Tanga. “Katika mazingira ya ajali nilikuta tayari watu watatu wameshafariki dunia palepale ambao ni baba, Joshua na binti mmoja na wengine wakiwa ni majeruhi ambaye ni mama, na watoto wengine ambapo wakati tukitafuta njia ya kuwasaidia yule kijana na yeye akafariki dunia na baadaye tukiwa hospitali miili mingine ikaletwa yote nilipambana kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa,”anaanza kusimulia Miraji Ramadhani Mkazi wa Kiwangwa Chalinze mkoani Pwani ambaye ndiye shuhuda na mtu wa kwanza kufika eneo la ajali, na kusaidia kwa hali na mali kuhakikisha miili imehifadhiwa vizuri na vitu vingine ambavyo vilikuwepo ndani ya gari zinakuwa salama.
Hatua ya Ramadhani imezua mjadala kwenye shughuli ya mazishi ya wanafamilia hao ikielezwa kuwa ni kitendo kisicho cha kawaida kufanywa na shuhuda wa tukio la ajali kuwa karibu na majeruhi na kuanza kutafuta njia ya kuwasaidia pamoja na kustiri miili ya marehemu waliofariki. Hii imetokana na kuzoeleka kuwa wanaoshuhudia matukio ya namna hiyo kulaumiwa kwa kuiba mali za waathirika.
Anaeleza kuwa siku ya Jumapili Septemba 14,2025 akiwa eneo la Msata akitoka kupeleka mgonjwa hospitali akapata taarifa kwamba kuna ajali imetokea, hivyo alikimbilia eneo la tukio kwa nia ya kushuhudia na kutoa msaada.
Katika eneo la tukio anasema alikuta tayari Francis ameshafariki dunia na watoto wengine watatu, ila mmoja hali yake ilikuwa ni mbaya pamoja na mama yao Sophia ambaye alikuwa akiomba msaada baada ya kumuona.
“Nilianza kwa kuchukua simu na kuanza kuwatafuta ndugu na jamaa kwa ajili ya kuwapa taarifa. “Mama (Sophia) akaniambia mpigie mtu anaitwa Erick ambaye alisema ni mfanyakazi mwenzake nilimtafuta ila akawa anakata simu ikibidi nimtumie ujumbe,”anaeleza Ramadhani hatua ambazo alichukua awali.

Anasema baada ya kuongea na ndugu na jamaa kuwapa taarifa kuhusu tukio la ajali, tayari watu wengine walishafika kwenye ajali na kuanza kutoa msaada ikiwamo kuwabeba majeruhi kuwapeleka hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi.
Anaeleza kuwa gari la Polisi lilifika na kuanza kutoa msaada kwa kuwapeleka majeruhi Hospitali ya Msata na alihusika kama ndugu kwa kusimamia mambo ya matibabu na kulinda mabegi yao yote.
“Mama aliniomba niwasaidie hawana ndugu na tunahitaji msaada, hivyo nilimjibu nipo tayari kuwapa msaada mpaka mwisho na nilifanya hivyo kuanzia hapo mpaka dakika ya mwisho tunafika hospitali na kupokea miili na nilihusika kama ndugu kwenye taratibu zote za kuhifadhi miili yao,”anasema Ramadhani.
Kutokana msaada ambao Ramadhani ametoa eneo la tukio familia ya Kaggi imeamua kumpa heshima maalumu na wametangaza kwa sasa ni ndugu wa familia hiyo rasmi, na watasaidiana kama familia kwa kile ambacho alifanya.
Akizungumza nyumbani kwa familia hiyo Magaoni jijini Tanga, wakati wa shughuli ya maziko, Joseph Chacha alisema wameamua kutoa heshima hiyo kwa Ramadhani kwani amekuwa msaada kubwa kwa kuwastiri ndugu zao.
Alisema Ramadhani alisimamia kwenye eneo la tukio kuhakikisha usalama unakuwepo kwa kulinda mali zilizopo, lakini pia kuhifadhi miili vizuri hadi pale wananchi wengine walipofika na kutoa msaada zaidi, na hakuonyesha tamaa yoyote ya kutaka mali.
“Kutokana na hili familia imeamua kumpa heshima maalumu na kuanzia sasa atakuwa kwenye familia ya Kaggi, na kuwa mwanafamilia mwenzetu kwa sababu ya msaada alioutoa,”alisema Chacha.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mikanjuni jijini Tanga Jeremia Mboko akiwa kwenye ibada ya mazishi ya miili hiyo mitano, ameunga mkono familia ya Kaggi kutangaza kuwa kuanzia sasa Ramadhani ni mwanafamilia.
Mchungaji Mboko alisema kijana huyo anastahili pongezi kwa sababu ulimwengu wa leo binadamu wanaangalia zaidi mali, na sio utu. Hivyo ameipongeza familia ya marehemu Francis kwa kutambua juhudi za Ramadhani ambaye aliwahi eneo la tukio na kusaidia kulinda mali zilizokuwepo hapo, lakini kustiri vizuri miili.
Alisema ulimwengu wa sasa binadamu wengi wamekosa moyo wa kusaidia hasa kwenye matukio, lakini kijana huyo ameweza hilo kwa kufanikiwa kusaidia waathirika.
“Katika kitu ambacho kimenishangaza kwa huyu kijana ni kutunza mali zote ambazo zilikuwa eneo la tukio, ni jambo la ajabu hakuwa na tamaa bali moyo wake ulijaa huruma kwa kuangalia miili na mali husika, hili sio jambo rahisi ni la kupongezwa sana kwa jinsi matukio yanavyotokea,”alisema Mchungaji Mboko.Wanafamilia hao walipoteza maisha kwenye ajali ya gari iliyotokea Septemba 14, 2025 katika eneo la Msata, Bagamoyo mkoani Pwani wakitokea Tanga kwenye msiba wa mama wa Francis.
Waliopoteza maisha ni wafanyakazi wawili wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Francis Elineema Kaggi (Ofisa Tehama) na Elineema Hamis Kaggi (mhasibu), watoto watatu wa Francis na shemeji yake.