Jamhuri ilivyojibu mapigo pingamizi la Lissu kesi ya uhaini

Dar es Salaam. Upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, umeiomba Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kutupilia mbali pingamizi aliloweka mshtakiwa kuhusu hati ya mashtaka kwa madai kuwa hakuonyesha ni wapi hasa kwenye kasoro.

Maombi hayo yamewasilishwa leo, Alhamisi Septemba 18, 2025, na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, wakati akijibu hoja za pingamizi la Lissu.

Katuga amedai kwamba iwapo hati hiyo ya mashtaka ingekuwa na upungufu, mshtakiwa alitakiwa kuyaainisha kwa kuyataja moja kwa moja, jambo ambalo hajalifanya, hivyo hana sifa za kupinga.

Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kinachotokana na maneno aliyoyatamka kuhusu kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Inadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania kwa nia ya uchochezi, Lissu alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu huo.

Aidha, anadaiwa kutoa kauli za kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania, akisema miongoni mwa maneno yafuatayo:”Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (Kiongozi wa jopo), James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde.

Akijibu hoja za pingamizi, Katuga ameeleza kuwa hati ya mashtaka haina upungufu kwa kuwa imetayarishwa chini ya kifungu cha 138 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ambacho hakiruhusu pingamizi katika hatua ya usikilizaji wa awali.

Amefafanua kuwa kifungu cha 138(a)(1) kinaeleza wazi kuwa hati ya mashtaka lazima ianze na maelezo ya kosa, huku 138(a)(2) kikielekeza iandikwe kwa lugha ya kawaida ili kuepuka kutumia maneno ya kitaalamu.

Vilevile, 138(a)(3) kinafafanua kuwa maelezo ya kosa lazima yaeleze nani, lini, wapi na vipi kosa lilivyotendwa, na maelezo hayo yote yapo kwenye hati ya mashtaka.

Kuhusu kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2022, ambacho ndicho kinachotumika kumshtaki Lissu, Katuga ameeleza kuwa kifungu hicho kinabainisha viini vinavyounda kosa la uhaini.

“Hivyo, kwa kupitia kifungu cha 39, waheshimiwa majaji, mtaona viini mbali na hivi nilivyovitaja,” ameeleza.

Wakili wa Serikali, Katuga, amefafanua kuwa hata mtu anapokuwa nje ya nchi, anaweza kutengeneza au kuchochea nia ya kutenda, kushawishi au kushauri mtu au kundi la watu kutekeleza vitendo vinavyolenga kutishia Bunge au Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amedai kuwa mtuhumiwa atadhihirisha nia hiyo kupitia kuchapisha maandishi au kwa njia nyingine yoyote, na endapo itathibitika amefanya hivyo, atakuwa ametenda kosa la uhaini ambalo adhabu yake ni kunyongwa.

“Kwa mujibu wa maneno yaliyotumika, kifungu kinachomrejelea mshtakiwa kinaainisha makosa 13, lakini yeye alidai yapo 10 tu,” amesema Katuga.

Aidha, amesisitiza kuwa hati ya mashtaka inamtaja mshtakiwa kwa jina, ikionesha akiwa Kinondoni na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alichochea vitendo husika, huku maneno mengine yakiachwa na kuonesha nia ya kuchochea umma kuzuia uchaguzi wa mwaka 2025.

Katuga amebainisha kuwa kudhihirisha nia ya kutenda kosa la uhaini kunahusisha mambo mawili; kwanza, kuchapisha maandishi au kuchora mchoro unaoonesha nia hiyo, na pili, vitendo vya moja kwa moja vinavyothibitisha kosa hilo.

Amedai kuwa maneno ya mshtakiwa yalilenga kuitishia Serikali na hakuna popote kwenye hati ya mashtaka palipoeleza kuwa anashtakiwa kwa kuzuia uchaguzi. Akasema iwapo mshtakiwa angesikiliza kwa makini wakati anasomewa, angeelewa hoja hiyo.

Kuhusu hoja ya wakili wa utetezi kwamba kuzuia uchaguzi si kosa la uhaini, Katuga amejibu kuwa mshtakiwa anashtakiwa kwa kutengeneza nia na kuidhihirisha kupitia kuchapisha taarifa yenye lengo la kuitishia Serikali.

Vilevile, akijibu madai ya Lissu kwamba hakuna sehemu ambayo Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wametajwa katika hati ya mashtaka, Katuga amesema suala la kuwataja au kutowataja ni jambo la ushahidi litakalothibitishwa na Mahakama baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi wake.

Kuhusu tofauti kati ya hati ya mashtaka iliyosomwa Mahakama ya Kisutu na ile ya Mahakama Kuu, Katuga ameeleza kuwa hati ya Kisutu ilikuwa ya awali chini ya kifungu cha 262(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), ikibainisha pendekezo la kosa la uhaini.

Amefafanua kuwa mabadiliko ya hati za mashtaka yanaruhusiwa kisheria kwa mujibu wa vifungu vya 251 na 254 vya CPA, na Mahakama haina utashi wa kuzuia marekebisho hayo.

Katuga ameongeza kuwa Mahakama ya Kisutu ilikuwa na mamlaka ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo, lakini haina mamlaka ya kufanya marekebisho ya hati ya mashtaka.

“Kifungu cha 262(6) CPA kinaeleza kuwa DPP anapothibitisha ushahidi unaojitosheleza, ataandaa hati ya mashtaka na kuwasilisha Mahakama Kuu pamoja na maelezo ya mashahidi na nyaraka husika. Kifungu hiki kinahusu kesi zinazohusika Mahakama Kuu,” amesema Katuga.

Ameongeza kuwa baada ya maandalizi ya hati ya mashtaka kuwasilishwa Mahakama Kuu, ndipo hupunguzwa chini kwa kusomwa kupitia mchakato wa committal proceedings chini ya kifungu cha 263 CPA.

Katuga amebainisha kuwa hati ya mashtaka iliyosomwa kwa maelezo ya mashahidi na vielelezo ni ile iliyosajiliwa Mahakama Kuu, na ndiyo yenye mamlaka ya kufanyiwa marekebisho kwa mujibu wa kifungu cha 263 CPA. Kesi imeahirishwa hadi Jumatatu, Septemba 22, 2025 ambapo Mahakama itatoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo.