Mwanza. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewaruhusu wananchi walioko nje ya vituo walivyojiandikisha kupiga kura ya urais katika vituo walipo.
Sambamba na hilo, wananchi wametakiwa kuendelea kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea ili kufanya uamuzi sahihi wa kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo na kuboresha maisha yao ya kila siku.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Septemba 19, 2025, na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ilemela, mkoani Mwanza, Herbert Bilia, wakati wa utoaji wa elimu ya mpigakura kwa viongozi wa wafanyabiashara wadogo na vikundi mbalimbali vya kijamii.
Amesema kuwa mara nyingi baadhi ya Watanzania huamini kuwa uchaguzi ni wa watu wachache, hali inayowafanya wasishiriki kikamilifu, na baadaye huishia kulalamikia uongozi.
“Tunawahimiza wananchi wote wajitokeze kushiriki mchakato huu muhimu wa kidemokrasia. Kusikiliza sera za wagombea ni hatua ya kwanza kuelekea kufanya uchaguzi wenye tija kwa jamii,” amesema Bilia.
Ameongeza kuwa kila mwananchi ana nafasi na wajibu wa kuhakikisha anatumia haki yake ya kupiga kura kwa uelewa na uwajibikaji, ili kuchagua viongozi wanaogusa maisha yao moja kwa moja.
“Kuacha mtu mwingine akuchagulie kiongozi bila wewe kushiriki ni hatari, kwani kiongozi ndiye anayehakikisha huduma muhimu kama barabara, bei nafuu ya bidhaa na huduma nyingine za kijamii zinapatikana,” amesema.
Kwa mujibu wa msimamizi huyo, katika Jimbo la Ilemela, wagombea 16 wamejitokeza kuwania nafasi ya ubunge kupitia vyama mbalimbali vya siasa, huku nafasi za udiwani katika kata 17 zikigombewa na wagombea 68 kutoka vyama 17.
Akiwasilisha mada kwa washiriki wa kikao hicho, Ofisa Uchaguzi Ilemela, Shilinde Malyagili, amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2024, wapigakura wanaotarajia kuwa katika vituo tofauti na walivyojiandikisha siku ya uchaguzi wataruhusiwa kupiga kura ya rais.
Amesema watakachotakiwa kufanya ni kuwasilisha maombi kuanzia leo, Septemba 19, hadi Oktoba 2, 2025, saa 10:00 jioni.
Malyagili amesema maombi yanaweza kuwasilishwa kwa kujaza fomu namba 29 katika ofisi za wasimamizi wa uchaguzi au kwa njia ya kielektroniki kupitia tovuti ya INEC.
Ametaja wenye sifa za kuomba kupiga kura hiyo kuwa ni wale waliopo safari ya muda mrefu au biashara, walio masomoni au likizo ya masomo, au waliohamishwa kituo cha kazi au makazi. Sifa n yingine ni wale walioko katika matibabu, waliohukumiwa kifungo kisichozidi miezi sita, kuhamishwa gereza au chuo cha mafunzo, na waliomaliza kutumikia kifungo.
Mshiriki wa kikao hicho, Octavian Maxmillian, Katibu wa Soko la Wilaya ya Ilemela (Kiloleli), amesema ameomba matangazo ya gari yapite mitaa yote kwa angalau siku tatu ili kuhamasisha wananchi waliopo nje ya vituo walivyojiandikisha kuomba kupiga kura ya rais.
Mfanyabiashara wa soko la Kiloleli, Hakimu Abduli, amesema elimu kama hiyo irudiwe tena kabla ya uchaguzi mkuu ili jamii ambayo bado haijafikiwa ipate fursa ya kushiriki.
Naye Martha Wilson, mfanyabiashara wa wilayani humo, amesema wagombea wapewe ushauri, waridhike na matokeo ya uchaguzi ili kuepusha vurugu, na kwamba asiyeshinda arudi nyumbani akajipange kwa uchaguzi mwingine.
Mkazi wa Buzuruga, Rehema Kusana, amesema wasimamizi wa uchaguzi wasiwe wakali, kwani wakati mwingine hata maelekezo wanayoyatoa kwenye semina hayafuatwi ipasavyo.