Arusha. Juhudi za Emmanuel Mushi, mkazi wa Kibaha mkoani Pwani, kujinasua katika kifungo cha miaka 20 jela limegonga mwamba kwa mara ya pili.
Mushi alihukumiwa kifungo hicho baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ngono kwa kumuingizia vidole sehemu za siri mtoto wa jirani yake aliyekuwa na umri wa miaka mitatu kwa wakati huo.
Rufani hii iliyokuwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Barke Sehel, Amour Khamis, na Dk Ubena Agatho ni ya pili kutupwa kwa sababu zilizoelezwa udhaifu wa utetezi uliotolewa na mrufani.
“Baada ya kupitia upya utetezi wa mrufani, tunaona kwamba ulikuwa dhaifu sana wa kutia shaka juu ya kesi ya mashtaka, mashahidi wake waliunga mkono ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba mrufani alikamatwa kwa madai ya unyanyasaji mkubwa wa kingono na alijaribu kutatua kesi hiyo nje ya mahakama,” amesema Jaji Sehel.
Hukumu ya rufaa hiyo ya jinai namba 845/2023 ilitolewa Septemba 10, 2025 na nakala ya uamuzi huo imepakiwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Majaji hao walitupilia mbali rufaa hiyo baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi dhidi ya mrufani.
Akizungumzia sababu za kuitupa rufaa hiyo, Jaji Sehel amesema wameona mahakama katika rufani ya kwanza ilizingatia ushahidi wa pande zote mbili, lakini mwishoni haikushawishika na utetezi kuwa shtaka hilo ni la kutengenezewa na kuwa mahakama mbili zilihitimisha kuwa utetezi wa mrufani ulishindwa kuthibitisha madai yake.
“Yote yaliyozingatiwa hapo juu, tumeridhika kwamba kesi ya upande wa mashtaka dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila shaka yoyote. Kwa hiyo rufaa imetupiliwa mbali,” alisema Jaji Sehel.
Mrufani katika utetezi wake, alikana kutenda kosa hilo na kudai kulikuwa na kutokuelewana kati yake na shahidi wa kwanza ambaye ni mama mzazi wa mwathirika.
Alidai shahidi wa kwanza (mama wa mwathirika) alikuwa akimtongoza kimapenzi na alitaka ampe kipande cha ardhi kwa ajili ya kulima, lakini alikataa.
Awali, katika Mahakama ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, mrufani alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ngono kinyume na kifungu cha 138C(1) (a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu,ambapo alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Oktoba 7, 2020 eneo la Kongowe wilayani Kibaha, Pwani Mushi alidaiwa kwa ajili ya kujiridhisha kimapenzi, alimuingizia mtoto huyo wa jirani yake vidole sehemu zake za siri na kumsababishia maumivu.
Mashahidi wa upande wa mashitaka wakiwamo kaka wa mwathirika na mama wa mwathirika waliithibitishia mahakama kuhusu tuhuma dhidi ya mrufani.
Pia, shahidi wa tatu, Charles Kaila, aliyemchunguza mtoto huyo, aliieleza mahakama kuwa aliona uwekundu na michubuko nje ya ukuta wa uke wa mtoto huyo ambaye alikuwa akisikia maumivu kila alipoguswa sehemu za siri.
Katika utetezi wake, Emmanuel licha ya kudai shahidi wa kwanza alikuwa akimtongoza kimapenzi akitaka ampe kipande cha ardhi kwa ajili ya kulima, lakini alikataa.
Emmanuel alikuwa na mashahidi wengine wawili ambao ni Anisue Patrick na Happiness Mushi, walioiambia mahakama kuwa walihusika kujaribu kutatua kesi ya jinai nje ya mahakama.
Walidai shahidi wa kwanza alisisitiza kulipwa Sh5 milioni ili kufuta kesi na kwa kuwa hawakuweza kukusanya fedha hizo kesi ilipelekwa mahakamani.
Mrufani alikuwa na sababu tano ikiwamo nadai kwamba Jaji alikosea kwa kupokea ushahidi wa mashahidi wa pili na nne kinyume na kifungu cha 127 (2) cha Sheria ya Ushahidi, na kuufanya ushahidi huo kukosa thamani ya kumtia mrufani hatiani.
Hoja nyingine ni Jaji alikosea kushikilia hukumu dhidi yake wakati ushahidi wa mashahidi wa kwanza, pili, nne, tano na sita ulikuwa wa ajabu, usiotegemewa.
Pia, Jaji alikosea kuunga mkono hukumu dhidi yake bila kuzingatia ucheleweshaji wa kumkamata mrufani kuanzia Oktoba 7, 2020 hadi Novemba 4,2020.