Katika maisha ya mijini, “kodi ya meza” imekuwa utaratibu usioandikwa wa kupanga matumizi ya fedha za nyumbani. Ni utaratibu wa “kuweka juu ya meza” kiasi fulani kila siku kwa ajli ya matumizi ya siku kama vile chakula, nishati ya kupikia, maji, na hata nauli za watoto kwenda shule.
Kwa haraka haraka, mtindo huu unaonekana mwepesi na unaoleta utulivu wa maisha kwani siku inaisha salama, “kodi ya meza” ikiwa imelipwa. Lakini urahisi huo mara nyingi huficha gharama halisi za maisha.
Manthalani kununua rejareja kwa bei ya juu, kuchoka kiakili kwa kupanga kila siku, na kuishi kwenye mzunguko wa “nitapata wapi kodi ya meza ya kesho.” Wakati mwingine mtu analazimika kufanya jambo ambalo hakulipangilia kitu “kodi ya meza” ipatikane.
Changamoto kubwa ni dhana kwamba kiwango cha kila siku ndicho kipimo cha uhalisia wa mahitaji ya familia.
Watu wengi hasa kina mama na kinababa wanaulizana “kodi ya meza ni ngapi?” badala ya kuuliza “familia ina ukubwa gani, malengo ni yapi, na lini bili kubwa hulipwa?”
Matokeo yake ni madeni madogo madogo yanayojikusanya, kukosa uwezo wa kukabiliana na dharura, na kuleta mazoea ya fedha bila kuwa na mpango wa mwezi. Mtu anapoachiwa bahasha ya siku, kazi yake hubaki “kutosha leo,” si “kujenga kesho.”
Pia inaficha matumizi mengine kama kodi, ada, manunuzi ya nguo, na pia manunuzi ya vitu vya muda mrefu. Inakufanya kuwa na fikra nyingi ambazo hazipo kwenye meza moja, na inaweza ikaondoa kabisa uwezekano wa kuweka akiba. Mpango huu pia umesababisha migongano kwenye familia nyingi.
Hata hivyo, “kodi ya meza” inajenga nidhamu, inazuia ubadhirifu wa chakula na matumizi yasiyo kwenye mpango inapotokea unaponunua kwa wingi bila mpango. Inajenga kujituma, kwani kwa kutegemea kiasi fulani kila siku inakufanya kiasi hicho kipatikane. Pamoja na faida hizi, inafanya watu kubaki kwenye mtego wa rejareja. Ni wazi kuwa kuna umuhimu wa kuunganisha urahisi wa kila siku na uimara wa mipango ya mwezi.
Hatua ya kwanza ni kubadili kipimo cha muda. Badala ya kufikiri kwa “siku,” fikiria kwa “mwezi.” Andika orodha ya bili zisizokwepeka (kodi, ada za shule, usafiri, bima, deni), kisha gawanya kipato chote kwa makundi: mahitaji ya msingi, matumizi yasio ya msingi, na akiba/madeni.
Kanuni rahisi ya kuanzia ni 50–30–20, ukirekebisha kulingana na kipato chako. Jenga “akiba ya dharura” ya angalau miezi 1–3 ya matumizi ya msingi; huanza kwa wiki, kisha mwezi, hadi ifike lengo. Siri ni kanuni ya “jitolee kwanza”: mara tu kipato kinapoingia, hamisha asilimia ya akiba kabla hujaanza matumizi ya kila siku.
Upande wa ununuzi, changanya busara ya jumla na uhalisia wa kuhifadhi. Nunua kwa jumla bidhaa zisizoharibika haraka (mchele, unga, maharagwe, mafuta, sabuni), na uache rejareja kwa vinavyohitaji ubichi. Unda mpango wa vyakula kwa wiki, andika orodha, na linganisha bei sokoni, dukani, na mtandaoni.
Hifadhi kwa weledi: tumia jokofu/friza, tenga vyakula kwenye vyombo visivyopitisha hewa, na fuata kanuni za uhifadhi wa vyakula ili kuzuia upotevu. Kumbuka pia gharama ya muda: safari tatu dukani kwa wiki ni pesa iliyojificha.
Fanya haya ili kujiondoa na muzunguko wa kila siku: 1) andika bajeti ya mwezi na tarehe za bili, 2) fungua akaunti ya akiba na uweke angalau asilimia 10 hadi 20 ya unachokipata, 3) nunua kwa jumla vyakula visivyoharibika na uvihifadhi ipasavyo, 4) weka siku mbili ya “bila matumizi” kila wiki.
Ukifanya hivi mfululizo kwa miezi mitatu, utaanza kujinasua taratibu kutoka kwenye mduara wa “kodi ya meza” kuelekea uhuru wa kifedha wenye mwelekeo wa kesho.