TANGU msimu wa 2013-14 ambao Azam FC ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni mara ya kwanza kwao, wamepita makocha mbalimbali kuifukuzia rekodi hiyo, wameshindwa.
Mzigo huo sasa umeangukia kwa Florent Ibenge, kocha mwenye rekodi kubwa katika soka la Afrika kutokana na kushinda mataji yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Ibenge ana mtihani wa kuifanya Azam kuwa mshindani wa kweli kwenye michuano ya ndani mbele ya wakongwe, Yanga na Simba ambao wamekuwa na mtindo wa kubadilishana taji la Ligi Kuu Bara tangu wakati huo ambao Azam ilichukua mara ya mwisho.
Kabla ya Azam haijachukua msimu huo, Yanga na Simba zilikuwa ziki-badilishana tangu mwaka 1989 hadi 1999 na 2000 Mtibwa Sugar ilipowatibulia, lakini wakaendeleza moto wao hadi pale Azam ilipoingilia kati.
Hata hivyo, utawala wa Yanga na Simba katika Ligi Kuu Bara, umeitia hasira Azam, timu iliyoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 2008, huku msimu huu ukiwa ni wa 18.
Jambo la kwanza ambalo Ibenge anajivunia katika kuifanya kazi yake, ni kubaki kwa kiungo aliyeibuka kinara wa asisti katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyeongeza mkataba hadi 2027 baada ya kuwepo kwa taarifa nyingi za kutakiwa na Simba, Yanga sambamba na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Kubaki kwa Fei Toto ambaye misimu miwili aliyoitumikia Azam akitokea Yanga, amekuwa na mchango mkubwa katika kufunga mabao, ule wa kwanza 2023-2024 alifunga 19, mawili nyuma ya kinara Aziz Ki (21), pia asisti saba, kisha 2024-2025 akafunga manne na asisti 13.
Msimu bora zaidi kwa Azam FC ulikuwa ni ule wa 2013-2014 ambao ilimaliza kwa kutwaa ubingwa mbele ya Yanga iliyoshika nafasi ya pili, huku Simba ikiwa ya nne. Mbeya City ya tatu.
Pia timu hiyo imemaliza katika nafasi ya pili mara sita ambazo ni misimu ya 2011-12, 2012-13, 2014-15, 2015-16, 2017-18 na 2023-24.
Katika nafasi ya tatu, imemaliza mara nane ikiwa ni katika misimu ya 2009-10, 2010-11, 2018-19, 2019-20, 2020-21, 2021-22, 2022-23, 2024-25. Msimu wa kwanza 2008-09 ilimaliza nafasi ya nane, huku ule wa 2016-2017 ikimaliza nafasi ya nne.
Ndani ya kikosi cha Azam, kuna wachezaji wameondoka kutokana na sababu mbalimbali. Wapo waliofikia maku-baliano ya kusitisha mikataba, kutolewa kwa mkopo na mikataba yao kumalizika.
Waliotolewa kwa mkopo ni Abdallah Kheri Sebo aliyepelekwa Pamba Jiji, Hamis Yasin (KMC), Ally Hassan (Mbeya City) na Abdulkarim Kiswanya (Namungo).
Walioagwa kwamba hawatakuwa mali ya timu hiyo ni Jhonier Blanco, Mamadou Samake, Frank Tiesse, Ever Meza, Sospeter Bajana na Mohamed Mustafa.
Wakati hao wakiondoka, kuna majembe mapya 11 yametua katika nafasi mbalimbali wakiwamo makipa wawili, Issa Fofana na Aishi Manula. Mabeki ni Lameck Lawi na Edward Manyama. Viungo kuna Himid Mao na Sadio Kanoute. Mawinga Baraket Hmidi na Pape Doudou Diallo, wakati washambuliaji ni Taieb Ben Zitoun, Jephte Kitambala na Muhsini Malima.
Florent Ibenge ndiye kocha mkuu wa Azam FC, huku wasaidizi wake ni Addis Worku, Anicet Kiazayidi na Kassim Liogope. Wengine wanaounda benchi hilo la ufundi ni Mehdi Marzouk na Murshid Kika ambao ni makocha wa utimamu, Rody Mountaro (kocha wa makipa) na Omar Boukathem (mchambuzi wa video).
Hivi karibuni, Ibenge aliliambia Mwanaspoti kuwa hadi Ligi Kuu ianze, anaiona timu hiyo ikizipa upinzani Simba na Yanga, huku akiahidi makubwa kwa kikosi chake.
Pia amekiri Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa imekuwa bora akieleza kwamba ikiwa msimu wake wa kwanza kufanya kazi hapa nchini anahitaji kuendana na ubora na ushindani huo. Ibenge aliyasema hayo Septemba 6, mwaka huu baada ya kutoka kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mbeya City na kushinda 2-0.
“Naendelea kusuka timu na kutengeneza muunganiko, Ligi ya Tanzania ni bora na tumeona kwenye CHAN hali ilivyokuwa na hata Simba na Yanga zimecheza fainali Kombe la Shirikisho Afrika, nahitaji kuendana na ushindani huu kwa muda ambao nimeanza kufanya kazi hapa nchini,” anasema kocha huyo.