Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman ametaja mambo manne ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege, akisema ndiyo ufunguo wa kuifungua Pemba kimaendeleo na kiuchumi.
Mengine ni miundombinu ya bandari, mawasiliano, utawala mwema na mzunguko wa watu wanaoingia na kutoka Pemba.
Othman ameeleza hayo leo Alhamisi Septemba 18,2025 wakati akihutubia wananchi mkoani katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mpitango kisiwani Pemba katika mwendelezo wa kusaka kura za urais.
Amesema mpango wa ACT-Wazalendo kiikishika dola ni kutenga maeneo ili kutoa fursa ya watu kujenga nyumba za kisasa zitakazotumiwa na wageni watakaotembelea kisiwa hicho tofauti na ilivyo sasa.
“Huu ni mpango tulioandaa miaka mitatu iliyopita, tunachokifanya tunakwenda kuukamilisha. Wote tuliowasiliana nao wameukubali na wengine wametaka kuwa mwanzo kuwekeza, watu wakiingia na kutoka na si biashara hii ndio kuifungua Pemba,” amesema Othman.
Amesema lazima bandari ya kisasa ya mkoani na Wete zijengwe ili kuifungua Pemba, hilo litafanyika chini ya Serikali itakayoundwa na ACT Wazalendo.
“Hatutatizama bandari ya watu kusafiri pekee yake, kwa sababu Pemba ilipo ni lango la biashara. Ukiwa na bandari ukaweka mafuta, meli zitakazopita zitakuja kuweka mafuta Pemba hii ni biashara kubwa.”
“Fedha za kuwekeza au wawekezaji wapo isipokuwa na wanataka Serikali yenye uhakika zaidi. Hii ni ahadi yetu, na vijana zingatieni haya ndio yatakayotengeneza ajira, tutawezesha, tutawasomesha ili mfanye kazi katika miradi hii ikiwemo ya uwanja wa ndege,” amesema Othman.
Amesema ukiwa na uwanja wa ndege wa kisasa ni biashara, mizigo na abiria watasafiri kwenda Pemba na kuchochea uchumi ili kukifungua kisiwa hicho.
Kuhusu mawasiliano, Othman amesema atahakikisha anaimarisha huduma za mawasiliano, akisema kuna wataalamu wengi wa Kizanzibari wapo sekta hiyo walioko nje watakaokuja kuifanya kazi hiyo.
“Katika kuboresha huduma hiyo, baadhi ya maeneo ya Pemba na Unguja yatakuwa na huduma ya intaneti ya bure ‘free Wi-fi’ huko ndiko dunia iliko. Kuna kazi siku hizi ili uzifanye lazima uwe na uhakika wa intaneti na mawasiliano.
“Ndio maana wakati tunaandaa ilani yetu, tuliwashirikisha ndugu zetu walioko nje ambao ni wataalamu wa eneo hili. Ukiwa na mawasiliano yaliyoimarika, tutakuwa na uhakika Pemba itafunguka na kuwa kisiwa cha neema,” amesema Othman.
Kuhusu utawala mwema Othman amesema,“ Lazima mjue Zanzibar kuna injini mbili, Unguja na Pemba, hata hivyo Pemba huwa haisemwi sana kama Unguja. Nataka niwaambie Pemba inawezekana kufanyika maendeleo na pakabadilika.
“Kukiwa na utawala mwema, watu wakiwa na amani, mtu akiwa na uhakika wa biashara yake na ardhi bila kufanyiwa vurugu, wawekezaji watakuja kuwekeza Pemba,” amesema Othman.
Othman amesema ufunguo wa Pemba kimaendeleo ni pamoja na wananchi kuwa na uhakika wa kupatiwa haki zao za msingi bila bughudha.
“Naomba Mungu aendelee kuniweka mtakuja kuona raha za watu, siku tutakayochukua Serikali. Kwa sasa siwezi kuipima, lakini najua wengine hawawezi kufurahi endapo Othman akiwa Rais ila mabadiliko yataonekana,” amesema Othman.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa amesema chama hicho hakina wasiwasi ushindi wa Oktoba 29 kwa sababu kamati ya ushindi anaiongoza yeye, akiwataka Wazanzibari kutembea kifua mbele.
“Mambo ya kudhulumiwa tumeyashika tangu 2020, sasa mwaka 2025 tunakwenda kuandika historia mpya. Nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu amani na utulivu, akisimamia kauli basi sisi atatukuta mbele tunamsubiria.
Jana Jumatano Septemba 17,2025 akiwahutubia wananchi wa Kajengwa Jimbo la Makunduchi mkoa wa Kusini Unguja Rais Samia alisema atahakikisha amani na utulivu vinatawala katika msimu wote wa Uchaguzi Mkuu wa 2025.
“Sisi tutamuunga mkono dada yetu (Rais Samia) yale aliyoyasema, lakini si kwa vitimbi vinavyoandaliwa…,” amesema Jussa ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Ushindi ya ACT Wazalendo.