Dar es Salaam. Wakati dunia ikijiandaa kuadhimisha siku ya amani Septemba 21, 2025, nchini Tanzania vijana wameeleza nafasi yao katika kudumisha amani, huku mambo manne yakijadiliwa katika kongamano la maadhimisho hayo.
Septemba 21 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya amani, hapa nchini maadhimisho hayo yameanza leo Septemba 18, 2025 kwa vijana kutoka maeneo mbalimbali kushiriki kongamano la pili la vijana, amani na salama.
Kongamano hilo litafanyika kwa siku tatu mfululizo, likilenga kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa vijana katika ajenda ya amani na usalama, likiwa na kauli mbio isemayo: Vijana na amani, chukua hatua sasa kudumisha utamaduni wa amani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la The African Leaderships Initiative for Impact, Joseph Malekela amesema mambo manne yatajadiliwa kwenye kongamano hilo ikiwamo ushiriki wa vijana katika uongozi na mchakato wa maamuzi.
Pia watajadili suala la vijana na amani katika zama za kidijitali, uwezeshaji wa vijana kiuchumi kama mpango wa kujiepusha kujihusisha na vitendo vya uhalifu na jitihada za vijana kuchukua hatua za mabadiliko ya tabianchi.

Katika kongamano hilo linaloshirikisha vijana kutoka taasisi, vyuo, asasi za kidini, balozi za nchi mbalimbali nchini sanjari na raia wa kawaida, linaangazia ushiriki wa vijana katika maamuzi, kuwalinda na kuwajengea uwezo kujihusisha na masuala ya kiuchumi.
“Vijana ndio idadi kubwa ya wananchi waliopo nchini kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, wanapojengewa uwezo katika masuala ya amani na usalama, tunajenga Taifa imara,” amesema Malekela akibainisha kwamba katika kilele cha kongamano hilo, kutakuwa na mbio fupi zitakazoanzia fukwe ya Coco hadi ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere ili kuhamasisha amani na kuzidi kuwa nchi yenye umoja na ushirikiano.
Mkurugenzi wa huduma za ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Josephine Matiro amesema kama wizara moja ya majukumu yake ni kuhakikisha vijana wanawezeshwa na kuwa mstari wa mbele kulinda amani na usalama.
“Suala la kulinda amani na usalama ni ya kila mtu, nitoe wito kwa vijana kuhakikisha hilo ni kipaumbele chao katika majukumu yao ya kila siku,” amesema.
Naye mjumbe maalumu wa Umoja wa Afika kuhusu wanawake, amani na usalama, balozi Liberata Mulamula amesema hali ya amani ulimwenguni hivi sasa inatetereka na kwenye migogoro mingi kundi la vijana limekuwa likihusishwa kwa namna moja au nyingine, akishauri kama nchi kuwe na mkakati wa kitaifa ambao utawahusisha pia vijana.
“Huwezi kusema utakuwa na maendeleo, amani na usalama bila kuwahusisha vijana.
“Pia watu wanaweza kusema mbona Tanzania ina amani hii mikakati ya nini, amani si kwamba hakuna vita, vitu ni vingi vinavyoondoa amani, hususan vijana wakijiingiza kwenye vitu ambavyo vitahatarisha maisha yao na Taifa,” amesema.
Wakizungumzia nafasi yao katika masuala ya amani na usalama, baadhi ya vijana wamesema wakiwa na
shughuli za kiuchumi sio rahisi kujiingiza kwenye matukio yatakayohatarisha amani na usalama wao.
“Kongamano hili limeonyesha mwanga kwa vijana katika mada ya kutunyanyua kiuchumi, kijana akiwa na shughuli za kumuingizia ni nyenzo ya kutunza amani, kwani sio rahisi kushawishika akafanye matukio yasiyo ya amani na usalama,” amesema.

Mwanafunzi wa Chuo cha Dk Salim Ahmed Salim, Marian Choga amesema katika kongamano hilo amejifunza jambo kubwa la vijana kuacha kutumika, badala yake akitoa wito kuzifanyia kazi fursa zinazopatikana huku wakiendelea kutunza amani.
Wakati mwakilishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Zanzibar kutoka Idara ya Vijana, Shafii Kasim amesema vijana hawapaswi kurubuniwa akishauri wawe mstari wa mbele kutoa elimu ya amani na usalama kwa wengine ili kuzidi kuwa na Taifa bora.