CRESCENTIUS Magori juzi alitoa kauli ambayo hapa kijiweni tunaamini ndiyo inapaswa kutolewa na kiongozi pindi timu inapopoteza mechi kama ya Jumanne wiki hii dhidi ya Yanga.
Amewataka Wanasimba kuwa na utulivu wa hali ya juu katika kipindi hiki ambacho imetoka kupoteza mechi ya sita mfululizo dhidi ya Yanga na katika mechi hiyo ilifungwa bao 1-0.
Ni kweli inauma, siyo kwa Simba tu, bali shabiki wa timu yoyote ila ambayo inapoteza mechi dhidi ya mtani wake wa jadi mfululizo.
Kwa tabia za timu zetu, kunapotokea mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha kama ilivyo kwa Simba dhidi ya Yanga, mambo ndani huwa siyo mazuri na lazima kutokee mifarakano na mpasuko wa ndani kwa ndani lakini unaweza kuonekana hadi nje.
Hali kama hiyo haiwezi kuisaidia timu na badala yake huwa chanzo cha kufanya vibaya na kusababisha ishindwe kutimiza malengo ambayo imejiwekea katika msimu husika.
Hivyo kijiwe kinampa kongole mapema Mzee Magori kwani kwa sasa ndio mwenyekiti wa Bodi ya Simba, hivyo sauti yake inasikilizwa na kufanyiwa kazi kwa haraka na Wanasimba kuliko mtu miwngine na ukizingatia ni mtu anayeshimika katika timu kabla hata hajapata nafasi hiyo ya uenyekiti wa Bodi ya Simba.
Msimu ndiyo kwanza unaanza na Simba ina kibarua cha kutimiza malengo makubwa ambayo imejiwekea kwa ajili ya msimu wa 2025/2026 ambayo ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu isipokuwa na utulivu na mshikamano, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi hawawezi kuwa sawa kisaikolojia na hilo linaweza kuchangia timu kufanya vibaya katika mashindano inayoshiriki.
Wanasimba wanapaswa kumuelewa Magori na kuungana pamoja kuisapoti timu badala ya kutengeneza makundi hasimu ambayo yatairudisha simu.