Folz achomoa watatu Angola kikosi cha Dabi 

KOCHA wa Yanga, Romain Folz amefanya mabadiliko ya wachezaji watatu katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambacho kitaivaa Wiliete  ya Angola jioni hii huko Luanda, tofauti na kile ambacho kilianza katika Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, Septemba 16.

Yanga inatupa karata ya kwanza katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikisaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi, hii ni mechi ya kwanza kwa Folz kimataifa akiwa na kikosi hicho ambacho siku chache zilizopita alikiongoza kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba bao 1-0.

Mabadiliko hayo yamegusa maeneo mawili tofauti, moja ni ukuta ambapo ametoa nafasi kwa nahodha mkuu, Bakari  Mwamnyeto kuongoza jahazi akichukua nafasi ya Dickson Job, hivyo atacheza sambamba na Ibrahim Hamad ‘Bacca’.

Eneo lingine ni ushambuliaji ambapo, ameamua kuanza na Clement Mzize badala ya MaxibNzengeli  huku pia akitoa nafasi kwa Mamadou Doumbia badala ya Mudathir Yahya. 

Kikosi kamili kilichoanza; Djigui Diarra, Israel Mwenda,Chadrack Issaka Boka, Bakari Mwamnyeto,Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Aziz Andabwile, Clement Mzize,Duke Abuya, Prince Dube, Mamadou Doumbia na Pacôme Zouzoua.