TRA Geita yavuka lengo la makusanyo, ikiwageukia wafanyabiashara wasio rasmi

Geita/Dodoma. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Geita imekusanya Sh69.2 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/25, sawa na asilimia 113 ya lengo la Sh61.7 bilioni ililopaswa kukusanya.

Sambamba na mafanikio hayo, mamlaka hiyo imetangaza mkakati mpya wa kuwashirikisha wafanyabiashara wadogo na wale wa sekta isiyo rasmi kupitia dawati maalumu la uwezeshaji biashara, ili kuwawezesha kurasimisha shughuli zao na kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Sekta isiyo rasmi inatajwa kuwa ndiyo ajira kuu kwa Watanzania wengi, lakini wafanyabiashara wake hukabiliwa na changamoto za kutotambulika kisheria, kushindwa kupata huduma za kifedha na kuendesha biashara bila mwongozo wa kitaasisi.

Akizungumza kwenye hafla ya kuzindua dawati hilo, Meneja wa TRA Mkoa wa Geita, Elirehema Kimambo amesema litakuwa na jukumu la kuwatambua, kuwasikiliza na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, ili wapate nafasi ya kukua na kuchangia kikamilifu katika pato la Taifa.

“Dawati litawaunganisha wafanyabiashara na taasisi za Serikali na kifedha ili kurahisisha urasimishaji wa biashara na kuwawezesha kupata mikopo ya mitaji,” amesema Kimambo.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa dawati maalumu la uwezeshaji biashara, amesema Serikali imelenga kuwaweka karibu wafanyabiashara wa ngazi zote kwa kuwapatia elimu na msaada utakaowawezesha kufanya biashara kwa tija.

“Lengo la kuanzishwa kwa dawati hili ni kuwatambua, kuwasikiliza na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa. Pia litakuwa jukwaa la kusikiliza changamoto zao na kwa pamoja kutafuta suluhisho,” amesema Gombati.

Ameongeza kuwa dawati hilo litawaunganisha wafanyabiashara na taasisi za Serikali ili kurasimisha biashara zao na kuwawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa lengo la kukuza mitaji na biashara zao.

Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria hafla hiyo wameeleza matumaini yao kuwa dawati hilo litawapa uelewa kuhusu kodi na namna bora ya kufanya biashara.

Wakati huohuo, Serikali imezindua kamati za usimamizi na utekelezaji wa mkakati wa muda wa kati wa mapato kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2025/26 hadi 2027/28, ukiwa na lengo la kuimarisha mfumo wa ukusanyaji mapato, kuongeza makusanyo na kukuza utamaduni wa ulipaji kodi kwa hiari.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba ameyasema hayo alipokuwa akizindua mpango huo jijini Dodoma.

Dk Mwamba amesema utekelezaji wa mkakati huo utaboresha usimamizi wa mapato ya Serikali na kuweka msingi wa bajeti endelevu itakayowezesha utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi kupitia mapato ya ndani.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa mkakati huo utaongeza uwiano wa mapato ya Serikali kwa Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 0.83 katika mwaka wa fedha 2025/26, asilimia 1.27 mwaka 2026/27 na asilimia 1.3 mwaka 2027/28.

“Mkakati huu umezingatia matarajio ya mwenendo wa uchumi wa Taifa, umechambua vihatarishi vinavyoweza kujitokeza na kuweka mbinu za kuviepuka ili kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wake,” amesema Dk Mwamba.

Katibu tawala Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati akizungumza wakati wa uzinduzi wa dawati maalum la uwezeshaji biashara mkoa wa Geita.

Aidha, amesema mkakati huo umeainisha maboresho ya mikakati na hatua mbalimbali ambazo Serikali imekuwa ikitekeleza ili kuongeza mapato kutoka vyanzo vya ndani. Amesema kamati tendaji inaundwa na wataalamu wenye ujuzi na uzoefu katika masuala ya uchumi, kodi na fedha kutoka serikalini na sekta binafsi, hivyo ana imani watatekeleza vyema majukumu yao.