Chaumma: Hakuna atakayenyanyaswa kwa sababu ya uraia

Kagera. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimewaahidi wananchi mkoani Kagera na maeneo mengine ya mipakani kuwa, kikipata ridhaa ya kuongoza dola, kitahakikisha hakuna raia anayebughudhiwa au kunyanyaswa kwa sababu ya uraia.

Chama hicho kimesema kitaunda Serikali itakayothamini rasilimali watu kwa maendeleo ya Taifa, kama ilivyo kwa mataifa ya China na Marekani, yaliyo mstari wa mbele kujali rasilimali watu kama msingi wa kupiga hatua kimaendeleo.

Ahadi hiyo imetolewa leo, Septemba 19, 2025, na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho, Salum Mwalimu, alipozunngumza na  wakazi wa Nyakanazi, Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera.

Mwalimu ameeleza kusikitishwa na namna ambavyo baadhi ya raia wanaoishi maeneo ya mipakani, hususani Kagera na Kigoma, wanavyonyanyaswa kwa tuhuma za uraia, hali aliyoeleza kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Tunahitaji rasilimali watu katika sekta kama vile kilimo na ufugaji. Nikichukua nchi, hakuna atakayesumbuliwa kwa sababu ya uraia. Kama si Mtanzania tuambie, kama ni Mtanzania tuambie. Watakaoamua kubaki nchini watapewa vitambulisho vya uraia ili wachangie maendeleo ya Taifa,” ameahidi.

Mwalimu akitoa mfano wa raia wa Burundi wanaoishi nchini, amesema haina maana kuwanyima haki au huduma kwa sababu tu ya asili yao.

“Kama mtu anatoka Burundi lakini ameishi hapa, ameanzisha familia, anashabikia hata klabu za hapa, kwanini asipewe nafasi ya kuishi kwa heshima kama wengine?” amehoji.

Kwa mujibu wa Mwalimu, si sahihi kulinda nchi kwa kuwanyima watu vitambulisho vya uraia, bali kupitia uwekezaji kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, kama Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Amesema ni muhimu vyombo hivyo kuimarishwa na kuwa na vifaa vya kisasa.

“Inashangaza kila siku watu wanachokozwa kuhusu uraia wao. Kama mtu ni mwadilifu, anayelipa kodi, mwenye mchango kwa Taifa, kwa nini asiachwe aishi kwa amani? Tukipata madaraka, suala la kusumbuliwa kwa sababu ya uraia litakuwa historia,” amesema mgombea huyo.

Mwalimu anazunguka maeneo mbalimbali nchini kunadi sera za Chaumma ili kuushawishi umma kuchagua chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025. Katika kinyang’anyiro hicho, anachuana na wagombea kutoka vyama 17.