Bado Watatu – 33 | Mwanaspoti

HAKUMALIZA sentensi yake akaninyooshea mkono wake na kukikunjua kiganja alichokuwa amekifumba. Akanionyesha kitu alichokuwa amekishika.
Kilikuwa funguo ya gari la Shefa!
“Hizi funguo ni za gari la Shefa na nimezikuta ndani ya pochi yako humu chumbani.”
Mshituko nilioupata ulinifanya nitwete kama niliyekuwa nafukuzwa. Kumbe mume wangu aliichukua ile pochi na kuifungua, ndiyo maana niliikuta kitandani wakati mimi mwenyewe niliiweka juu ya stuli.
Mtiririko wa maelezo yake tayari ulishaniweka kwenye hatia. Hata kama baba yangu alinifundisha nizikanushe tuhuma za kumuua Shefa, hapo ningekana nini?
“Ngoja nikwambie. Wewe ni mume wangu, nitakueleza ukweli,” nikamwambia Sufiani huku nikikaa kitandani. Nisingeweza kuendelea kusimama kwa sababu nguvu ziliniishia kabisa.
“Nakusikiliza.”
“Ni kweli Shefa alikuja nyumbani kabla ya kuuawa. Alikuja usiku akanigongea mlango…”
Nikamueleza uongo Sufiani kwamba Shefa alikuwa amelewa sana na hakunieleza alikuwa amefuata nini kwangu.
“Nilimkaribisha sebuleni akalala hapo hapo. Nilijaribu kumuamsha ili aende zake lakini Shefa hakuamka, nikamuacha na kuingia chumbani kulala.”
“Kwanini hukunipigia simu usiku huo na kunifahamisha kuwa Shefa amekuja na amelala hapa nyumbani?” Mume wangu akaniuliza.
“Hapo nakiri kuwa nilifanya kosa.”
“Enhe…baada ya hapo, nini kiliendelea?”
“Niliamka saa kumi alfajiri nikaenda kumtazama sebuleni alipokuwa amelala, sikumkuta. Nikahisi labda alikuwa ameamka na kuamua kwenda zake. Nikatoka ili kuhakikisha kama kweli ameondoka. Nikamkuta ameanguka karibu na mlango wa choo. Nilipomtazama nikaona anatokwa na damu kichwani na karibu yake palikuwa na lile rungu nililokwambia nimelichukua Sahare.”
Nilipofika hapo nilinyamaza nikamtazama Sufiani usoni. Kusema kweli alikuwa amegwaya.
Nikaendelea. “Niligundua kuwa Shefa alikuwa ameshakufa. Nikafanya uchunguzi ili nijue ni nani aliyempiga lile rungu, nikaona lile dirisha limetobolewa tundu kama ambavyo umelikuta. Sasa sijui kama alikuja mwizi akampiga au alikuja mtu mwingine.”
Sufiani alikuwa ameduwaa akinisikiliza. Nikaona akishusha pumzi ndefu kabla ya kuniuliza: “Baada ya hapo ulifanya nini?”
“Kusema kweli niliogopa sana. Shefa alikuwa mume wa mtu na mimi ni mke wa mtu. Baya zaidi, Shefa ameuawa nyumbani kwangu usiku mzito wakati mume wangu hayupo, nitaelewekaje? Nilichofanya hapo ni kuuhifadhi mwili wake stoo pamoja na lile rungu. Siku ya pili yake nikaupakia kwenye gari saa sita usiku nikaenda kuutupa makaburini.”
Wakati namueleza hivyo, mume wangu alikuwa akitikisa kichwa kusikitika.
“Hii habari ni ya siri mume wangu. Sijamueleza mtu yeyote zaidi yako. Naomba unistiri. Najua nimefanya makosa kukuficha lakini hayo yote ni kwa sababu ya woga. Raisa aliniona wakati nautupa mwili wa Shefa lakini alipokuja kuniambia nilikataa nikamwambia sio mimi.”
“Huyu Shefa alifuata nini hapa nyumbani usiku huo?” Sufiani akaniuliza.
“Hakunieleza hasa alichofuata. Kwa vile alikuwa amelewa hatukuweza kuelewana.”
Sufiani alinyamza akatafakari kisha akaniambia.
“Mke wangu sitaki nikufikirie vibaya kwa sababu Shefa alikuwa rafiki yangu lakini nataka nikwambie kuwa umejitia katika matatizo makubwa hasa kwa vile mke wa Shefa ameanza kukushuku. Maelezo yake yanaonyesha kuwa anakushuku wewe. Na baya zaidi unaweza kujikuta ukikabiliwa na kosa la mauaji.”
“Lakini siye mie niliyemuua.”
“Ni nani sasa?”
Nikabetua mabega yangu: “Sijajua mpaka sasa.”
“Huwezi kusema hujui kwa sababu alipouawa mlikuwa pamoja humu ndani!”
“Mimi nilikuwa nimelala chumbani mwangu. Yeye alikuwa sebuleni.”
“Huwezi kuaminika.”
“Labda ni mwizi alivunja dirisha ili aibe, alipomuona akampiga rungu.”
“Sasa huyo mwizi aliiba nini?”
“Hakuwahi kuiba kitu. Baada ya kuona ameua akakimbia.”
“Suala dogo tu linaweza kukukwamisha, hebu fikiria wewe mwenyewe ni kwanini Shefa aache gari nyumba ya tatu halafu aje hapa kwako usiku.”
Sikutegemea kwamba Sufiani angeniuliza swali hilo, nikajibu uongo.
“Aliniambia kuwa gari lake liliisha petroli, akaona aliegeshe kule kule.”
Sufiani akatikisa kichwa kuonyesha kutokubaliana na maelezo yangu lakini hakusema kitu akanyamza kimya.
“Unanifikiria nini mume wangu?” nikamuuliza nilipoona yupo kimya akiwaza.
“Nafikiria endapo utakamatwa utajiteteaje?”
“Ngoja basi nimuite baba, yeye pia anajua habari hizi.”
“Itakuwa vizuri, muite baba yako.”
Hapo hapo nikampigia simu baba.
“Baba naomba uje hapa nyumbani,” nikamwambia.
“Kuna nini?” Sauti ya baba ikauliza kwa wasiwasi.
“Mume wangu amekuja na tulikuwa tunazungumzia lile suala.”
“Suala gani?”
“Si lile la mauaji”
“Kwani imekuwaje?’
Nikamueleza hali iliyotokea pale nyumbani baada ya Sufiani kuliona lile rungu pamoja na funguo za gari la Shefa zilizokuwa kwenye pochi yangu.
Baba aliyaona mazito. Akaniambia:
“Nakuja sasa hivi.”
Nikakata simu. Baada ya nusu saa tu, baba yangu pamoja na mama wakawasili.
Tukakaa sebuleni na kulizungumzia lile suala. Alianza Sufiani. Akaeleza jinsi alivyowasili kutoka Dar na kufikia kwenye msiba wa rafiki yake. Akaeleza maelezo ya shutuma dhidi yangu aliyoyapata kwa mjane wa Shefa.
Sufiani akaendelea kueleza jinsi alivyofika pale nyumbani na kukuta lile tundu kwenye dirisha ambapo nilimueleza kuwa alikuja mwizi akavunja. Akaeleza alivyolikuta lile rungu stoo pamoja na funguo za gari la Shefa alizozikuta kwenye pochi yangu.
Akaeleza jinsi alivyoniuliza pamoja na maelezo niliyompa yaliyoonyesha kuwa Shefa alifika kwangu ambapo aliuawa usiku na mtu asiyejulikana.
Wakati Sufiani akieleza, baba yangu alikuwa ameinamisha kichwa chake huku mara moja moja akinitupia jicho la shutuma.
Baada ya Sufiani kueleza, baba naye akaeleza kivyake:
“Hizo habari sisi tunazo. Mke wako alikuja kutueleza. Sisi tulimwambia mume wako atakapokuja usimfiche kitu, mueleze ukweli. Lakini unajua wanawake ni waoga, ameona akufiche mpaka pale ulipombana ndipo akaona akueleze ukweli. Hilo tukio ni kweli limetokea na sisi lilitushangaza sana. Kusema kweli huyu marehemu rafiki yako hakuwa mtu mzuri.”
“Kwanini baba unasema hivyo?” Sufiani akauliza.
“Si mtu mzuri kwa sababu utakwendaje nyumbani kwa mtu saa sita usiku wakati ukijua huyo rafiki yako unayemfuata hayupo? Sasa tatizo kama hili limetokea, ni nani wa kulaumiwa? Kwa hali ilivyo atalaumiwa mke wako, lakini ukweli ni kuwa mke wako hana kosa.”
“Sisi tunaweza kusema hana kosa lakini hili suala likifika polisi, polisi watamuona ana makosa. Kwa vyovyote vile, yeye ndiye atakayekuwa mtuhumiwa!”
“Polisi pia wanafanya uchunguzi. Wanapokuona una makosa, maana yake wamejiridhisha na uchunguzi wao kuwa una makosa kweli, si vinginevyo. Mimi mwenyewe nimekuwa polisi kwa zaidi ya miaka kumi. Ninazijua vyema kazi za polisi na za kiupelelezi,” baba yangu aliendelea kumwambia Sufiani.
“Sawa baba. Kwa hiyo wewe unaona kwamba mke wangu hana makosa, mwenye makosa ni marehemu?”
“Ndiyo. Marehemu alikuwa rafiki yako na alikuja nyumbani kwako kama rafiki. Kwa bahati mbaya yakatokea yaliyotokea. Hapo utasemaje kuwa mke wako ndiye mwenye makosa?”
“Lakini baba, angalia yale mazingira yenyewe. Shefa amekuja nyumbani kwangu saa sita usiku, ameliegesha gari nyumba ya tatu na sio hapa nyumbani kama kawaida yake. Alikuwa anahofia nini?”
“Ndiyo nikakwambia yeye ndiye mwenye makosa. Angekuwa hai angetueleza alikuwa anahofia nini.”
“Lakini aliniambia kuwa gari lake liliisha mafuta, ndiyo maana aliliacha pale,” nikajitetea.
“Hilo jambo limemtia mashaka mume wako. Anadhani labda Shefa alikuwa hawara yako!”
“Hapana baba, sina mawazo hayo. Hili jambo limeshatokea, mimi nataka tuzungumze tuone tutalitengeza vipi kwa sababu mke wangu ameanza kushukiwa.”
“Anashukiwa kwa kosa gani?”
“Kwa kosa la mauaji.”
“Sasa mimi nakwambia mke wako siye aliyemuua marehemu. Kama polisi watafanya uchunguzi wao, hata wewe unaweza kushukiwa.”
Sufiani akaruka: “Mimi nishukiwe kitu gani wakati tukio hili linatokea sikuwepo?”
“Kama hivyo wewe una shaka na mke wako juu ya uhusiano wake na Shefa aliyeegesha gari nyumba ya tatu na kuja nyumbani kwako saa sita usiku. Inaweza kuchukuliwa kuwa wewe ndiye aliyemuua Shefa baada ya kumfumania nyumbani kwako. Hili jambo liko wazi kabisa. Hao wanaomshuku mke wako hawajui.”
Sufiani aling’aka: “Baba mbona unataka kunitia kwenye hatia? Hili tukio lilipotokea mimi sikuwepo Tanga.”
“Uchunguzi hautazingatia kwamba wewe hukuwepo Tanga. Yatakayozingatiwa ni yale mazingira ya tukio. Unaweza kuonekana labda ulimdanganya mke wako ukajifanya hupo, kumbe unamfanyia uchunguzi.”
Kwanza sikujua ni kwanini baba alikuwa akimwambia mume wangu maneno yale, lakini baadaye niligundua kuwa alimwambia hivyo kihekima kwa vile baba alikuwa akimshuku mume wangu kuhusika na mauaji ya Shefa. Hivyo alimwambia hivyo ili ajue kuwa hata yeye anashukiwa, si mimi peke yangu.
Sufiani baada ya kuambiwa hivyo, ile jazba aliyokuwa nayo ikatulia. Sasa akataka suluhu na baba.
“Hili jambo sasa litawaingiza waliokuwamo na wasiokuwamo. Mimi naamini mimi na mke wangu hatuhusiki, lakini kama tutahusishwa tutahusishwa na binadamu tu.”
“Sufiani mkwe wangu, hebu jaribu kufikiria nani atakuwa amemuua rafiki yako?”
“Mpaka sasa sijajua bado.”
“Hili tatizo linawalenga nyote wawili, wewe na mke wako. Lazima tuambiane ukweli na tutafakari majibu ya kuwambia polisi.”
“Baba wewe umesema umekuwa polisi kwa miaka mingi, hebu tusaidie kimawazo.”
“Kwanza hii lugha ya kumshutumu mke wako ningependa uiache. Ni lazima nyote wawili muwajibike kwa pamoja.” 
“Ndiyo baba, nimekuelewa.”