MATAJI aliyoyapata Rehema Said katika mashindano ya kimataifa ya tenisi kwa walemavu 2025 (International Tennis Federation Wheelchair Tournament), yamempa nguvu mwanadada huyo katika kufanya makubwa zaidi katika michuano mingine ijayo.
Mashindano hayo ya mwaka huu yalifanyikia jijini Nairobi, Kenya na Regema alishinda mataji matatu, moja ya binafsi na mengine mawili ya kushindana dhidi ya wachezaji kutoka nchi nane, Kenya, Rwanda, Afrika Kusini, Morocco, India na Hispania.
“Najisikia fahari hasa kuwapa nguvu watu wenye ulemavu kutimiza ndoto zao bila kujali hali walizonazo, kama mimi naweza kufanya makubwa hata wao wanaweza,” alisema Rehema na kuongeza;
“Yalikuwa mashindano magumu, lakini nilijipanga na nimeipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa kuchukua tuzo tatu, ushindi huo unaendelea kunipa nguvu ya kuendelea kuamini katika mambo makubwa kupambana bila kuchoka.”
Rehema alisema katika mashindano mbalimbali yatakayofanyika mwaka huu, anatamani kushinda mataji mengi, ili kuendelea kujiweka nafasi nzuri za kiwango ndani na nje ya nchi.
Katika orodha ya Wachezaji tenisi (Women’s Single Ranking) Rehema ni namba moja Tanzania, tano Afrika, moja Afrika Mashariki na Kati, huku kwa duniani akishika nafasi ya 78 kwa mmoja mmoja na kwa ujumla kwa wanawake (doubles ranking ) anashika nafasi ya 62 duniani.