DABI ya kwanza ya Kariakoo msimu huu imemalizika kibabe baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba, juzi Jumanne.
Ushindi huo umeifanya Yanga, kuendeleza ubabe mbele ya Simba, ikishinda mchezo wa sita mfululizo dhidi ya watani wao hao, rekodi ambayo itaendelea kuwafanya Wekundu kuumizwa na maumivu mithili ya kidonda kisichopona.
Hata hivyo, kuna mambo mbalimbali yalitokea ndani ya uwanja huku kipa wa Yanga, Djigui Diarra akionekana kuwa mwiba mchungu kwa Simba kutokana na uimara wake golini.
Makipa wote walicheza vizuri, lakini ushindi wa Yanga umechangiwa kwa kiasi kikubwa bna ushujaa wa Diarra ambaye alikuwa na mechi nyingine bora kabisa.
Diarra alifanya kazi kubwa tatu akiokoa nafasi mbili za Simba kupitia mashambulizi ya Kibu Denis na Shomari Kapombe, kipindi cha kwanza ambayo wote alikutana nayo uso kwa uso, kisha akaweka ugumu wa mpira kwenda wavuni.
Kama haitoshi, kipindi cha pili akazuia mabao mengine mawili kupitia kichwa cha Kibu na shuti la Seleman Mwalimu, yote na kuwa kona ambazo hazikuzaa bao lolote.
Huu ni muendelezo wa ubora kwa Diarra, kwani msimu uliopita straika Leonel Ateba alibaki uso kwa uso na kipa huyo, lakini ‘Screen Protector’ akaingia uvunguni na kuudaka mpira ambao kila mtu aliamini lingekuwa ni bao la kuongoza kwa Simba.
Ubora wa Diarra juzi uliibakisha Yanga mchezoni, ambapo kama angeruhusu mabao ya mapema, presha ingekuwa kubwa kwao.
ATAKAVYOWAPASUA KICHWA YANGA
Diarra ambaye mkataba wake msimu huu unakwenda ukingoni, huenda akawa mchezaji atakayewapasua vichwa mabosi wa Yanga, kwani tangu atue ndani ya kikosi hicho ameonyesha ubora usiotetereka kila anapopewa nafasi.
Lakini kiwango chake kimeendelea kumpa nafasi kwa makocha wote waliofundisha kikosi hicho kuanzia Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead Ramovic, Miloud Hamdi mpaka sasa Romain Folz, huku akitajwa kama kipa bora aliyeleta zama mpya katika ligi.
Kama msimu huu pia atauwasha, basi mabosi wa Yanga watapambana na ofa nyingi nzuri zitakazofika mezani kwani kama hawatamuwahi, anaweza kuwapa presha baadaye ya kusaka mbadala wake.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa kocha mpya wa Yanga, Romain Folz, ambaye kikosi hicho kikiwa chini yake, kimeichapa Simba.
Matokeo hayo yatamshusha presha kocha huyo Mfaransa, ambapo ilionyesha kwamba bao hilo lilikuwa na maana kubwa, alikimbia umbali mrefu mpaka kwenye kona ya kibendera akishangilia, baada ya kutotulia kwenye benchi lake, huku akiwapa maelekezo wachezaji wake.
Yanga wachezaji wake wengi walicheza vizuri, lakini wako ambao walifanya vizuri zaidi, ukiondoa Diarra, kuna viungo Aziz Andabwile na Mohamed Doumbia walikuwa bora.
Andabwile licha ya huo kuwa mchezo wake wa kwanza akianza dhidi ya Simba, alionyesha ubora mkubwa akiwapa nguvu kubwa mabeki wa Yanga ambao alikuwa mbele yao, akitibua hesabu zote za wapinzani kutoka katikati ya uwanja.
Kipindi cha pili Yanga ilimuingiza Doumbia, ambaye pia alikuwa anapiga pasi nyingi za kwenda mbele ambazo ziliufungua ukuta wa Simba.
Wamo pia beki Dickson Job, aliyekuwa bora kufunga njia za mashambulizi ya Simba hata Duke Abuya eneo la kiungo cha kati.
De REUCK, CAMARA FRESHI SIMBA
Simba licha ya kupoteza mechi ya sita mfululizo za dabi hiyo, ilicheza vyema mechi hiyo juzi ikifanya mashambulizi mengi.
Beki wa kati mpya, Rushine De Reuck, ambaye alikuwa na dakika 90 za kwanza bora dhidi ya Yanga, alicheza kwa hesabu kubwa, haikuwa rahisi kwa wapinzani kupita kwake.
Kipa wa Simba Moussa Camara, alikuwa na dakika 90 bora sawa na wajina wake Naby Camara, ambaye licha ya kucheza nafasi mbili ndani ya dakika 90 akianza kama beki wa kushoto na baadaye kiungo lakini alikuwa imara.
Kipa Camara alifanya vizuri, unakumbuka lile shuti la Pacome Zouzoua akimchungulia kwa mbali? Kipa huyo aliupangua kiufundi na kuwa kona.
Bao ambalo Simba iliruhusu ukiondoa utata wa kama lilikuwa ni la kuotea ama sio, lilionyesha udhaifu kwa Wekundu, kwani licha ya kuwa wengi kwenye eneo lao golini wakiwa nane, lakini walishindwa kuwazuia vizuri wachezaji watano wa Yanga.
Simba walishindwa kuwabana vizuri Yanga na kujikuta wanajichanganya na kuruhusu bao hilo kirahisi.
Angalau Simba ingeanza na mshambuliaji Seleman Mwalimu, ambaye licha ya kuingia dakika za mwisho alionyesha utulivu, lakini Steven Mukwala ambaye alianza mchezo huo alikosa ubora wa kuwasumbua mabeki wa Yanga.
Nafasi nzuri za kufunga Simba ilizitengeneza kwa kuwatumia mabeki na viungo, lakini hakuwa Mukwala ambaye muda mrefu alikuwa akipambana na kocha wake Fadlu Davids akimuelekeza namna ya kucheza.
Beki wa Simba, Abdulrazack Hamza, alishindwa kumaliza dakika 90 zingine juzi, baada ya kuumia kichwani akipasuka kisha kutolewa dakika ya 24 kipindi cha kwanza.
Itakumbukwa Hamza amewahi kukosa kabisa mechi kama hiyo msimu uliopita, kutokana na majeraha ambapo mashabiki wa Simba walianza kufurahia uwepo wake uwanjani akionyesha kiwango kizuri na mara moja ilibaki kidogo afunge kwa kichwa.
Simba mastaa wake wawili Jean Charles Ahoua na Ellie Mpanzu, ambao kwenye mechi zingine wamekuwa moto, lakini juzi haikuwa hivyo.
Shida ya mastaa hao haikuonekana, lakini unaweza kuangalia mchezo huo na usijue kama Mpanzu na Ahoua wapo, kwani hawakufanya kazi kubwa sawa na viwango vyao. Kwa ufupi walicheza kawaida.
Simba imefungwa mara sita mfululizo na Yanga, lakini kati ya mechi hizo nne ni chini ya kocha Fadlu, na haijapata bao hata moja.
Hata hivyo Fadlu, ameonyesha anaendelea kusuka timu imara kwani, juzi ilicheza vizuri lakini ikakosa matokeo tu, mashabiki wa Simba wanataka ushindi shida itaanzia hapo.
Lakini kwa upande wa kikosi kilichoisumbua Yanga, basi wamefanikiwa kwani kipindi cha kwanza chote kilikuwa cha jasho na damu kote kulikuwa kumefunga, hakuna pa kupita.
Unaweza kusema ni moja kati ya mechi kubwa, yenye ushindani unaoonyesha nguvu ya usajili mzito uliofanywa na mabosi wa klabu hizi, huenda dabi za msimu huu zitakuwa ngumu kuliko zilizopita kama vikosi vyote vitaendelea kujinoa.