KAMATI UTEKELEZAJI MKAKATI WA MUDA WA KATI WA MAPATO MIAKA 3 WAZINDULIWA DODOMA.

Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt Natu Mwamba amesema kuwa lengo kuu la Mkakati wa muda wa kati wa Mapato ni pamoja na kuweka misingi imara katika ukusanyaji wa Mapato,kuongeza makusanyo,kutambua na kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi pamoja na kuimarisha imani kwa Wananchi na Wawekezaji katika mfumo wa Mapato.

Dkt Mwamba ameyaeleza hayo leo Jijini Dodoma Septemba 18,2025 katika Uzinduzi wa Kamati za Usimamizi na Utekelezaji wa Mkakati wa Muda wa kati wa Mapato ya miaka 3 kwa mwaka 2025/26 hadi 2027/28.

Na kuongeza kuwa utekelezaji huu utaboresha usimamizi wa Mapato ya Serikali kwa kuhakikisha kuwa bajeti inakuwa endelevu itakayopelekea Serikali kuongeza kasi ya utoaji huduma muhimu kwa Wananchi kwa kutumia Mapato ya Ndani.

“Utekelezaji wa Mkakati huu una lengo la kuweka misingi imara ya ukusanyaji wa mapato,kuweka utabirifu wa Sera za Mapato, kuongeza makusanyo ya mapato,kuongeza uhiyari wa ulipaji kodi,kutambua na kuziba mianya ya ukwepaji kodi,kupunguza nakisi za bajeti na kuimarisha imani ya Wananchi na Wawekezaji katika mfumo wa Mapato”.

Naye Dkt Johnson Nyella ambaye ni Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera ametumia wasaa huu kuzikumbusha Kamati hizo kuwa Kamati tendaji na Kamati ya Wataalam kwani majukumu ya Kamati hizo ni kuweka misingi imara ya ukusanyaji kodi na kutambua na kuziba mianya ya ukwepaji kodi huku lengo likiwa ni kuwa na uwezo wa kupata Mapato kutoka ndani ya Nchi yetu na kuweza kujitegemea wenyewe kama Nchi na kuwa na Maendeleo bila kuwategemea watu wengine.

Mkakati huu umeandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wengine mbalimbali wakiwemo Washiriki wa Maendeleo na Wadau wengine kutoka Taasisi za Serikali na Sekta binafsi ambapo umeainisha maboresho ya Mikakati na hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikiendelea kutekelezwa na Serikali katika kuhakikisha Serikali inakusanya Mapato mengi kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani.