang’anyiro cha urais 2025, yupo kwenye siasa tangu mwaka 1967.
Aprili 23, 1957, kwenye Zahanati ya Makongoro, Wilaya ya Nyamagana, Mwanza, mwanamke aliyekuwa mjamzito, Modesta Manugwa Nabeji, alijifungua salama mtoto wa kiume.
Mume wa Modesta, Gabriel Fille Bussungu, alimpa jina Georges mtoto aliyezaliwa.
Kiasili, Gabriel Bussungu ni mwenyeji wa Misungwi, Mwanza.
Hata hivyo, majukumu yake ya kikazi, yalisababisha awe anahamishwa wilaya moja hadi nyingine. Alikuwa mwalimu na baadaye ofisa kilimo.
Mwaka 1962, Gabriel Busungu alihamishiwa Wilaya ya Nzega, akiwa Meneja wa Kituo Kidogo cha Kilimo. Hiyo ndiyo sababu maisha ya Georges Bussungu, kuanza kujengwa utotoni kijijini Mwanhala.
Mwaka 1964, Bussungu alianza darasa la kwanza, Shule ya Msingi Utwigu Lower. Mwaka 1967 alimaliza darasa la nne. Bussungu alipata ufaulu mzuri kwenye mitihani ya darasa la nne, hivyo alichaguliwa kuendelea na masomo ya shule ya kati, Mwanhala Middle School, kuanzia mwaka 1968 na alihitimu darasa la nane mwaka 1971.
Mwaka 1972, Bussungu alisoma Shule ya Sekondari Lake, Mwanza. Mwaka 1973, Bussungu akiwa kidato cha pili, alihamia Shule ya Sekondari Kazima, Tabora.
Elimu ya sekondari alihitimu Kazima mwaka 1975. Kisha, alijiunga na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dar es Salaam mwaka 1976, alikosomea Masomo ya Biashara.
Mwishoni mwa mwaka 1976, Bussungu alipata ajira yake ya kwanza Wizara ya Viwanda na Biashara, akiwa Msaidizi wa Biashara daraja la tatu.
Mwaka 1977, Bussungu alirejea chuoni, alidahiliwa Chuo cha Ushirika Moshi, alikosomea stashahada ya Uongozi na Uhasibu. Alihitimu stahahada (diploma) yake mwaka 1979.
Alipomaliza masomo ya diploma, Bussungu hakurejea kazini kwake, badala yake alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Alikaa jeshini mwaka mzima, akiwa kambi mbili, Bulombola, Kigoma na Mgambo, iliyopo Kabuku, Tanga. Mwaka huo, 1979, Tanzania ilikuwa kwenye Vita ya Kagera dhidi ya Idi Amin Dada. Bussungu alikuwa jeshini wakati wa vita.
Mwaka 1980, Bussungu alirejea Chuo cha Ushirika Moshi, alikosomea stashahada ya juu ya Uongozi wa Ushirika, aliyohitimu mwaka 1981. Baada ya kutunukiwa stashahada ya juu ya Uongozi wa Ushirika, Bussungu alipanda cheo na alipangiwa kazi kuwa Ofisa Biashara katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Mwaka 1983, Bussungu alihamishiwa Musoma, Mara, akiwa Ofisa Biashara wa Mji wa Musoma. Mwaka 1984, alipanda tena ngazi kuwa Ofisa Biashara Msaidizi, Mkoa wa Mara. Mwaka 1985, Bussungu alijiunga na Chuo cha IDM Mzumbe, alikosomea stashahada ya umahiri wa Uongozi, aliyohitimu mwaka 1986.
Kuanzia mwaka 1988, IDM Mzumbe, Bussungu alisoma shahada ya uzamili ya Uongozi wa Biashara, ambayo alihitimu mwaka 1990. Hapa Bussungu anataka rekodi ikawa sawa kwamba yeye ndiyo mhitimu wa kwanza wa shahada ya uzamili, Chuo cha Mzumbe.
Tangu alipochukua kadi ya uanachama ya Umoja wa Vijana Tanu mwaka 1969, Bussungu aliendelea kuwa mwanasiasa. Mwaka 1971, alichukua kadi ya uanachama wa Tanu. Februari 5, 1977, Bussungu alikuwa mmoja Watanzania waliobadili kadi zao za uanachama, kutoka Tanu hadi Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya vyama vya Tanu na ASP (Afro Shiraz Party), kuungana na kupatikana CCM.
Mwaka 2019, Bussungu akiwa mwanaCCM mwenye historia tangu Tanu, alijitokeza kugombea uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM. Jina la Bussungu halikurudi baada ya chujio la Kamati Kuu. Hivyo, alienguliwa kuwa mgombea. Pamoja na hivyo, aliendelea kubaki CCM.
Mwaka 2021, Bussungu aliachana na CCM, akajiunga na Ada Tadea.
Februari 2022, Bussungu aligombea uspika wa Bunge, baada ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kujiuzulu na kuacha kiti wazi.
Bussungu hakupata kura hata moja katika uchaguzi wa spika. Alirejea kwenye chama chake cha Ada Tadea, ambacho kilifanya uchaguzi mkuu mwaka huo (2022), alishinda unaibu katibu mkuu.
Mei 10, 2025, Bussungu aliteuliwa na chama chake kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bussungu ni baba wa familia yenye mke na watoto 10. Mkewe anaitwa Yasinta Medard Chuleha, watoto wake ni Gloria, Georgina, Gabriel, Gertrude, Gerald, Godfrida, Gladness, Gilian, Geofrey na Grace. Bussungu anasema, alishukiwa na malaika, akafunuliwa watoto wake wote awape majina yenye kuanza na herufi G.
Oktoba 29, 2025, Watanzania watapiga kura kumchagua Rais wao, wabunge na madiwani. Zanzibar atachaguliwa Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wabunge na madiwani. Kipindi hiki kampeni zinaendelea, Bussungu anawaangukia Watanzania ili afanye mapinduzi ambayo anayaita ya njano.
Bussungu anasema akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ataleta mapinduzi aina ya tatu. Mapinduzi ya kifikra, teknolojia na uchumi. Anaeleza kuwa ataweka mkazo kwenye mapinduzi hayo, kwa sababu ndicho Tanzania inahitaji ili kutoka ilipo na kusonga mbele kwa kasi.
Katika kuleta mapinduzi anayoyakusudia, Bussungu anaahidi kutumia falsafa yake ya U-tano, ambayo ni Utafiti, Ubunifu, Uzalishaji, Uuzaji na Uwajibikaji. Anasema utekelezaji wa U-tano utaifanya Tanzania ibadilike kwa muda mfupi na Watanzania wataona matokeo chanya mapema.
Bussungu anasema, Mwalimu Nyerere alitangaza maadui watatu, Ujinga, Maradhi na Umaskini. Kwa upande wa Bussungu, anaona hao siyo maadui tena, maana hivi sasa Tanzania ina wasomi, maprofesa wengi, huduma za afya ni bora, hadi kuna utalii wa matibabu, watu wa nchi nyingine wanakuja kutibiwa. Anasema, umaskini ndiyo unaongezeka.
Sababu ya mkwamo huo, Bussungu anatumia neno lenye herufi tatu, “URU” kwamba ndiyo chanzo cha umaskini Tanzania kuendelea kushamiri licha kupiga hatua kwenye utoaji elimu na huduma za afya. Kuhusu URU, Busungu anafafanua kwamba ni Upendeleo, Rushwa na Uwajibikaji.
Anasema, upendeleo bila kuzingatia sifa ni jambo ambalo linaiumiza nchi. Rushwa ni adui mkuu wa Taifa. Wafanyakazi serikalini na mashirika ya umma kutowajibika ni saratani inayoitesa nchi.
Bussungu anasema bila kushughulikia URU, nchi haitakwenda popote. Anaahidi kuikabili na kuitokomeza rushwa, kufuta upendeleo na uwajibikaji utakuwa wa hali ya juu endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.