Dar es Salaam. Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema)Tundu Lissu, itaendelea leo katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde, itaendelea leo Septemba 18, 2025 kwa upande wa Jamhuri kujibu hoja na pingamizi iliyowekewa na Lissu, Septemba 16, 2025
Lissu, aliibua hoja mpya dhidi ya mashahidi wa Jamhuri wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo inayomkabili, akidai kuwa hawastahili kisheria kufika mahakamani kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo.
Aliibua hoja hiyo mpya wakati wa mwendelezo wa usikilizwaji wa pingamizi lake kuhusiana na uhalali wa hati ya mashtaka.
Hii ni sababu mpya au hoja mpya aliyoiongeza siku hiyo katika sababu za awali za pingamizi lake hilo na kufanya kuwa na sababu tatu za kupinga kesi hiyo.
Katika hoja zake Lissu amesema kuwa mashahidi hao wa Jamhuri walioorodheshwa hawastahili kisheria kutoa ushahidi wao katika kesi hiyo kwa kuwa maelezo ya ushahidi wao yaliyowasilishwa mahakamani ni batili kutokana na kuandaliwa na kinyume cha sheria.
Akihitimisha hoja hizo za kupinga kesi hiyo ameieleza mahakama kuwa ameonewa kwa kuwa hana hatia na hajamkosea mtu yeyote bali ameshtakiwa na kukaa mahabusu muda wote mpaka sasa kwa kosa lisilokuwepo.
Siku hiyo aliisihi Mahakama hiyo kukomesha huo anaodai ni uonevu dhidi yake, kwa kutenda haki.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Itakumbukwa kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali Septemba 8, 2025, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam lakini Lissu aliibua pingamizi akiiomba mahakama hiyo isiisikilize kesi hiyo bali iifute akitoa sababu mbili ikiwamo ubatili wa hati ya mashtaka na uhalali wa mamlaka ya mahakama hiyo kama inaweza kusikiliza kesi ya uhaini.
Septemba 15, 2025 mahakama hiyo ilitoa uamuzi ambapo iliitupilia mbali sababu ya Mahakama kutokuwa na mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.
Baada ya uamuzi ndipo Lissu akaleta hoja nyingine ya ubatili wa hati ya mashtaka ambayo ameendelea nayo leo, huku akiibua sababu hiyo mpya ya tatu ya pingamizi kuwa maelezo ya mashahidi hao yaliyosomwa katika Mahakama ya Ukabidhi (committal court),katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu ni batili.
Kuhusu hoja hiyo amedai kuwa maelezo ya mashahidi 10 ambao ni maofisa wa Polisi yana kasoro za kisheria kwa kuwa wameandika, kujionya na kujithibitisha wenyewe wakati utaratibu unataka waende kuthibitishwa mbele ya ofisa mwingine wa Polisi.
Lissu amedai Mahakama Kuu ilitoa amri ya kulinda mashahidi ambao sio maofisa wa Polisi kwa kuficha anuani zao, makazi yao, ndugu zao na ajira zao, lakini katika maelezo ya mashahidi aliyopewa, amri hiyo ya kuwaficha mashahidi haikutekelezwa kwani kuna baadhi ya mashahidi wamewekwa hadi namba zao za simu, “Huku ni kukiuka amri iliyotolewa na mahakama Kuu.”