Gwiji Simba ampa ujanja Yakoub Suleiman

ENDAPO kama kipa wa Simba, Yakoub Suleiman atazingatia ushauri wa mkongwe katika nafasi hiyo, kocha Idd Pazi ‘Father’ basi huenda akairejesha Tanzania One baada ya Aishi Manula kusajiliwa Azam FC.

Pazi aliwahi kuwa kipa Tanzania One enzi akiwa Simba alisema, kipa huyo mpya wa Simba aliyetua kutoka JKT Tanzania anatakiwa kuzingatia mazoezi ya timu na  binafsi yatakayomjenga kujiamini na mbinu pamoja na kujituma vilivyo mazoezi ili kumshawishi kocha Fadlu Davids kumpa nafasi.

“Simba ina historia ya kutoa makipa Tanzania One, kuanzia mimi kisha, nilimwachia Mohammed Mwameja nilimpendekeza asajiliwe kutoka Coastal Union, ambaye naye akamwachia Juma Kaseja, kisha akaja Manula sasa anatakiwa kuiendeleza Yakoub,” alisema Pazi kipa wa kwanza wa Tanzania kucheza soka la kulipwa Sudan na Indonesia miaka ya 1980 aliyeongeza;

“Kaseja nyuma ya kiwango alichokuwa anakionyesha uwanjani, alikuwa anafanya sana mazoezi , alikuwa ananiomba nimfundishe ya binafsi kwa kuangalia mechi alizodaka ili kama kuna mapungufu ayaboreshe.

“Yakoub kiwango chake ndicho kitakachomshawishi kocha awe anampa nafasi ya kumpanga mara kwa mara, anachotakiwa ni ubunifu wake akiwa golini ambao utatokana na mazoezi yake na kujifunza kutoka kwa makipa tofauti.”

Pazi alisema analisema hilo kwa kuzingatia kuwa Simba tayari imeshamwamini Moussa Camarra aliyepo tangu msimu uliopita, aliyewakalisha benchi Manula, Hussein Abel na Ally Salim ambao baadhi wameshaondoka Msimbazi, hivyo ni lazima ajipange kulinda namba yake.

Mkongwe huyo alisema kumpa ushauri huo Yakoub ili aendelee kushika namba moja Stars (Tanzania One), hana maana kwamba Manula zama zake zimeisha itatokana na kile atakachokifanya Azam kwa msimu huu kwa upande wa Abuutwalib Mshery wa Yanga akiona nafasi yake ngumu kupenya kwa kipa namba moja Djigui Diarra aliyemaliza na cleansheets 17 nyuma ya Camara aliyekuwa na 19.

Kwa upande wa Yakoub aliyemaliza msimu uliyopita na cleansheets nane aliwahi kukiri: “Katika makipa namba moja waliyopita Simba nilikuwa namfuatilia Kaseja kwa ujasiri wake.”