Ada Tadea yaahidi ajira, kugawa mitungi ya gesi bure kwa wananchi

Tanga. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Ada Tadea, Georges Busungu, amesema wananchi wakimchagua atasaidia kupatikana kwa ajira, pamoja na kuboresha mazingira ya bandari na miundombinu kama barabara.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika leo Ijumaa, Septemba 19, 2025, katika viwanja vya Tangamano, mkoani Tanga, amesema kwa mkoa huo endapo atapewa ridhaa ataboresha zaidi Bandari ya Tanga ili ato ajira zaidi.

Ameeleza kuwa, kwa kuanzia, atajenga reli ya kutoka Tanga kwenda Kilimanjaro mpaka Arusha, ambayo itaboresha usafirishaji wa abiria na mizigo, hali itakayosaidia wananchi kupata ajira kwa shughuli ambazo zitaanzishwa.

Amesema Tanga ilikuwa ikiongoza Tanzania kwa kuwa na viwanda vingi, ila kwa sasa vingi havifanyi kazi, hivyo akipewa ridhaa na wananchi, wataanza na uboreshaji wa barabara ambazo zitatumika zaidi kwa usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa mkoani humo.

Ameeleza kuwa Serikali yake itakwenda kuboresha maisha ya wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kujenga masoko ya kisasa, ambayo yatawasaidia kufanya biashara bila changamoto, tofauti na hali ya baadhi ya masoko yaliyopo sasa.

“Serikali ya Ada Tadea itahakikisha kwamba vibanda vya kisasa vinajengwa kwa wafanyabiashara wa Jiji la Tanga ili kuboresha biashara zao kwa kuweka mazingira yao safi. Kila Mtanzania anatakiwa kuwa na mazingira mazuri ya nyumbani na kwenye biashara. Mkinichagua kuwa Rais, niwaahidi haya,” amesema Busungu.

Mgombea mwenza, Ali Makame Issa, amezungumzia kuhusu uwepo wa Muungano na kueleza kuwa endapo watapewa ridhaa na wananchi watalinda Muungano, kwani umeasisiwa kwa maana ya kuwa kitu kimoja.

Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakibeza uwepo wa Muungano, jambo ambalo ni kosa, kwani Serikali ilikuwa na maana ya kuunganisha pande hizo mbili na zipo faida zinazoonekana kutokana na uwepo wake.

Amewataka wananchi kupuuzia wale wote ambao wanaleta chokochoko za kutaka Muungano uvunjwe, kwani hawafahamu historia yake na wanafanya hivyo kwa maslahi yao binafsi.

Pia, amezungumzia kuhusu utunzaji wa mazingira na kuahidi kuwa wakichaguliwa watagawa mitungi ya gesi kilo 20 bure kwa wananchi kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya kutunza mazingira.

Amesema gesi itasaidia katika utunzaji wa mazingira kwa wananchi kuacha kutumia nishati kama mkaa na kuni, hivyo kila nyumba itapatiwa mtungi wa gesi wa kilo 20 bure, na hilo linawezekana kutokana na Tanzania kuwa na rasilimali nyingi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Ada Tadea Taifa, Salehe Mohamed Msumari, kwa upande wake amesema wakipata ridhaa Serikali yao itawakusanya wasomi na kuwataka wabuni mambo mbalimbali kwa lengo la kutengeneza ajira.

“Haiwezekani vijiti vya meno na vile vya kusafishia masikio tunaagiza kutoka nje. Jambo hilo si sawa, hivyo Ada Tadea itatengeneza vituo ambavyo vitakusanya wasomi, na tutatengeneza ajira kupitia wabunifu hao,” amesema Msumari.