Uzembe barabarani ajali zaua 25 ndani ya wiki

Dodoma. Janga la ajali limezidi kuwa tishio nchini baada ya watu 25 kupoteza maisha katika matukio tofauti ndani ya wiki moja, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa baadhi yao wakiwa mahututi.

Ajali hizo zilitokea kwa nyakati tofauti katika mikoa tofauti, zikiwemo Pwani ambako watu watano wa familia moja walipoteza maisha juzi, Mwanza (watano), Mara (sita), na Dodoma (tisa).

Ajali mpya katika hizo imetolea alfajiri ya leo Septemba 18, 2025 na kuondoa na maisha ya watu tisa, akiwemo dereva wa basi la Kampuni ya Abuu Trans, huku wengine 16 wakijeruhiwa.

Basi linalofanya safari zake kati ya Dodoma na Kondoa lilipata ajali likitokea Kondoa kwenda mjini Dodoma.

Chanzo cha ajali hiyo kinaelezwa ni dereva lori hilo aona ya Fuso kutaka kulipita basi bila kuchukua tahadhari na kusababisha kugongana uso kwa uso katika eneo la Kambi ya Nyasa wilayani Chemba.

Kufuatia ajali hiyo watu watano wamefariki dunia papo hapo na wengine wanne walifariki dunia wakati wanapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kupatiwa matibabu.

Miongoni mwa majeruhi ni mtoto anayekadiriwa kuwa na umri chini ya mwaka mmoja, ambaye wazazi wake hadi tunaandika taarifa hizo walikuwa hawajajulikana.

Mmoja wa majeruhi katika ajali hiyo, Sada Amiri ambaye alikuwa na ndugu zake wanne kwenye basi hilo, amesema eneo la ajali hapatamaniki na hatamani kupita.

“Kwenye basi lile kulikuwa na watoto wangu wawili, Omar Athuman (8) na Elfan Athuman (11), mama yangu Fatuma Juma na mdogo wangu Swed Amiri, wote wako wodini na mpaka sasa sijui hali zao, ila huyu mdogo tumemwacha nyumbani kavunjika jino, hataki kuja hospitali tena anaweweseka,” amesema Sada.

Akizungumzia bado hilo, amesema: “Kule kijiji linatoka usiku karibu saa 9:30 au 10:00 alfajiri, lakini hatujashuhudia ajali mbaya kama hii, mimi naomba Serikali inisaidie matibabu ya ndugu zangu kwani sina wa kumtegemea, nami ni mjane,” amesema.

Akizungumza kwa tabu kwenye wodi namba moja mmoja majeruhi, Abdulazizi Ramadhan amesema wakati ajali inatokea alisikia kishindo kikubwa na akaona vumbi, lakini hakuona kitu hadi mchana alipoambiwa yupo hospitali.

“Abdulazizi (14) ambaye amesema hana ndugu Dodoma na alikuwa anaenda Musoma, anabainisha kuwa aliposikia kishindo ni kama alihisi watu wanapiga kelele, lakini kwa kuwa basi lilikuwa limejaza na wengine kusimama, hakujua chochote ingawa kwa maelezo yake dereva wao hakuwa katika mwendo mkali.

Akizungumza kuhusu ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera amesema chanzo cha ajali hiyo iliyotokea majira ya 12:40 alfajiri ni uzembe wa dereva wa lori aliyehama upande wake na kusababisha magari hayo kugongana uso kwa uso.

Hyera amesema basi lililogongana na lori lilikuwa likitokea Kondoa kwenda Dodoma na lori hilo lilikuwa likitokea mkoani Dodoma kwenda Kondoa.

“Dereva wa lori alihama upande wake wa kushoto kwenda upande wa kulia na kugongana uso kwa uso na basi, katika ajali hiyo mabati ya upande wa kulia ya basi na upande wa kulia wa lori yamefumuka kwa kiwango kikubwa kuonyesha kuwa madhara yalikuwa makubwa,” amesema.

Hyera amesema dereva wa lori alikuwa katika mwendo mkali na ndio maana madhara yalikuwa makubwa.

Amewataja baadhi ya waliopoteza maisha kuwa ni wanafunzi wanne, Carolyne Joachim (13), Rukia Ally (14) Bashir Hashim (13) na Nasra Mohamed (18). Wengine walikuwa hawajatambuliwa

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa wito kwa madereva kupumzika pale wanaposhindwa kuendelea na safari kutokana na uchovu na usingizi, kwani ajali hiyo imetokea eneo ambalo barabara imenyooka na kila mmoja anamwona mwenzake.

Senyamule amesema si vema na haki kuendesha chombo cha moto wakati akili ikiwa imechoka au mtu anasinzia, kwani madhara yake ndiyo hayo ya kupoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

Ajali hii ni mwendelezo wa mfululizo wa ajali baada ya ajali mbili tofauti za barabarani zilizotokea Jumatatu katika mikoa ya Pwani na Mwanza kusababisha vifo vya watu 10 wakiwemo masista wanne na dereva wao.

Masista hao wanne wa Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, walifariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori jijini Mwanza.

Waliopoteza maisha ni Mama Mkuu wa shirika hilo, Mtawa Nelina Semeoni (60), raia wa Italia; msaidizi wake Lilian Kapongo (55), mkazi wa Tabora; Damaris Matheka (51), Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bukumbi; Stellamaris Kamene Muthin (48), raia wa Kenya na dereva wao Boniphace Msonola.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa alisema, ajali hiyo ilitokea Septemba 15, 2025 saa 1:50 usiku katika Kijiji cha Bukumbi, Kata ya Idetemya, Wilaya ya Misungwi, Barabara ya Usagara-Kigongo Feri.

Watawa hao walikuwa wakielekea Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakitokea Jumuiya ya Bukumbi.

Kamanda Mutafungwa alieleza kuwa gari ndogo aina ya Toyota Land Cruiser, mali ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Bukumbi lilihama njia, hivyo kutokea ajali hiyo.

Ajali nyingine katika kipindi hiki imetokea wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani ambapo watu watano wa familia moja walifariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na gari lingine.

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni wafanyakazi wawili wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Francis Elineema Kaggi na Elineema Hamis Kaggi wakiwamo watoto watatu wa Francis na shemeji yake.

Mke wa Kaggi alinusurika katika ajali hiyo ingawa alipata majeraha na kupelekwa Hospitali katika ajali ambayo ilitokea Septemba 14, 2025 katika eneo la Msata, Bagamoyo walipokuwa wakitoka Tanga kwa maziko ya mama mzazi wa Francis.

Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Buganjo wilayani Rorya wakati gari aina ya Toyota Succeed likiwa limebeba watu saba lilipokuwa linatoka mjini Tarime kuelekea Kijiji cha Busurwa wilayani Rorya, liligonga kwa nyuma gari aina ya Fuso liliokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara baada ya kuharibika.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Mark Njera alielezea ajali hiyo kwamba ilitokea Septemba 11, 2025 saa 11 alfajiri na kusabisha vifo vya watu sita.

“Gari aina ya Succeed iliyokuwa inatoka Tarime kuelekea Rorya iligonga kwa nyuma gari aina ya Fuso lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara baada ya kuharibika,” alisema.

Kwa ujumla katika ajali zote hizo, uzembe wa madereva umetajwa kama sababu na kupelekea vifo hivyo.

Hali hii inaunaga na ripoti za polisi zilizochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuwa asilimia 44.1 ya ajali zote zilizotokea mwaka 2024, zilichangiwa na uzembe.

Ingawa baada ya ripoti hiyo kuchapishwa, madereva walisema hawapaswi kulaumiwa moja kwa moja, kwani hadi ajali inapotokea huwa kuna sehemu tatu, ikiwamo upande wa dereva mwenyewe na chombo husika.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya vifo vya ajali mwaka 2024 iliongezeka hadi kufikia watu 1,715 kutoka 1,647 waliokuwapo mwaka uliotangulia.

Ongezeko hilo, lililotokana na ajali ambazo pia ziliongezeka kubwa zikifikia 1,735 na matukio madogo 3,104,501, ikilinganishwa na matukio makubwa 1,733 na madogo 3,170,073 ya mwaka 2023.