Pemba. Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ADA Tadea, George Bussungu amesema endapo atapata ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi kuiongoza Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025 kipaumbele chake kitakuwa ni ujenzi wa viwanda katika kila wilaya Kisiwani Pemba.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Kangagani Kisiwani Pemba, leo Septemba 18, 2025 Bussungu amesema Serikali yake itaweka mkazo kwenye uchumi wa viwanda akiamini ni moja ya kichocheo kikubwa cha maendeleo katika nchi.
Amesema chama hicho kikipata ridhaa kitajenga viwanda kila wilaya kulingana na uchumi wa eneo na rasilimali iliyopo ili kuhakikisha Pemba inafunguka na inapiga hatua kiuchumi.
“Haiwezekani kisiwa kimebarikiwa zao la mwani na mengine ya aina mbalimbali lakini hakuna kiwanda cha kusarifu mazao, Ada Tadea italiangalia hilo,”amesema.
Amesema kutokana na shughuli kuu za Zanzibar ni kilimo na uvuvi hivyo watajenga maghala ya kuhifadhia samaki ili watu wanaotoka nje ya Zanzibar wawanunue kwa urahisi.
Amefafanua ili kulikamilisha hilo watawawezesha wavuvi kupata vifaa bora vya uvuvi vitakavyowawezesha kufanya shughuli zao katika bahari kuu.

Kwa upande wake mgombea mwenza wa chama hicho, Ali Hassan amesema wananchi watakapokiunga mkono watajenga daraja kubwa katika Kivuko cha Kojani kwa lengo la kuwarahisishia wananchi wa kisiwa hicho kufanya shughuli zao bila bughudha.