Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya China, maarufu kama Canton Fair, yamepata umaarufu mkubwa duniani.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957, upangaji, uratibu na usimamizi wake vimeyafanya kuwa kivutio kikubwa kwa wafanyabiashara, maonesho hayo kwa sasa ni kitovu cha biashara kwa maelfu ya wafanyabiashara kutoka nchi 150 duniani wanaofika kununua na kuuza bidhaa.
Katika sifa kubwa za Canton Fair ni ukubwa wake na upangaji mzuri wa majengo, miundombinu ya wauzaji na kumbi za maonesho, kwa mujibu wa taarifa za tovuti rasmi ya maonesho hayo CFTC, eneo la maonesho lina ukubwa unaofika mita za mraba milioni 1.6, Ukubwa huo unajumuisha sehemu ya ndani ya maonesho katika kumbi na sehemu za nje.
Vuta taswira kuwa inaweza kuwa takribani mara nne ya eneo lote la Kariakoo Dar es Salaam maduka na biashara zake.
Hali kadhalika, ubora wake unaongezwa na namna vile ilivyopangwa, kwa mfano, eneo lote la maonesho limegawiwa katika maeneo matatu makuu (Zoni A, B na C), katika maeneo yote matatu kubwa kumbi za maonesho 45, lenye idadi ya vizimba 73,000 na uwezo wa kupokea wafanyabiashara na waoneshaji takribani 30,000 kwa wakati mmoja.
Kuweka maeneo mahsusi kwa ajili ya sekta tofauti kunasaidia katika kupanga ratiba, kurahisisha utafutaji wa bidhaa kwa wageni wanaofika kufanya manunuzi, na kuwasaidia wageni kuelewa kwa urahisi uelekeo, na pia kuwapatia nafasi makampuni ya sekta zinazofanana kukaa pamoja.
Mathalan, mtu anajua kuwa Zoni A ndiyo lango kuu lenye huduma za kutolea vitambulisho na malipo ya usalama, na wauzaji vifaa vya kielektroniki, mitambo na zana.
Zoni B, ambayo iko katikati, inahusisha wauzaji wa vifaa vya jikoni, kauli, bidhaa za nyumbani, pamoja na huduma za benki, migahawa na kituo cha waandishi wa habari. Hivyo mnunuzi hapotezi muda wala kutaabika kutafuta bidhaa.
Vilevile, upangaji huu unarahisisha huduma za usafirishaji na kuhudumia mahitaji ya wageni wanaofika, ni rahisi kujua kwa sasa msongamano mkubwa wa wanunuzi uko wapi, inasaidia jitihada za kuratibu usafiri zielekezwe eneo gani la maonesho kusaidia uchukuzi wa watu wanaohitaji kwenda maeneo mengine.
Lakini pia ubunifu wa matumizi ya teknolojia inasaidia sana upangaji wa maonesho haya. Kwa mfano uwepo wa skrini kubwa katika kumbi za maonesho inawezesha washiriki kufuatilia shughuli zinazoendelea muda wote. Kama filamu isiyoisha.
Aidha, waandaaji wametengeneza programu mbili, moja kwa wanunuzi na nyingine kwa wasambazaji, zinazorahisisha utafutaji wa bidhaa, mapendekezo, na huduma kama skani ya beji ya kidijitali, na mengine hutolewa. Jambo hili linasaidia katika utafutaji wa bidhaa kwa kunganisha wanunuzi na wauzaji kwa njia rahisi.
Lakini pia uwepo wa huduma nyengine muhimu kwa wageni huongeza mvuto wa maonesho hayo. Benki, migahawa, kumbi za kupumzikia na miundombinu ya usafiri treni za umeme, mabasi, husaidia kuchukua watembezi kutoka kumbi za maonesho, jambo linalowarahisishia wageni kufika na kuondoka kwa haraka.
Kuna mambo kadhaa ambayo mamlaka zetu zinapaswa kuangalia ili kuwekeza katika kuboresha maonesho ya kibiashara na kuendana na mahitaji ya wafanyabiashara na ongezeko la wageni;
Kwanza, ni muhimu kuongeza ukubwa wa eneo la maonesho ili kuruhusu ujenzi wa miundombinu zaidi, ikiwamo njia bora za usafiri. Hii itawasaidia wageni na wanunuzi ambao hawawezi kutembea umbali mrefu, na pia kurahisisha matembezi na biashara kufanyika kwa uharaka zaidi.
Pili, kugawa eneo la maonesho kwa sekta maalumu ni mkakati bora. Utaratibu huu utarahisisha utendaji, kuimarisha mwongozo wa wageni, na kurahisisha utambulisho wa bidhaa. Ramani au viashiria vya uelekeo vinaweza kuwekwa kuwasaidia wageni kujua wapi wanapata bidhaa fulani.
Tatu, kuanzisha jukwaa la mtandaoni linalofanya kazi mwaka mzima kutawaunganisha waoneshaji na wanunuzi kabla, wakati na baada ya maonesho. Jukwaa hili litakuza biashara zisizo na mipaka, kuongeza mauzo ya ndani, na kutoa huduma muhimu kama usajili, uhamasishaji, pamoja na urahisi wa kutafuta wasambazaji na wateja. Na mengineyo.
Nne, huduma kiungo kama benki, migahawa, vituo vya habari na maeneo ya kupumzika zinapaswa kupewa kipaumbele. Kila mwaka idadi ya wageni huongezeka, hivyo huduma hizi ni muhimu ili kuongeza mvuto na ufanisi wa maonesho.
Tano, mamlaka ya maonesho inaweza kukuza ushiriki wa kimataifa kupitia mikakati ya uhamasishaji, kushirikiana na balozi za kigeni, na kuandaa maonesho ya sekta maalum. Hatua hii itafungua fursa mpya za kibiashara na ushiriki wa wadau kutoka nje ya nchi.
Mwisho, ni muhimu pia kuwekeza katika mafunzo ya stadi za biashara, ujasiriamali na ubunifu kwa wajasiriamali wadogo. Mafunzo haya yatawasaidia kushiriki kikamilifu na kushindana katika soko la kimataifa.