Dodoma. Majeruhi wawili kati ya 11 waliokuwa wakipatiwa matibabu baada ya ajali ya basi la abiria na lori iliyotokea Chemba, mkoani Dodoma, wamefariki dunia, hivyo kufanya idadi ya vifo kufikia 11.
Ajali hiyo ilitokea alfajili ya jana, Alhamisi Septemba 18, 2025, na kusababisha vifo vya watu tisa, watano wanaume na wanne wanawake.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi, amesema majeruhi wawili wamepoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu.
“Jana tulipokea majeruhi tisa, baadaye waliletwa wengine wawili waliokuwa wamefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Chemba, kwa bahati mbaya hawa ndio walipoteza maisha,” amesema.
Miongoni mwa waliofikishwa hospitalini, amesema ni mtoto mdogo wa umri wa chini ya mwaka mmoja ambaye ndugu wameshamtambua na kumtaja mama yake kuwa ni miongoni mwa majeruhi tisa waliofikishwa hospitalini akiwa hajitambui.
Awali, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma wa hospitali hiyo, Renatha Mzanje, amesema miongoni mwa waliofariki ni mwanamke anayekadiriwa kuwa na miaka 35.
Kuhusu mtoto, Mzanje amesema: “Wakati anapata ajali alikuwa na mama yake mzazi ambaye amelazwa hapa, lakini bado hali yake siyo nzuri. Ndugu wameshafika na wamemtambua. Kwa sasa anaendelea na matibabu.”
Akitoa taarifa kuhusu ajali hiyo jana, Septemba 18, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, alisema chanzo ni uzembe wa dereva wa lori aliyehama upande wake wa kushoto na kwenda kulia, hali iliyosababisha magari hayo kugongana uso kwa uso.
Endelea kufuatilia Mwananchi