Mbeya. Licha ya zaidi ya asilimia 64 ya Watanzania kutegemea kilimo kwa maisha yao, sekta hiyo bado inakua kwa kusuasua kwa kiwango cha asilimia 4.5, hali inayochangiwa na mabadiliko ya tabianchi na utegemezi wa msimu wa mvua pekee.
Hatua hiyo imesababisha kudhoofika kwa mnyororo wa thamani ya mazao, kutokana na ukosefu wa kilimo cha umwagiliaji na upungufu wa nguvu kazi.
Kauli hiyo imetolewa leo, Alhamisi Septemba 18, 2025, na Profesa Humphrey Moshi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati akiwasilisha mada kuhusu uchumi jumuishi kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Kongamano hilo limeandaliwa na Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Taaluma za Umajumui wa Afrika, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta Binafsi na Umma (PPPC), chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Washiriki wa Kongamano la kujadili mwenendo wa uchumi jumuishi kuelekea Dira 2050 ya Maendeleo ya Taifa. Picha na Hawa Mathias
Profesa Moshi amesema kuwa licha ya asilimia kubwa ya Watanzania kutegemea kilimo kama chanzo kikuu cha maisha, sekta hiyo inaendelea kukua kwa kasi ndogo ya kati ya asilimia nne hadi 4.5, ikilinganishwa na ukuaji wa uchumi wa jumla unaofikia asilimia sita.
Amebainisha kuwa sababu kuu za ukuaji huo wa kusuasua ni pamoja na kilimo chenye tija ndogo kinachotegemea msimu wa mvua pekee, hali inayosababisha upungufu wa malighafi kwa sekta ya viwanda na kuathiri mnyororo wa thamani katika uchumi.
Profesa Moshi amesema hali hiyo imekuwa ikidhoofisha mnyororo wa uzalishaji na kuchangia upungufu wa ajira kwa vijana, kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.
Katika hatua nyingine, Profesa Moshi ameshauri kuwa ili kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, Serikali inapaswa kuwa na mkakati thabiti wa utekelezaji unaojumuisha bajeti ya kutosha na mipango ya maendeleo ya kila miaka mitano.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya usimamizi, ufuatiliaji na tathmini, ili kubaini changamoto zinazojitokeza na kuzifanyia kazi kwa wakati, sambamba na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika mchakato huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila amesema Serikali imeweka mikakati ya kufikia hekta milioni tano za kilimo cha umwagiliaji ifikapo mwaka 2050, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa uchumi jumuishi na wa kisasa.
“Kuna ongezeko la maeneo ya kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 540,000 mpaka 928 ,000, lakini kufikia Dira 2050 matarajio ni kuzifikia hekta milioni tano jambo ambalo litaleta tija katika sekta ya kilimo,” amesema.
Kafulila amesema ni wakati sasa sekta binafsi zikashirikishwa ili kuweke msukumo kufikia malengo ya Dira ya 2050 ya uchumi jumuishi wa Maendeleo ya Taifa la Tanzania.
Awali, Mwenyekiti wa Kongamano la Kigoda hicho, Profesa Alexander Makulilo amesema lengo la kongamano hilo ni kukutanisha wadau mbalimbali kujadiliana kwa masilahi mapana ya Taifa.