Dar es Salaam. Madai ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kushambuliwa wanachama wake na Polisi wakiwa Mahakama Kuu walipokwenda kuhudhuria kesi ya uhaini ya Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, yameisukuma Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kuanzisha uchunguzi.
Chadema, katika taarifa yake ya Septemba 15, 2025, imelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kumshambulia na kumdhalilisha Wakili Deogratius Mahinyila, mmoja wa mawakili wa Lissu, baadhi ya viongozi na wanachama wengine.
Siku hiyo hiyo Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam walitoa taarifa wakieleza kuwadhibiti wafuasi wa chama hicho waliosababisha fujo Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Jana Jumatano, Septemba 17, 2025, akizungumza na waandishi jijini Dodoma, Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, amesema kwa kuwa watu wa tume hiyo hawakuwepo eneo la tukio kufahamu kilichotokea, hivyo wanafanya uchunguzi.
“Malalamiko ninayoyaeleza yanaliangalia Jeshi la Polisi kwa kuwa watu wetu hawakuwepo eneo la tukio, tunachoweza kusisitiza ni watu wafuate sheria na kanuni wanapotekeleza majukumu yao. Hili halituzuii kufanya uchunguzi kuangalia nini kilijiri pale.
“Yapo maelezo yanayotolewa na Chadema na Jeshi la Polisi. Sasa ili uwe na uhakika nini kilijiri hadi watu wakapigwa ni lazima watu wetu waende eneo la tukio, kuzungumza na watu wajue nini kilitokea,” ameeleza jaji huyo.
Jaji Mwaimu amesema tume hiyo imeundwa kwa mujibu wa Katiba na sheria, hakipaswi kutekeleza majukumu yake kwa mihemko bali kulingana na sheria na taratibu zilizopo.
Amesema wanayaona matukio mengi, lakini ili kuhakikisha kile wanachokisema ni sahihi, lazima waende kufanya uchunguzi.
“Matukio yanayojitokeza mara nyingi tunafanyia uchunguzi na kutoa mapendekezo kwa taasisi zinazohusika, na tumefanya hivyo mara nyingi,” amesema.
Amesema kwa matukio mengine ambayo waliona taarifa za awali, walitoa matamko ya kulaani na uchunguzi unaendelea.
Jaji Mwaimu amesema katika matukio hayo, uchunguzi hutegemea ukubwa wa tukio na aina ya watu wanaoweza kuhojiwa kutoa ushahidi.
Kuhusu muda sahihi wa uchunguzi, jaji huyo amesema hauwezi kuchukua wiki mbili au tatu, bali utategemea namna wanavyoweza kupata taarifa kwa usahihi.
“Tunapofanya uchunguzi, upo uchunguzi unaweza kuchukua muda mfupi, muda wa kati hadi mwingine miezi mitatu ndipo uchunguzi unaweza kukamilika,” amesema.
Kulingana na taarifa ya Chadema, Wakili Mahinyila ameshambuliwa, kujeruhiwa vibaya na kudhalilishwa na askari wa Jeshi la Polisi katika eneo la Mahakama Kuu alipokuwa akihudhuria kesi ya uhaini inayomkabili Lissu.
Chadema imeeleza kuwa, polisi walimshambulia na kisha kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi, ambako alishikiliwa na baadaye kuachiliwa.
“Ifahamike kuwa, Mahakama ni eneo la haki na siyo himaya na uwanja wa Jeshi la Polisi kunyanyasa na kuwafanyia ukatili Watanzania. Chadema inalitaka Jeshi la Polisi liheshimu eneo la Mahakama na Watanzania wanaofika eneo hili kufuatilia kesi mbalimbali,” imeeleza taarifa hiyo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ameeleza kuwa asubuhi ya Septemba 15, 2025, baadhi ya wafuasi wa Chadema waliokuwa nje ya Mahakama walianzisha fujo na kujaribu kuwashambulia askari, ambao walijihami na kutuliza fujo hizo haraka.
Kulingana na taarifa aliyoitoa kwa umma kutokana na tukio hilo, Muliro ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea baada ya ukumbi uliokuwa unatumiwa kwenye kesi ya Lissu kujaa, na hivyo baadhi ya wafuasi hao waliokuwa nje ya Mahakama kuanzisha fujo.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kuwa kitendo chochote cha kuwachokoza askari kitashughulikiwa haraka na kuyarejesha mazingira ya usalama kwenye eneo husika haraka kwa kadiri inavyowezekana,” imeeleza taarifa hiyo ya polisi.